Habari

Mwenyezi Mungu kuwa Pamoja na Mja Wake, Sababu na Athari zake

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa Viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

 {هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنْزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنْتُمْ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ }

Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akakaa vyema juu ya enzi. Anayajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayo yatenda.

 

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu tunakuomba umswalie umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

 

Na baada ya Utangulizi huu:

 

Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa karibu na waja wake kunaweza kukawa ni kwa kuwachunga, au kuwasaidia. Kuwachunga kuna maana ya yeye Mtukufu kuvijua vilivyo, Viumbe vyake vyote, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ}

Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho bainisha.

 

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَى ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَى مِن ذَلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ  إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ}

Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong’ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wane wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

 

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ }

Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari.

 

Na ya pili ni: Uwepo wa pamoja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mja wake katika kumsaidia, kukuwafikisha, kumlinda, kumuunga mkono na kumlea. Na amewatengea haya Mitume wake A.S, na Mawalii wake, na Watu wema katika waja wake walio pamoja naye.

     Na hakika Qurani Tukufu imeashiria katika sehemu nyingi Ukaribu huu wa Mja na Mola wake ambao huwa wanaupata Watu Maalumu katika waja wake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na katika hili, maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mitume wake wawili, Mtume Musa A.S, na Haruna A.S, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {اذْهَبْ أَنْتَ وَأَخُوكَ بِآيَاتِي وَلَا تَنِيَا فِي ذِكْرِي * اذْهَبَا إِلَى فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَى * فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَيِّنًا لَعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَى * قَالَا رَبَّنَا إِنَّنَا نَخَافُ أَنْ يَفْرُطَ عَلَيْنَا أَوْ أَنْ يَطْغَى * قَالَ لَا تَخَافَا إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَى}

Nenda, wewe na ndugu yako, pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka. Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri. Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.

 

Na Upamoja huu aliouzungumzia Mtume Musa A.S, pale Watu wake walipodhani kuwa Firauni na Wanajeshi wake wamekwishawazingira, na hakuna kimbilio lolote litakalowaokoa na mabavu yake, mbele yao kuna bahari, na Firauni na Wanajeshi wake wako nyuma yao. Hapo wakapiga kelele wakisema:

 

 {إِنَّا لَمُدْرَكُونَ }

Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!

 

Akajibu Musa A.S, huku akiwa na yakini na Imani ya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba atamsaidia na atamnusuru. Akasema:

{قَالَ كَلَّا إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ}

(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa

 

Na Uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mja Wake S.A.W, wakati wa Hijirah yake ambapo anasema Bwana wetu Abubakari Siddiiq R.A: Nilikuwa na Mtume S.A.W, Pangoni, nikaiangalia miguu ya Washirikina na Nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama mmoja wao angeliangalia miguu angetuona, akasema Mtume S.A.W: Ewe Abubakari: Unapofikiria uwili wetu tambua kwamba watatu wetu ni Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na katika hili, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِلَّا تَنْصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّهَ مَعَنَا فَأَنْزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللَّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ}

Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.

 

Utukutu ulioje anapokuwa Mja pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yoyote atakaekuwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu basi hakuna kioicho dhidi yake, kwa yoyote aliye dhidi yake na yule aliye pamoja naye. Na ili Uwepo wa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu upatikane kwa Mja, anapaswa Mja huyu kuingia katika Milango ya kuelekea katika uwepo huo, na lazima atumie njia itakayopelekea kumwezesha Jambo hili, na miongoni mwa Milango hiyo Muhimu ni: Ni kuifikia Imani kamili ya kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu

Ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَأَنَّ اللَّهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ}

Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na Waumini

 

Na hali ya Imani ni kama alivyoitaja Mtume S.A.W: Ni kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Malaika wake na Vitabu vyake na Mitume wake na Siku ya Mwisho, na Kuamini Qadar, Kheri na Shari yake. Na ukweli wa Imani ni kudhihirika athari zake katika Maadili na Mwenendo wa Mtu na jinsi anavyoishi na Watu, ambapo anasema Mtume S.A.W: Mwislamu ni yule ambaye Watu watasalimika na Ulimi wake na Mikono yake, na Muumini ni yule ambaye Watu watamwamini kwa Maisha na Mali zao.

Na miongoni mwake ni: Ni pale Mja anapofanikisha Uchamungu na Wema wake kwa Watu wote, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إنَّ اللَّهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ}

Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na watendao mema.

 

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ}

Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.

 

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِنَّ اللَّهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ}

Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.

 

Ni kitendo cha kila Mja ambacho kinamridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kujiepusha na kila kinachomuudhi Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni mkusanyiko wa kila jambo la heri. Na Qurani Tukufu imebainisha katia sehemu nyingi, miongoni mwazo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:

{لَيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَى حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ أُولَئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ}

Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.

 

 Anasema Mtume wetu S.A.W: Msihasidiane, msipandishiane bei katika bidhaa zenu, msibughudhiane, msifanyiane vitimbi, na aziuze yoyote katika nyinyi dhidi ya mauzo ya nduguye, na kuweni Waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ndugu, Mwislamu ndugu yake Mwislamu, hamdhulumu, wala hamtupi na wala hamchukii. Uchamungu uko hapa (kifuani).

 

Na anaashiria kifuani kwake mara tatu, inamtosha mja kupata shari yake anapomchukia ndugu yake Mwislamu. Kila Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu ni haramu. Damu yake, Mali yake na Heshima yake.

Na Nguzo ya Ihsani, Mtume S.A.W, ameibainisha vizuri katika Maneno yake yeye mwenyewe aliposema: Ni Kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu kama unamwona, na kama Wewe humuoni basi hakika yeye anakuona.

Na hapo, Mja huifikia kikamilifu hali ya kumchunga Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Yakini kamili kwamba Mola wake Mlezi hamsahau yeye katika hali yake ya Siri na ya Wazi, na katika shughuli zake zote na utulivu wake pia.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {أَلَمْ يَعْلَم بِأَنَّ اللَّهَ يَرَى} .

Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona?

 

Na miongoni mwa njia za kuingia katika Kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni: Uvumilivu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ}

Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.

 

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ * الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ * أُولَئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ}

Na wabashirie wanao subiri, Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.

 

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ}

Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama.

 

Anasema Mtume S.A.W: Na utambue kwamba kukivumilia unachokichukia kuna heri nyingi sana. Na Uvumilivu ni: kuizuia nafsi yako na huzuni, na kuuzuia ulimi usilalamike na kuvizuia viungo na hasira, na hali hii hupatikana kwa kupambana vikali na nafsi, na kufanya hivyo ni kutoa kitu bora zaidi. Anasema Mtume S.A.W: … Na mwenye kujitahidi kuvumilia basi Mwenyezi Mungu Mtukufu humjaalia uvumilivu, na hajapewa mtu kitu bora  na kipana zaidi kuliko uvumilivu.

Na miongoni mwa njia za kukufikisha katika Kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni: Mzinduko wa dhamira yako; kwani Mtu mwenye Dhamira iliyo hai anatambua fika ya Kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu yuko pamoja naye anapokuwa safarini, au anapokuwa pale anapoishi, au anapokuwa peke yake au na watu, na hakuna kinachofichika kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wala hakuna siri yoyote au jambo la wazi linalompita.

 

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mtume Yusufu A.S, pale yule Mwanamke alipoifunga Milango ya nyumba, na akamwandalia mazingira ya kufanyia maasi, na Yusufu A.S, akajikinga kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kipindi chote na ulimi wake ukaanza kukariri na kuisema kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ إِنَّهُ لاَ يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ}

Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi.

 Na hilo ndilo lililotajwa na Mwanamke wa Kiongozi wa Misri kama inavyobainisha Qurani Tukufu kupitia Kauli ya Mwanamke huyo katika Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَقَدْ رَاوَدْتُهُ عَنْ نَفْسِهِ فَاسْتَعْصَمْ}

Na kweli mimi nilimtaka naye akakataa.

  Kuhisi kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni jambo Tukufu mno, na lo ni pale Mja anapokuwa na hofu ya Mola wake Mtukufu Duniani, na akaokoka na adhabu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu Siku ya Kiama. Na katika Hadithi Qudsiy, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Kwa Utukufu wangu mimi sikusanyi kwa mja wangu hofu mbili, na wala simkusanyii usalama wa aina mbili; anaponiamini Duniani, nitamwogopesha Siku ya Kiama, na anapo niogopa Duniani basi mimi nitampatia usalama siku ya Kiama.

Mwanadamu pia anabahatika kuingia katika kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ}

Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru.

 Na anasema Mtume wetu S.A.W: Kwamba anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Hadithi Qudsiy: Mimi niko katika dhana ya Mja wangu kwangu mimi, na Mimi niko nae anaponikumbuka, na iwapo atanitaja Mimi katika nafsi yake nami nitamtaja katika Nafsi yangu. Na akinitaja kwa watu, basi nami nitamtaja katika Watu walio bora zaidi…

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

***

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye pekee asiye na mshirika wake. Na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad, S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu, Mswalie, na umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote mpaka siku ya Mwisho.

Ndugu zangu Waislamu:

Hakika kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuna Athari kubwa ambapo Mja huchuma Matunda yake Duniani na Akhera. Miongoni mwake ni: Kwamba atakaeingia katika kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamponda na kila aina ya Shari na atamwondoshea kila lenye madhara.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ}

Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا}

Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake.

 Kwa maana ya: mwenyekumtosha, Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{أَلَيْسَ اللَّهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ}

Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake?

Na yoyote anayemtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na akamwamini vilivyo na inavyotosha, basi hakuna adui yoyote anaeweza kumdhuru yeye, na anachokitaka hakataliwi na anachokitamani hakitampita. Na tunaposimama katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mtume wetu Musa A.S:

{وَلِتُصْنَعَ عَلَى عَيْنِي}

na ili ulelewe machoni mwangu.

 Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَاصْطَنَعْتُكَ لِنَفْسِي}

Na nimekuteuwa kwa ajili ya nafsi yangu.

 Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu akimwambia Mtume wake S.A.W:

 {وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا}

Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا أَنَّ لَهُمْ قَدَمَ صِدْقٍ عِندَ رَبِّهِمْ}

na wabashirie wale walio amini ya kuwa watakuwa na cheo cha juu kwa Mola wao Mlezi.

Tunaitambua hadhi ya Mola kuwa na Mja, na fadhila zake na athari zake Njema.

Hapana Shaka yoyote kwamba kuingia Kweli katika nafasi ya kuwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwa chini yake ni katika Milango Muhimu mno ya Utulivu wa Mja, na kutulizana kwa moyo na kuwa na afya njema ya nafsi yake, na ni njia ya kujiepusha na kila upande wa ukosefu wa utulivu wa nafsi, Wasiwasi, mgongano wa mawazo, na msongo wa mawazo. Kwani vipi Mja anaweza kuwa na wasiwasi kama atafuata njia sahihi na akatambua ya kwamba jambo lolote liko katika mikono ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na anapoamua kitu husema kuwa na kikawa?.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{قُلِ اللَّهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَنْ تَشَاءُ وَتَنْزِعُ الْمُلْكَ مِمَّنْ تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَنْ تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَنْ تَشَاءُ بِيَدِكَ الْخَيْرُ إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ}

Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye, na humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni Muweza wa kila kitu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{ما يَفْتَحِ اللَّهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا  وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ  وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ}

Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Hakika Waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhisi kuwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuusogeza Utukufu wake katika nyoyo zao, huwafsnikishia wao na Jamii yao viwango vya juu vya daraja la amani na usalama wa kijamii kwani Waja wanapojua kwa uyakinifu Kwamba wao kamwe hawatoweki machoni mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu basi maadili yao hunyooka na Tabia zao zikawa nzuri, wakawa wanafuata maamrisho yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na wanajiepusha na Makatazo yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na wanasimama katika Mipaka yake na wanafanya kazi ili watengeneze Dunia kwa Dini yao. Na kila mmoja wao akawa anaishi kwa amani katika nafsi yake na katika Familia yake na ndugu zake anaowalea yeye, na Majirani zake, wenzake marafiki zake na Jamii yake na Watu wote. Na hiyo ndiyo Risala ya Uislamu aliyokuja nayo Mtume Muhammad, ambaye ni Rehma kwa Viumbe vyote.

Ewe Mola wetu Mtukufu, tunakuomba utuingize katika Wale unaowanusuru na kuwasaidia, na tukauomba utuongezee Fadhila zako, na utupanulie neema zako kwetu, na uturuzuku Nia njema katika mambo yetu yote na Uilinde Nchi yetu na nchi zote Duniani.

Umoja wa Kitaifa ndio Nguvu zake

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا}

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa Viumbe vyote, yeye pekee asiye na mshirika wake. Na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu Mtukufu mswalie, mrehemu, mswalie na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Na baada ya Utangulizi huu.

Hakika Mtume wetu S.A.W, alikuja na Ujumbe unaolingania Umoja na Mjongeleano baina yetu na Ujumbe huo ukazuia Mgawanyiko na Mpasuko baina yetu. Ukawakusanya Waarabu waliokuwa wameparaganyika na kuwafanya wawe Uma mmoja, na Mtume S.A.W, akawafanya wawe ndugu baina yao kwa undugu wa Imani na akazifungamanisha nyoyo zao kwa mfungamanisho wa Kujongeleana na kuzoeana, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ}

Hakika Waumini ni ndugu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ لَوْ أَنْفَقْتَ مَا فِي الأَرْضِ جَمِيعًا مَا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَكِنَّ اللَّهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ}

Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Vilevile Mtume S.A.W, ametuamrisha tupendane na tuhurumiane na kuhisiana huruma, Akasema S.A.W: Mfano wa Waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana na kuhisiana huruma, ni Mfano wa Mwili Mmoja, pindi kiungo kimoja kinapohisi maumivu basi mwili mzima huugulia kwa Kukesha na kwa Homa.

Itambulike kuwa Mjongeleano huu haujaishia kwa Waislamu tu peke yao, bali unajumuisha Watu Wote kwa ujumla. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ}

Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.

Na hivyo ndivyo Qurani Tukufu ilivyothibitisha, pale ilipouzungumzia Undugu wa Kibinadamu baina ya Mitume na Wanaowapinga katika Imani yao, na kwa ajili hiyo, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِلَى عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا}

Na kwa A’adi tulimpeleka ndugu yao, Hud.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِلَى ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا}

Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِلَى مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا}

Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua’ib.

Na baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutaja simulizi za Mitume waliotangulia, amesema:

{وَإِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ}

Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ}

Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.

 قال الإمام البغوي (رحمه الله) : بعث الله الأنبياء كلهم بإقامة الدين ، والألفة والجماعة ، وترك الفرقة والمخالفة .

Jambo ambalo halina shaka yoyote ni kwamba Uislamu kuulingania Umoja na Kukusanyika na kupinga Mgawanyiko na Uchoyo ni moja kati ya sababu muhimu sana za kuilinda nguvu ya Taifa na Amani ya Jamii; kwani mtu yoyote hata kama atakuwa na nguvu kiasi gani lakini katika Jamii nyonge, hakika mtu huyo ataendelea kuwa mnyonge tu, na pia upande mwingine, Mtu yoyote anapokuwa mnyonge katika Jamii yenye nguvu basi bae atapata nguvu hiyo kutokana na Jamii yake anayoishi ndani yake; na kwa hivyo Uislamu umeinua thamani ya Utaifa, na kusisitiza kuwa Nchi ni ya wote na yeye pia kwao ni wa Wote; kwani Umoja wa Kitaifa unahukumia kutokuwepo Mgawanyiko baina ya wananchi wake kwa misingi ya Dini, Rangi au Jinsia. Mwarabu sio bora kuliko Mwajemi, au Mweupe kuliko Mweusi, au Mweusi kuliko Mweupe isipokuwa kwa Uchamungu, na kufanya Mema. Na kuanzia hapa, ndipo ulipokuwapo ule waraka wa Madina alioupitisha Mtume S.A.W, na Mayahudi wa Madini, ambapo aliwapa Mayahudi haki za Waislamu kama vile: Uhuru, Usalama, na Amani. Na akawawajibisha ndani yake kuwa na Ulinzi wa pamoja wa Mji wa Madina, katika msisitizo mkubwa wa kwamba Nchi ni ya Wote, na inawatosha ikiwa tu kila mmoja atawajibika ipasavyo na kubeba majukumu yake. Uislamu pia, ume8nyanyua juu thamani ya Kazi kwa kushirikiana, na ukaufanya Umoja wa Watu, na kuunganisha Juhudi na kupiga vita tofauti kuwa ni Wajibu wa Uma bila kujali wakati au sehemu, na jambo hili Mwenyezi Mungu Mtukufu ameliamrisha katika Qurani Tukufu ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

  {وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا}

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.

Na anasema Mtume S.A.W:

Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anakuridhieni vitu vitatu na anachukia vitu vitatu; Anakuridhieni yafuatayo: Mumuabudu yeye na wala msimshirikishe yeye na kitu chochote, na mshikamane kwa kamba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu nyote na wala msitengane. Na chukia kwenu vifuatavyo: Usambazaji wa maneno yasemwayo, Kuuliza Maswali mengi, na Upotezaji wa Mali.

Na Mtume S.A.W, ametoa mifano ya Uma katika Umoja wake na Mshikamano wake na kutiana nguvu kwake katika jengo lililo imara, akasema Mtume S.A.W: Muumini na Muumini Mwenzake ni kama Jengo lililo imara; linajiimarisha lenyewe kwa lenyewe. Na akavishikamanisha vidole vyake.

Na Qurani Tukufu imetutolea mifano ya Umoja iliyopelekea kuilinda nchi na Amani ya Jamii, na kutokana na hayo, Mtume wetu Yusuf A.S, pale alipoandaa Mkakati wa uliopangikana watu wote wakashirikiana na wakawa pamoja nyuma ya lengo lao, na wakatekeleza Jambo hili katika uhalisia wakashirikiana na wakawa bega kwa bega kila mmoja kwa uwezo wake kwa mujibu wa Mfumo uliochorwa vyema na kwa Utashi wa lengo lililokusudiwa na hapo ndipo Nchi ilipofanikiwa na kuwa na Maendeleo na Maisha bora na Ulinzi na nguvu za Kiuchumi na Watu wakaja kutoka kila upande ili wapate Kheri zake ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa Kauli ya Mtume wetu Yusufu A.S:

{قَالَ تَزْرَعُونَ سَبْعَ سِنِينَ دَأَبًا فَمَا حَصَدتُّمْ فَذَرُوهُ فِي سُنبُلِهِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّا تَأْكُلُونَ * ثُمَّ يَأْتِي مِن بَعْدِ ذَلِكَ سَبْعٌ شِدَادٌ يَأْكُلْنَ مَا قَدَّمْتُمْ لَهُنَّ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّا تُحْصِنُونَ * ثُمَّ يَأْتِي مِن بَعْدِ ذَلِكَ عَامٌ فِيهِ يُغَاثُ النَّاسُ وَفِيهِ يَعْصِرُونَ}

Akasema: Mtalima miaka saba kwa juhudi. Mtacho vuna kiwacheni katika mashuke yake, isipo kuwa kidogo mtacho kula. Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayo kula kile mlicho iwekea isipo kuwa kidogo mtacho kihifadhi. Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao katika mwaka huo watu watasaidiwa, na watakamua.

Uislamu vilevile umelingania na kuhimiza katika kila jambo linalokuwa sababu ya Umoja wa Kujipanga na Kukusanyika, na ukalingania Rehma, Ulaini,  na Upole, akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَبِمَا رَحْمَةٍ مِنَ اللَّهِ لِنْتَ لَهُمْ وَلَوْ كُنْتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانْفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُتَوَكِّلِينَ}

Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea.

Kwa hivyo, Rehma, Ulaini na Upole, na kuhurumia ni sababu ya Kuungana na kujongeleana kwa nyoyo. Anasema Mtume S.A.W: Hakika Dini ni nyepesi. Na haikazwi na Mtu yoyote isipokuwa isipokuwa itamshinda huyo anayeikaza

 Rekebishane, na msogeleane, na msaidiane (katika safari zenu) kusafiri mwanzoni mwa mchana, au mwisho wa Mchana au sehemu ndogo ya usiku. Amesema Mtume S.A.W: Hakika Mimi nimetumwa ili nije kukamilisha Maadili Mema.

Uislamu pia, umelingania kueneza hali ya kuzoeana na kuwa na Amani baina ya ndugu wa Jamii moja bila kujali tofauti zao za kiitikadi, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَقُولُوا لِلنَّاسِ حُسْنًا}

na semeni na watu kwa wema

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِين}

Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.

Mtume S.A.W, alikuwa anashirikiana na wasio kuwa Waislamu kwa njia hiyo ya Qurani Tukufu, akawa Mtume S.A.W anawatendea wema na anazipokea zawadi zao na anajibu mialiko yao na anawatembelea wagonjwa wao kwa ajili ya kuonesha Usamehevu wa Dini yetu hii na kwa kulinda Umoja wa Jamii na Mshikamano wake.

  Hakika Wajibu wa Wakati na Fiqhi ya Vipaumbele vinawataka wananchi Wote Wenye nia njema na nchi na wenye kuyatambua mazingira ya Kipindi hiki wasimame wote kwa pamoja mpaka wafikie kiwango cha juu cha uchapaji kazi kila mmoja katika nafasi yake. Kwa hiyo watu wa Tiba wafanye wawezavyo kwa ajili ya Nchi yao, na pia Watu wa Sheria wafanye kazi wawezavyo kwa ajili ya nchi yao, na vilevile Watu wa Uhandisi, Watu wa Kilimo, Watu wa Elimu na Bobezi zingine zote na Viwanda kwa ajili ya kustawisha moyo wa Utendaji na Kutoa; na huyu anafanya kazi kwa mikono yake, na yule anatoa mali yake, na huyu anawafundisha Watu, na kwa njia hii, kila mmoja anatumia nguvu zake na Vipaji kwa ajili ya kuitumikia Nchi yake. Na hili ndilo haswa linalotakiwa na Dini yetu Tukufu, ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anatusemesha sisi sote kwa tamko la kutujumuisha na kutukusanya, ambapo hakuna hata mtu mmoja anayetengwa na kubaguliwa katika Kazi na Bidii, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ وَإِلَيْهِ النُّشُورُ }

Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ}

Na itakapo kwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa.

Ninaisema kauli yangu hii na ninajiombea mimi na kukuombeeni nyinyi Msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

*    *     *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa Viumbe vyote, na ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu, mswalie, mrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Ndugu zangu Waislamu.

Hakika Mfuatiliaji mzuri wa Matukio ya Historia atagundua ya kwamba Kugawanyika na Kutofautiana ni moja kati ya sababu za Kushindwa na Kuwa na Unyonge. Na Qurani Tukufu imetutahadharisha na hayo, pale aliposema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَأُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ}

Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ}

wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.

Vilevile mgawanyiko na kutokuwa na kauli moja huondosha nguvu ya Uma na huurithisha Unyonge na Udhaifu, na inatosha kuonywa kuhusu Kugawanyika, kwama Mtu yoyote atakayekufa katika hali hiyo atakuwa amekufa kifo cha kijahiliya (kifo cha zama za kabla ya Uislamu).

Na kwa ajili ya hivyo, Uislamu umepiga vita kila aina ya mwenendo ambao unaweza kuleta mgawanyiko na hitilafu. Kwa hiyo, unauona Uislamu unakataza Ubaguzi ambao ndio athari miongoni mwa athari za kasumba za Kijahiliya (zama za kabla ya Uislamu) zinazotajwa vibaya. Akasema Mtume S.A.W: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amekuondosheeni nyinyi kiburi cha kijaahiliya na majigambo yake kwa Mababu, Muumini mchamungu, na mwovu jeuri, nyinyi ni Kizazi cha Adamu A.S, na Adamu anatokana na Udongo.

Mtume S.A.W, alibainisha pia kwamba Watu Wote ni sawa katika Haki zao na Wajibu wa kila mmoja wao.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Enyi Watu, tambueni kuwa Mola wenu Mlezi ni Mmoja, na Baba yenu ni Mmoja, mtambue ya kwamba Mwarabu sio bora kuliko Mwajemi, na Mwajemi sio bora kuliko Mwarabu, Na wama Mwekundu sio bora kuliko Mweusi, na Mweusi sio bora kuliko Mwekundu, isipokuwa kwa Uchamungu…

Ewe Mola wetu tuunganishe tuwe wamoja, na uzijongeleshe nyoyo zetu, na utuwafikishe kwa yale unayoyaridhia na uturuzuku Nia Njema katika mioyo yetu, kwa Kauli na kwa Vitendo, na uilinde Nchi yetu, na uipeperushe bendera yake Ulimwenguni.

Haki za Vijana na Wajibu wa kila Mmoja wao

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa Viumbe vyote anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آَمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى}

Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye peke yake asiye na mshirika wake. Na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake.Ewe Mola wetu tunakuomba umswalie na umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Na baada ya utangulizi huu:

Hakika kipindi cha Ujana ni katika vipindi Muhimu mno kwa Umri wa Mwanadamu; Ni kipindi cha nguvu za kimwili na ukomavu na uchangamfu, na kutoa, Matumaini Mapana, na kuwa wazi kimaisha. Hapana shaka Kwamba vijana ni Nguzo Kuu ya Uma na ni Moyo wake unaodunda na ni mkono wake wenye nguvu na hakuna yoyote anaeweza kuukana mchango wao muhimu katika ujenzi wa Mataifa na katika Maendeleo ya Uma na Kuimarika kwake.

Na Qurani Tukufu imekielezea kipindi hiki cha Ujana kama ni kipindi cha nguvu kati ya unyonge wa aina mbili, unyonge wa utotoni na unyonge wa Uzeeni. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{اللَّهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْ بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِنْ بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً}

Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe.

Utume na Risala vilikuwa wakati wa umri wa Ujana. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kisa cha Bwana wetu Yusufu A.S:

{وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ}

Na alipo fikilia utu uzima tulimpa hukumu na ilimu. Na kama hivi tunawalipa wanao tenda mema.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Bwana wetu Musa A.S:

{وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَى آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا  وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ}

Na Musa alipo fika utu-uzima baraabara, tulimpa akili na ilimu. Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema.

 Ibnu Abas R.A, amesema: Mwenyezi Mungu Mtukufu hajawahi kumtuma Mtume isipokuwa Kijana, na wala hajawahi kupewa Elimu Mtu isipokuwa akiwa katika umri wa Ujana.

Tunamuona huyu kipenzi cha Mwenyezi Mungu Mtukufu Nabii Ibrahim A.S, alipambana na Watu wanaoyaabudu Masanamu akiwa Kijana. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ}

Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.

Qurani Tukufu vilevile imeashiria juu ya Utambuzi na Akili pevu ya Bwana wetu, Mtume Suleiman A.S, tena akiwa katika kipindi cha Ujana wake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَفَهَّمْنَاهَا سُلَيْمَانَ وَكُلًّا آتَيْنَا حُكْمًا وَعِلْمًا}

Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Musa A.S, alipewa Utume na Mwenyezi Mungu Mtukufu alipokuwa katika kilele cha Ujana wake, nguvu na uaminifu ambavyo vilipelekea Binti wa Mja Mwema wavielezee kwa baba yao, kama isemavyo Qurani Tukufu:

{قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ}

Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amemsemesha Yahya A.S, ili asimame kwa amana ya Elimu na kulibeba jukumu la Ulinganiaji, kwa nguvu zote na azma ya Vijana, akasema:

{يَا يَحْيَى خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا}

Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa hikima angali mtoto.

Na kutokana na umuhimu wa kipindi hiki cha Ujana, Mtume S.A.W, amebainisha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atamuuliza Mja Wake swali maalumu Siku ya Kiama mpaka ajitahidi mtu kunufaika na Ujana wakena kuutumia vizuri kwa manufaa yake na ya Watu wote. Akasema Mtume S.A.W: Miguu ya Mja wangu siku ya Kiama haitapumzika mpaka aulizwe mambo manne; Aulizwe kuhusu Umri wake na ameumalizaje? Ujana wake aliumalizaje? na Mali yake aliichumaje na akaitumiaje? Na Elimu yake aliifanyia nini?

Na Uislamu umewahimiza sana vijana kwa himizo kubwa, na ukawajaalia majukumu, kwani wao wana haki ya kusomeshwa, Kuongozwa na kuandaliwa vizuri. Na Qurani Tukufu imelizungumzia jambo hili kwa yale aliyoyasema Luqmaani mwenye Hekima na Busara alipokuwa na mwanae. Ambapo yeye alipandikiza ndani ya kijana wake pande mbalimbali za Kidini na akamuasa awe mwema na mwenye kujitolea na ajipambe na Maadili mema. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ }

Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّهُ إِنَّ اللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ * يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ * وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ * وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ}

Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote. Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda.

Na hivyo ndivyo alivyokuwa Mtume S.A.W, anafanya anapokuwa na vijana. Akawa Mtume S.A.W, ana hima kwao kwa kiwango kikubwa mno na anapupia katika kuwawezesha kielimu na kuwaandaa vilivyo na alikuwa anapandikiza nyoyoni mwao na katika akili zao Misingi ya Dini Tukufu ya Uislamu na kupenda Elimu na Kujiwekea Sifa maalum. Kutoka kwa Ibnu Abas R.A, amesema: Nilikuwa nyuma ya Mtume S.A.W, Siku moja, akasema: Ewe kijana, mimi ninakufundisha maneno haya; Mlinde Mwenyezi Mungu Mtukufu naye atskulinda. Mlinde Mwenyezi Mungu Mtukufu utamkuta upande wako. Unapoomba basi mwombe Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na unapotaka msaada mwombe Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ujue kwamba kama Uma wote ungelikusanyika ili ukusfae kwa kitu chochote usingeliweza kukufaa isipokuwa kwa kitu alichokuandikia Mwenyezi Mungu Mtukufu na kama wangelikusanyika ili wakudhuru kwa kitu chochote wasingeliweza kukudhuru isipokuwa kwa kitu alichokuandikia Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kalamu zimekwisha nyanyuliwa, na vitabu vimekwisha kauka.

Na baada ya Elimu bora na Mafunzo yaliyokamilika, inafuatia haki ya vijana katika kuwawezesha na kuwapa msukumo – kila mmoja kwa mujibu wa uwezo na Sifa alizonazo – katika maeneo ya kazi au Uongozi na Majukumu. Na hivi ndivyo Mtume S.A.W, alivyofanya ampo aliwaajiri vijana wenye nguvu mbali mbali. Na akawasukuma ili waingie katika vita vya maisha; Mtume S.A.W, alimwamini kijana wakati wa Ulinganiaji wake, ambae Umri wake hauzidi miaka ishirini, nae ni Arqam R.A, ambae nyumba yake ilikuwa Makao Makuu yenye Usalama kwa Mtume S.A.W, na Maswahaba wake mwanzoni mwa Ulinganiaji wa Uislamu. Mtume vilevile, alimpa uongozi wa Jeshi la Waislamu, Usama bin Zaid R.A, na Umri wake Wakati huo ukiwa haujavuka miaka kumi na nane.

Omar bin Khatwab R.A, alikuwa akiwaita vijana katika makao yake pamoja na wazee katika kila jambo, na anasema: Hakatazwi yoyote miongoni mwenu kwa udogo wa Umri wake kutoa maoni yake, kwani hakika ya Elimu haimo kwa wadogo wala kwa wakubwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anaiweka atakapo. Na kwa hivyo katika Makao yake walikuwapo vijana akiwamo Abdullahi bin Abas R.A, ambaye Omar R.A, alikuwa akimzungumzia kwa kusema: Hakika Kijana huyu ana ulimi wenye kujitambua na moyo wenye akili.

Na jambo hili halijawahi kuishia kwa vijana wa kiume tu, bali na wa kike pia wana mchango wao usiopingika wa Ujenzi wa Ustaarabu wa Kiislamu, wao walikuwa na mchango wao Wakati wa amani na wakati wa vita. Miongoni mwao ni Bi Asmaa Binti Abuu Bakar Sidiiq, R.A, na mchango wake wa wazi katika Hijra ya Mtume S.A.W, na baba yake R.A, ambapo yeye Asmaa alikuwa anawaandalia chakula na vinywaji  Mtume na Baba yake Abu Bakar Wakati wa Hijra tukufu, bali wanawake walikuwa na mchango katika nyakati nzito na ngumu kuliko zote. Na Katika viwanja vya mapigano, Wanawake walikuwa wakiwanywesha maji wapiganaji na wakitoa huduma ya kwanza kwa wenye kujeruhiwa, na katika hilo ni kama ilivyokuwa katika siku ya vita vya Uhudi. Anasema Anas R.A: Nilimwona Aisha binti Abu Bakar R.A, na Umu Sula8m wakisambaza viriba vya maji migongoni mwao kisha wanavimaliza kwa kuwagawia watu maji hayo kisha wakarejea tena na kuvijaza viriba hivyo kisha kuja navyo na kuwagawia watu maji.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na nyinyi.

* * *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa Viumbe vyote, na ninashudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake asiye na mshirika wake, na ninashudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu mswalie, marehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Ndugu zangu Waislamu:

Hakika vijana wana majukumu mengi. Na la Kwanza: Kujiimarisha kielimu na kitamaduni, pamoja na kuendeleza kujielimisha huko kwani Elimu daima inasonga mbele kila dakika na hapana budi kwa vijana wetu kwenda sambamba na maendeleo na matukio ya Ulimwengu huu na kuchunga mahitaji ya soko la kazi, na mahitaji ya taifa, na kwa hivyo kujiongezea elimu kwa njia za mipango ya masomo na mafunzo na zoefu zinazohitajika mpaka vijana hawa wawe na uwezo wa kupambana na changamoto zilizopo. Na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hakumuamrisha Mtume wake S.A.W, kujiongezea chochote katika vitu vya duniani isipokuwa Elimu ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu, akimwambia Mtume wake S.A.W:

{وَقُلْ رَبِّ زِدْنِي عِلْمًا}

Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie ilimu

Tatu: Kujihimiza katika kunufaika na zoefu mbali mbali na kujihadhari na kudanganyika. Vijana wanapaswa wanufaike na hekima na uzoefu wa watangulizi wao wenye uzoefu kwani uhusiano baina ya vizazi vinavyofuatana sio uhusiano wa kupuuziana au kukinzana; bali ni uhusiano wa kushirikiana kikamilifu na Kunasihiana, na vijana wetu wajihadhari na majivuno ambayo huwa yanabomoa na wala hayajengi, bali humuangamiza muhusika. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kitabu chake Kitakatifu:

{وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولً}

Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.

Anasema Mtume wetu S.A.W: Mambo matatu huangamiza: Uchoyo wenye kunyenyekewa, na matamanio ya nafsi yanayofuatwa, na mtu kupendezwa mno na maoni yake, kupindukia.

Tatu: Kuweka nia upya kwa ajili ta kuitumikia Dini na Nchi. Mwanadamu hulipwa kwa mujibu wa Uzuri wa nia yake katika Kazi yake, na ukweli wa nia yake. Anasema Mtume S.A.W: Hakika matendo hutokana na Nia, na kila Mtu hukipata kile alichokinuia…

Nne: Ni Kuitumia fursa kwa kuongeza juhudi zaidi na kutambua kuwa Njia ni ndefu na Amana ni Nzito sana, kwa kuwa sisi tunaishi katika jamii inayoendelea kwa kasi kubwa mno na hakuna nafasi ya kwa wale wasio na bidii na wasiozijali kazi zao, na hasa katika kutekeleza kazi walizopewa wazitekeleze. Ili tuweze kufanikisha matarajio yetu na kuifikia nafasi yetu, ambayo sisi wenyewe tunaitarajia na kwa ajili ya taifa letu hapana budi tujitume kwa nguvu zote na juhudi zetu kwa mapana zaidi katika Kazi Zeru.

Tano: Kuurejesha wema kwa Taifa ambalo limetulea na sisi tukakulia ndani yake likatusomesha na kutuwezesha; Taifa lina haki kwa wananchi wake ambao wameishi ndani yake na wakalelewa na kujipatia uzoefu wake na wana wao ndani ya Taifa hilo kumbukumbu na historia zao na iwe nguvu yetu ni kuwa na msimamo na kuwa na nia isiyotetereka, na silaha yetu iwe Elimu na Ubunifu, na kauli mbiu yetu iwe Uzalendo na Kujitolea; kwa ajili ya kulitumikia taifa letu hili na kulilinda.

Ewe Mola wetu Mlezi wabariki vijana wetu, na uwalinde na kila ovu, na uwawafikishe katika Ujenzi na Uimarishaji wa nchi, na uwaongoze katika mambo yenye masilahi kwa Nchi yao na kwa. Watu wake, na Uilinde Nchi yetu na nchi zote Duniani.

 

Uma wa Soma, ni Uma wa kutekeleza Majukumu yake Ipasavyo Baina ya Wanachuoni wa Uma na Wanachuoni wa Fitina

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa Viumbe vyote anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ}

Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili.

Na ninashuhudia ya kuwa hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, aliye peke yake na wala hana mshirika wake, na ninashuhudia ya kuwa Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu, tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Na baada ya Utangulizi huu:

Uislamu umehimiza utafutaji wa Elimu na umehikiza pia bidii na jitihada katika kujipatia hiyo Elimu, na hakuna dalili bora zaidi kuliko aya ya kwanza kuteremshwa katika Quran tukufu nalo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ * خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ * اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ * الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ * عَلَّمَ الْإِنْسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ}

Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.

Kwa hiyo amri ya Kwanza ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyoteremshwa katika Wahyi ni Kusoma ambako ndio mlango wa kwanza katika milango ya Elimu. Kisha baada ya hapo ikaja ishara ya kalamu ambayo ndiyo njia ya kuandikia Elimu na kuinukulu kwake. Na katika hili kuna msisitizo kwa Watu wote juu ya ubainishaji

Hakika ya Wanachuoni Wakweli wa Uma huu, wautumia Wakati wao wote na juhudi zao, na wakatuletea Elimu yao wakiitumikia Dini na Nchi yao, na wakawapitisha Watu njia ya Ukati na Uuwiano, Usamehevu na Huruma, na Ulinganiaji wao ukaleta Matunda makubwa yenye manufaa kwa vizazi na vizazi, vizazi vinavyojenga na wala havibomoi, vinatengeneza na haviharibu, vinayaweka juu Maadili ya Kibinadamu, na kuinyanyua juu Heshima ya Mwanadamu, na amani na usalama. Na hii ndio Elimu yenye manufaa ambayo inakuwa akiba kwa mwenye nayo anapofariki. Anasema Mtume wetu S.A.W: Mtu anapofariki, matendo yake yote hukatika usipokuwa Mambo Matatu: Sadaka endelevu, ay Elimu inayowanufaisha Watu, au Mtoto Mwema atakayemwombea.

Na Mtume S.A.W: alikuwa anamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amuepushe na Elimu isiyokuwa na Manufaa, na wala haijengi wala haifundishi maadili na mwenendo Mzuri, na Mtume S.A.W, alikuwa anasema: Muombeni Mwenyezi Mungu Mtukufu, akupeni Elimu yenye manufaa, na mjikinge kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Elimu isiyokuwa na Manufaa.

Na moja ya Dua zake Mtume S.A.W: Ewe Mola wangu ninajikinga kwako na Elimu isiyokuwa na Manufaa, na Moyo usio kuwa na uchamungu, na nafsi isiyotosheka, na Dua isiyojibiwa.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni na nyinyi.

* * *

Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mola Mlezi wa Viumbe vyote. Na ninashuhudia ya kuwa hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, aliye peke yake na wala hana mshirika wake, na ninashuhudia ya kuwa Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu, tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote, na kila atakaewafuata kwa Wema mpaka Siku ya Mwisho.

Ndugu zangu Waislamu.

Hakika Wanachuoni wenye moyo msafi ndio watu wa Mwongozo Mwema, Mwenendo Mwema, na Nia njema na Uuwianifu, Watu ambao wanaibeba bendera ya Ukati katika kila zama na wanaiepusha Dini Tukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Uvurugaji wa Wenye misimamo mikali, na tafsiri potofu pamoja na kuwaiga wapotoshaji.

Kwa upande wa Wanachuoni wa Fitina ambao wameifanya Dini kama njia ya kuyafikia malengo yao na kufikia wanayoyakusudia, basi hao ndio waliothubutu dhidi ya Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na wakarusha makombora ya Fatwa ambayo yanadhuru na wala hayanufaishi, na yanawagawa watu na wala hayawaunganishi, na yanabomoa na wala hayajengi, na yanaufungulia Uma mlango wa kukufurisha ambao Uislamu umetutahadharisha tusiuingie mlango huo. Anasema Mtume S.A.W: Mtu yoyote atakaemwambia nduguye: Ewe Kafiri, basi mmoja wao atakuwa katika hali hiyo, ikiwa kama alivyosema ni vizuri, ni ikiwa kinyume na alivyosema basi kauli hiyo itamrejea yeye mwenyewe.

Wanachuoni wa Fitna wameufanya Ukali wa kutoa Fatwa, Ubishi Kuwabana watu, kama ni Mfumo wao; na huu ni Mfumo ulio mbali sana na Uislamu wenye Usamehevu na Ukati wa Mambo. Uislamu umewaondoshea Watu kila aina ya Uzito na ukawaowekea mbali aina zote za Ugumu wa Mambo.

Ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ}

Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini.

Na anasema Mtume S.A.W: Peaneni habari njema na wala msipeane habari mbaya, na mrahishiane na wala msisababishiane uzito.

Kwa hiyo ukali wa kutoa Fatwa unakwenda kinyume na Ukati wa Uislamu wenye Usamehevu na ambao Dini Tukufu ya Uislamu inajipambanua kwayo. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَكَذَلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ}

a vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu…

Na Ukati una maana ya Uadilifu, Uwastani na kujiepusha na Kujikweza ambako ni sababu ya kuangamia kwa Mataifa. Mtume S.A.W, anasema: Enyi Watu, jiepusheni na kujikweza katika Dini, hakika mambo yalivyo, huko kujikweza katika Dini kuliwaangamiza waliokuwa kabla yenu.

Na amesema Sufiyani Thauriy R.A: Hakika elimu kwetu sisi ni kibali cha Fiqhi na ama ukali katika Dini kila mmoja wetu anauweza vizuri sana.

Na wanaoandamana na Wanachuoni wa Fitna ni Wanachuoni wa kupotosha wanaozungumza bila ya kuwa na Elimu, na wala hawajazinduka na kuijua haja ya Uma ya kufuata njia bora kabisa a za maendeleo na hawajatambua ya kwamba Ujenzi wa Dunia ni katika Malengo Makuu ya Dini zote, na kwamba Watu hawataiheshimu Dini yetu kama hatutafanikiwa katika Dunia yetu. Na tukifanikiwa katika Dunia yetu basi watu wataiheshimu Dini na Dunia yetu kisha akawarahisishia wale wasioutambua hivyo, Mawaidha kwa ajili ya tahadhari ya wazi kutokan na Dunia yao kwa kuwasababishia wengi katika Watu kuangukia katika Ufahamu wenye Makosa wa Uhusiano wa Dini na Dunia na Umuhimu wa kutumia njia za mafanikio, wakaelewa maana potofu ya kuupa nyongo Ulimwengu Kwamba eti ni kujitenga kabisa na Maisha, na huku wakiwa wameghafilika na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu anayosema:

{رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ}

Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto

Hakika sisi tunasisitiza kwamba uthubutu wa kutoa Fatwa kwa wasio kuwa na sifa ya kufanya hivyo Kielimu ni upotofu na upotoshaji. Wingu ulioje wa Fatwa zilizotolewa bila ya Elimu na kusababisha madhara makubwa sana kwa Maisha ya watu. Kutoka kwa Jabir bin Abdillah R.A, amesema: Tulikuwa safarini na mmoja wetu akaumizwa na jiwe lililompiga kichwani na likamuumiza, kisha akaota ndoto ya kuingilia mwanamke, na akawauliza wenzake: Je mnaniruhusu nitayamamu? Wakasema: Hatuwezi kukuruhusu wakati Wewe una uwezo wa kuoga, basi mtu yule akaoga na akafa. Na tilipofika kwa Mtume S.A.W, tukamweleza juu ya tukio lile, na akasema: Wamemuua, na Mwenyezi Mungu atawaua. Kwanini wasiulize wasichokijua, kwani hakika mambo yalivyo, tiba ya ujinga ni kuuliza, ilimtosha mtu yule Kutayamamu na kukamua kidonda chake, au akafunga kitambaa juu ya jeraha lake kisha akapangusa juu yake na akaosha sehemu ya mwili iliyobakia. Haja iliyoje kwa kila mmoja wetu kufuata ubobezi wake, na ajitahidi katika yale anayoyaweza vizuri, kwa ajili ya kumwogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa ajili ya kuiheshimu Elimu, na kwa kuijali hatari ya Neno. Ni maneno mangapi yaliyosemwa na mtu bila ya Elimu, na ikawa sababu ya uharibifu, maangamizi, na Ufisadi. Kwani kunyamaza ni bora zaidi kuliko kuzungumza maneno yanayosababisha madhara kuliko kunufaisha, na kama mtu asiyejua angenyamaza basi pasingelikuwapo hitilafu. Mtume wetu Muhammad S.A.W, anasema: …na anaemwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu na Siku ya Mwisho basi na aseme maneno mazuri au anyamaze.

Ewe Mola wetu tunakuomba utuoneshe Ukweli na uturuzuku kuufuata, na utuoneshe batili na uturuzuku jinsi ya kujiepusha, na utufundishe mambo yanayotunufaisha na utunufaishe kwa uliyotufundisha, na utuzidishie Elimu, na uilinde nchi yetu na nchi zote Duniani.