Urafiki na Athari zake katika Kuujenga Utu

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{الْأَخِلَّاءُ يَوْمَئِذٍ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ إِلَّا الْمُتَّقِينَ}

Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui  wao kwa wao isipokuwa wachamungu.

 Na ninashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, peke yake asiye na mshirika wake, na ninashuhudia kuwa Bwana Wetu na Mtume wetu Muhammad S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mswalie, marehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake na kila mwenyekuufuata mwongozo wake kwa wema mpaka siku ya mwisho.

Na baada ya utangulizi huu,

Hakika mwanadamu ni kiumbe wa kijamii kimaumbile, na anaishi maisha ya kijamii anaathirika kwayo na anaambatana nayo kupitia alama zake zinazotofautiana na wengine, kwa hakika kukaa pamoja na kulinganisha kuna athari zake za wazi zenye nguvu katika fikra ya mwanadamu na mwenendo wake na ni sababu ya kuainisha mwelekeo wake na furaha yake Duniani na Akhera.

Na wala hakuna hitilafu yoyote kwamba sisi tunahitaji utu ulio sawa na wenye maana za juu ya utu huo, na daraja za juu za kitaifa, ili tuweze kutoa kizazi kinachojenga na wala sio kubomoa, na kinachoyatanguliza masilahi makuu ya taifa juu ya masilahi mengine yoyote. Na sheria ya Uislamu imeamrisha ujenzi mzuri wa utu ili mtu awe na mwamko  akayatambua mambo ya hatari na akawa mbora wa kupambana na mazito ya maisha, na kuziogopa fitna na mambo yenye utata. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً }

 Na jikingeni na Fitna ambayo haitowasibu walio dhulumu peke yao kati yenu

Sheria pia imeelekeza mtu awe na utu wa kujiamini, sio kusitasita, utu ambao unatambua usawa wenye manufaa, na unafuata haki, na wala hauingii katika magomvi na wagomvi. Anasema Mtume S.A.W: Msiwe bendera fuata upepo; mkawa mnasema: Watu wakifanya vizuri na sisi tutafanya vizuri, na wakidhulumu nasi tutadhulumu. Bali bali zitulizeni nyoyo zenu, iwapo watu watafanya vizuri nanyi mfanye, na wakipotoka msizidhulumu nafsi zenu. Na hapana shaka kwamba katika mambo muhimu ambayo yana athari kubwa katika ujenzi wa utu wa mtu ni urafiki. Mtu huathiriwa na yule anaekaa nae na humuiga kifika, kiakida, kimwenendo na kikazi. Na hili limewekwa wazi na Sheria, Akili, Uzoefu, na Uhalisia pamoja na kuona.na urafiki mzuri una umuhimu wake mkubwa katika kuujenga utu wetu ulio sawa, wenye manufaa kwa dini yake na nchi na jamii yake. Na hivi ndivyo Mtume S.A.W alivyowalea Maswahaba wake R.A, akiwemo mwanzoni kabisa, Bwana wetu Abu Bakar Swiddiiq R.A, ambaye alipigiwa mifano bora wa urafiki mwema na jinsi alivyoupa haki yake, na hili lilitokea pale alipoambiwa na watu Makka: Hakika rafiki yako anadai kuwa alipelekwa Usiku hadi Nyumba tukufu ya Maqdis, kisha akarejea, akasema akiwa anajiamini na akiwa na yakini juu ya rafiki yake S.A.W, ikiwa yeye amesema hivyo basi amesema kweli; mimi ninamwamini kwa yaliyo makubwa kuliko hayo, nimawamini katika habari za Mbingu.

Na hivi ndivyo walivyokuwa wakifanya Maswahaba wa Mtume S.A.W, wao kwa wao. Nao ni mfano bora wa kuigwa katika Urafiki mwema na mzuri unaojengeka kwa undugu, kujaliana, uzalendo na umoja, pamoja na kufanya kazi nzuri inayonufaisha, na kupendana na kuhurumiana. Kutoka kwa Nuumani bin Bashiir R.A, anasema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu S.A.W: Mfano wa Waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao, ni kama mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana ni kama mwili mmoja; kiungo kimoja kinapolalamikia maumivu basi mwili mzima huugulia kwa kukesha na kwa homa. Vile vile Urafiki na watu wema,Baraka zake na fadhila zake hupatikana Duniani na Akhera. Anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakika ana Mwenyezi Mungu Mtukufu na Malaika wake waendao kwa kasi fadhila wanavifuatilia vikao vinavyotajwa Mwenyezi Mungu ndani yake, na wanapokuta kikao ndani yake kuna utajo wa Mwenyezi Mungu, huketi pamoja nao, na huwafunika wao kwa wao kwa mabawa yao, mpaka wakaijaza sehemu iliyo baina yao na umbingu wa Dunia, na wanapotawanyika, hupanda juu hadi mbinguni. Akasema: Na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwauliza hali ya kuwa yeye anajua yaliyotokea: Mmekuja kutoka wapi? Watasema: tumekuja kutoka kwa waja wako Duniani, wanakusabihi, na wanatolea takbiir, na wanatamka hakuna mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wanasema sifa zote njema ni zako na wanakuomba. Anasema Mwenyezi Mungu: Wananiomba kitu gani? Watasema: wanakuomba Pepo yako, atasema: Na je wao wameiona Pepo yangu? Watasema: Hapana. Hawajaiona. Atasema: Inakuwaje kama wangeiona Pepo yangu? Watasema: na wanakuomba uwaepushe. Atasema: wanataka niwaepushe na kitu gani? Watasema: Uwaepushe na Moto wako ewe Mola Mlezi.atasema: Je wameuona Moto wangu? Watasema: Hapana. Atasema: Je itakuwaje kama wangeliuona Moto wangu? Watasema: Na wanakuomba msamaha wako, akasema: anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakika nimewasamehe wao, na nimewapa wanachokiomba, na nimewakinga na kile walichoomba kukingwa nacho. Akasema: watasema: Ewe Mola wetu Mlezi: ndani kuna Fulani ambaye ni mja mwenye kufanya makosa kwa wingi, hakika mambo yalivyo alipita na kuketi nao, anasema: atasema Mwenyezi Mungu: Naye pia nimemsamehe, wao ni watu ambao hawi mwovu mwenye kukaa nao.

Na katika matunda ya urafiki mwema ni kwamba urafiki huo ni sababu ya kupendwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na kufuzu pepo yake. Kutoka kwa Abu Huraira R.A, kutoka kwa Mtume S.A.W, amesema: Mtu mmoja alimtembelea nduguye katika kijiji kingine, Mwenyezi Mungu akampelekea malaika wa kumfuatilia katika safari yake, alipofika kwa huyo mtu akamuuliza: Unaelekea wapi? Yule mtu akajibu: ninaelekea kijijini kwa ndugu yangu, akasema: Je wewe una neema yoyote unayoifuata kwake? Akasema: Hapana. Mimi ninampenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akasema: Hakika mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwako, kwamba Mwenyezi Mungu amekupenda kama ulivyompenda nduguyo

Na vile vile urafiki huwa ni sababu ya kufufuliwa pamoja Siku ya Kiama. Kutoka kwa Anas bin Malik R.A, anasema: Kwamba Mtu mmoja alimuuliza Mtume S.A.W, kuhusu Kiama, akasema: Kiama kitakuwa lini? Mtume S.A.W akasema: Umekiandalia kitu gani? Akasema: Sijakiandalia kitu chochote. Isipokuwa mimi ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W.  akasema: Basi wewe utakuwa na wale uliowapenda. Anasema Anas: Hatujawahi kufurahia kitu kama tulivyoifurahia kauli hii ya Mtume S.A.W: “Wewe utakuwa na wale unaowapenda”. Akasema Anas: Mimi ninampenda Mtume S.A.W, na Abu Bakar na Omar, na ninatarajia niwe nao kutokana na penzi langu kwao, hata kama sikufanya mfano wa matendo yao.

Anasema Imamu Shafi katika Shairi lake:

Ninawapenda wema na mimi si miongoni mwao

Huwenda nikapata uombezi kutoka kwao

Na ninamchukia ambaye biashara yake ni maasi

Hata kama tunamiliki bidhaa zinazofanana

Na vile vile katika matunda ya urafiki wa wema ni kwamba urafiki huo hukumbusha kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na huzaa matunda Duniani na Akhera.

Kutoka kwa bin Abas R.A, amesema: Palisemwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni wepi wazuri katika wale tunaokaa nao? Akasema: ni yule ambaye kumuona kwake hukukumbusheni Mwenyezi Mungu na huongeza uelewa katika elimu mliyonayo, na matendo yake hukukumbusheni Akhera.

Na rafiki wa kweli ni kioo cha ndugu yake, humhimiza kufanya kheri, na humkataza ya shari, na humpendelea yale anayoyapendelea kwa ajili ya nafsi yake.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَالْعَصْرِ * إِنَّ الْإِنْسَانَ لَفِي خُسْرٍ * إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ}

Naapa kwa zama. Hakika binadamu bila ya shaka yumo katika khasara, ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri.

Na kutoka kwa Anas R.A, kutoka kwa Mtume S.A.W anasema: Mnusuru nduguyo aliyedhululmu au aliyedhulumiwa. Tukasema sisi kumwambia Mtume: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nitamnusuru akiwa amedhulumiwa, ni vipi ninaweza kumnusuru akiwa ni mwenye kudhulumu? Akaasema: Unamzuia asidhulumu; na huko ndiko kumnusuru kwenyewe. Na hivi ndivyo alivyofanya Rafiki Mwema ambaye alimkuta rafiki yake akienda kinyume na haki, na anakengeuka kwa kumfuata Shetani na Matamanio yake, akamnasihi na kumbainishia haki na akamuusia yanayotakiwa ayafanye na kumuonya kuhusu  mwisho mbaya wa kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {قَالَ لَهُ صَاحِبُهُ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا * لَّكِنَّا هُوَ اللَّهُ رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِرَبِّي أَحَدًا * وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاءَ اللَّهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّهِ إِن تَرَنِ أَنَا أَقَلَّ مِنكَ مَالًا وَوَلَدًا * فَعَسَى رَبِّي أَن يُؤْتِيَنِ خَيْرًا مِّن جَنَّتِكَ وَيُرْسِلَ عَلَيْهَا حُسْبَانًا مِّنَ السَّمَاءِ فَتُصْبِحَ صَعِيدًا زَلَقًا * أَوْ يُصْبِحَ مَاؤُهَا غَوْرًا فَلَن تَسْتَطِيعَ لَهُ طَلَبًا * وَأُحِيطَ بِثَمَرِهِ فَأَصْبَحَ يُقَلِّبُ كَفَّيْهِ عَلَى مَا أَنفَقَ فِيهَا وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَى عُرُوشِهَا وَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُشْرِكْ بِرَبِّي أَحَدًا}

Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kaamili? Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi. Wala simshirikishi na yeyote. Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe,Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako, naye akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho chako, na kikageuka ardhi tupu inayo teleza. Au maji yake yakadidimia wala usiweze kuyagundua. Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua pindua viganja vyake, kwa vile alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingeli mshirikisha Mola wangu Mlezi na yeyote!

Anasema Mshairi:

Hakika nduguyo wa kweli ni yule anayekuwa nawe

Na anayejidhuru kwa ajili ya kukunufaisha wewe

Na yule ambaye unapokumbwa na misukosuko

Yeye huyavuruga yake kwa ajili ya kuyatengeneza yako.

Urafiki mwema una athari nzuri zenye manufaa Duniani na Akhera. Urafiki mbaya kwa hakika una athari zinazojitkeza katika utu wako mwovu, angamizi, uliokengeuka, na kwa hivyo madhara yake ni makubwa mno na uvurugaji wake ni wa hali ya juu mno hapa Duniani, na mwisho mbaya siku ya Mwisho; Urafiki mbaya huyaangamiza maadili mema, na hufuta tabia njema, na huwapotosha chipukizi na vijana, na huzorotesha mwenendo wa kazi na husambaza tetesi na kueneza upotofu na fitina kwa watu, na rafiki mwovu huwa anahangaikia kumpotosha rafiki yake kwa imani potovu na fikra angamizi . na Qurani tukufu imetufafanulia hali halisi ya rafiki mwovu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَى بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ * قَالَ قَائِلٌ مِنْهُمْ إِنِّي كَانَ لِي قَرِينٌ * يَقُولُ أَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُصَدِّقِينَ * أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَدِينُونَ * قَالَ هَلْ أَنْتُمْ مُطَّلِعُونَ * فَاطَّلَعَ فَرَآهُ فِي سَوَاءِ الْجَحِيمِ * قَالَ تَاللَّهِ إِنْ كِدْتَ لَتُرْدِينِ * وَلَوْلَا نِعْمَةُ رَبِّي لَكُنْتُ مِنَ الْمُحْضَرِينَ * أَفَمَا نَحْنُ بِمَيِّتِينَ * إِلَّا مَوْتَتَنَا الْأُولَى وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ * إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ * لِمِثْلِ هَذَا فَلْيَعْمَلِ الْعَامِلُونَ}

Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe. Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: hakika mimi nilikuwa na rafiki. Aliyekuwa akiniambia: Hivyo wewe ni katika wanaosadiki. Ati tukishakufa tukawa udongo na mifupa, ndio tutalipwa na kuhesabiwa? Atasema Je! Nyie mnawaona? Basi atachukuliwa amwone katikati ya Jahanamu. Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza. Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa walio hudhuriswha. Je? Sisi hatutakufa, isipokuwa kifo chetu cha kwanza. Wala sisi hatutaadhibiwa. Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa. Kwa mfano wa haya na watende watendao.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَى يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا * يَا وَيْلَتَى لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا * لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا}

Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki! Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shetani ni khaini kwa mwanaadamu.

Na Mtume S.A.W ametulinganishia rafiki mwovu kwamba ni kama muhunzi. Na akasema S.A.W: Hakika mfano wa rafiki mwovu na rafiki mwema wa kukaa naye ni kama mbeba miski na mhunzi. Muuza miski: ima akupake au ununue kutoka kwake, au ujipatie harufu nzuri. na mhunzi: ima azichome moto nguo zako au ujipatie harufu mbaya.

Vile vile, Urafiki mwovu unazingatiwa kama chombo cha kuangamizia,na kuidhulumu nafsi na pia kuwaonea watu maya; na hatari yake kubwa kuliko zote ni yule rafiki anayejaribu kukupitisha kwenye njia ya makundi angamizi yaliyopotoka na kukengeuka ambayo yanalingania kufanya uharibifu na kubomoa pamoja na kufanya ufisadi Duniani, na yule anayejaribu kukupitisha kwenye njia ya madawa ya kulevya na uraibu wake, kwa maneno na mwenendo wake, kwani huyu na yule wote wanamchukua mtu na kupelekea kwenye njia iangamiayo na ipotoshayo na inayopelekea katika kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu Duniani na Akhera.

Ninaisema Kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu na kukuombeeni nyinyi Msahama.

*     *     *

Sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. Na ninashuhudia na kukiri kuwa hakuna mungu mwingine yoyote anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hana mshirika wake, na ninakiri na kushuhudia kuwa Bwana wetu Muhammad na Mtume wetu, ni Mja wake na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu msalie, mrehemu na umbariki yeye, na Jamaa zake, na Maswahaba wake wote, na kila atakayewafuata kwa wema hadi siku ya Malipo.

Ndugu zangu waislamu.

Tunapaswa sisi sote tujihadhari na kuambatana na marafiki waovu na kutochanganyika nao.

Ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّى يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ إِنَّكُمْ إِذًا مِثْلُهُمْ إِنَّ اللَّهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا}

Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya kwamba mnapo sikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli, basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa nanyi mfano wao hao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanaafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannamu,

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّى يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ وَإِمَّا يُنْسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَى مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ}

Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet’ani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu.

Na Mtume wetu S.A.W anasema: Mtu huifuata Dini ya Kipenzi chake, na aangalie mmoja wenu ni nani wakumfanya kipenzi yake.

Na anasema S.A.W: Usimfanye rafiki isipokuwa muumini, na wala asile chakula chako isipokuwa mchamungu. Na kutoka kwa Abdallah bin Masoud R.A, amesema:

Wazingatieni watu kwa waliokaribu nao kwani mtu hawi karibu isipokuwa na yule anayempenda.

Anasema Mshairi;

Unapokuwa na watu basi ambatana na wabora wao

Na wala usiambatane na duni kimaadili ukarejea chini

Usimuulizie mtu bali muulizie rafiki yake

Kwani kila rafiki humfuata anayekuwa naye

Tunalazimika sisi kuhakikisha kuwa ujenzi wa utu kupitia upatikanaji wa urafiki mwema ni jukumu la pamoja; na jamii nzima inapaswa kuwa bega kwa bega, na kila mtu atambue ukubwa wa jukumu hili. Anasema Mtume S.A.W: Nyinyi nyote ni wachunga, na nyote mtaulizwa kuhusu mnachokichunga. Imamu ni mchunga na ataulizwa kwa anachokichunga, na mtu ni mchunga na ataulizwa juu ya nanachokichunga. Na mwanamke ni mchunga katika nyumba ya mume wake na ataulizwa juu ya anachokichunga. Na Mtumishi ni mchunga wa mali ya mwajiri wake na ataulizwa kwa anachokichunga. Tunapaswa sisi sote kuwa na ari ya mapema ya malezi ya chipukizi na vijana na kuwalinda kupitia familia, shule, jamii, msikiti na taasisi nyingine zote za kijamii  zinazotoa elimu na malezi, kielimu na kifikra, na kupitia vyombo vya habari, pamoja na kukusanya juhudi na kushirikiana kikamilifu kwa ajili ya kuwalinda chipukizi na vijana kutokana na fikra zenye mitazamo mikali na makundi danganyifu na angamizi, na kufanya kazi ya kuimarisha uzalendo wa kitaifa, kwani malezi ya watoto wetu na vijana wetu, na kushirikiana nao katika kuwachagua marafiki wazuri ni amana kubwa na ni jukumu zito mno.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَاأَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا}

Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu atamuuliza kila mtu aliyempa jukumu la kuwachunga watu, Je amehifadhi au amepoteza? Mpaka atakapomuuliza mtu Kuhusu watu wa nyumbani kwake.

Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu tunakuomba uturuzuku urafiki mwema, na utujaalie matunda yake ewe Mola wa viumbe vyote..