Maana ya Kuhama baina ya zama zilizotangulia na sasa

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

 {إِلَّا تَنْصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّهَ مَعَنَا فَأَنْزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللَّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ}

Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.

Na ninashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, peke yake asiye na mshirika wake, na ninashuhudia kuwa Bwana Wetu na Mtume wetu Muhammad S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mswalie, marehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake na kila mwenyekuufuata mwongozo wake kwa wema mpaka siku ya Malipo.

Na baada ya utangulizi huu,

Maudhi yalipoongezeka dhidi ya Maswahaba wa Mtume S.A.W, huko Makkah, Mtume aliwaidhinisha Maswahaba mwaka wa tano tangu apewe utume, wahamie Uhabeshi, akisema: Hakika katika Ardhi ya Uhabeshi kuna mfalme asiyemdhulumu yoyote kwake, basi nendeni katika nchi yake, mpaka Mwenyezi Mungu atakapokuleteeni faraja na njia ya kutoka katika hali mliyonayo. Baadhi ya Maswahaba wakatoka na kuelekea Uhabeshi. Mpaka wakafika katika ardhi ya nchi hiyo, na wakaishi katika makazi bora zaidi, na wakiwa katika ujirani mwema, na wakawa na usalama wa Dini yao, na wakamwabudu Mola wao Mlezi, mpaka wakafikiwa na habari ya kwama watu wa Makkah wameingina katika Uislamu, wakaamua kurejea kwa mara nyingine nyumbani kwao. Na walioikuta hali iko tofauti na walivyoisikia, na wakakumbana na maudhi kwa mara nyingine tena, Mtume S.A.W akawaidhinisha tena wahamie Uhabeshi kwa mara ya pili, na katika Wahamiaji wa Uhabeshi alikuwepo Bwana wetu Jafari bin Abi Twalib R.A, katika safu ya mbele.

Makuraishi walipojua kuwa wahamaji hao wako katika amani, heshima na ulinzi pembezoni mwa mfalme mwadilifu, wakataka kuwarejesha kwa mara nyingine, wakamtuma mjumbe wao kwa mfamle Najashi wa uhabeshi wakimtaka awasalimishe kwao, akasema: Hapana kwa kweli, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, sitawasalimisha watu waliokimbilia katika nchi yangu, na wakachagua kuwa pembezoni mwangu na pembezoni mwa wengine, mpaka niwaite na niwasikilize, kisha Jafari bin Abu Twalib akasimama R.A, ili ayarudi madai ya Makuraishi na uzushi wao, akasema: Ewe Mfalme, Sisi tulikuwa watu tunaoabudu masanamu, na tunakula nyamafu na tunahalisha yaliyo haramu, na tunafanya machafu ya uzinzi, na tunaukata undugu, na tunawatendea uovu majirani zetu, na mwenye nguvu katika sisi anamdhulumu mnyonge, tulikuwa hivyo. Mpaka Mwenyezi Mungu Mtukufu akatuletea Mtume miongoni mwetu, tunaijua nasaba yake, ukweli na uaminifu wake, utu wake, akatulingania kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ili tumpwekeshe yeye na tuachane na vile tulivyokuwa tukiviabudu sisi na baba zetu kinyume na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama vile Mawe na Masanamu, na akatuamrisha tuwe wakweli katika maneno yetu na kufikisha amana, na kuunganisha undugu, na kuwa na ujirani mwema, na kujiepusha na yaliyoharamishwa na pia umwagaji damu, na akatuzuia kufanya uzinzi, kusema uongo na kula mali ya yatima, na kuwasingizia uzinifu wanawake wema,, na akatuamrisha tumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake bila kumshirikisha na kitu chochote, na akatuamrisha tuswali, tutoe zaka, na tufunge. Bwana wetu Jafari R.A akazungumzia vitu vingi kuhusu Uislamu kisha akasema: tukamwamini, na tukamfuata kwa yale aliyokuja nayo, tukamwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufuna hatukumshirikisha na kitu chochote, na tukayaharamisha yale aliyotuharamishia, na tukayahalalisha yale aliyotuhalalishia na watu wetu wakatufanyia uadui, wakatuadhibu na wakatufitini ili tuiache dini yetu, waturejeshe katika kuyaabudu masanamu badala ya kumwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu, na tuhalalishe yale tuliokuwa tunayahalisha katika machafu, na walipotutenza nguvu na wakatudhulumu na kutufanyia mazito, na wakatuwekea vizuizi baina yetu na Dini yetu, tuliamua kutoka na kukimbilia katika nchi yako, na tukakuchagua wewe tukawaacha wengine, na tukawa na utashi wa kuwa karibu yako, na tukawa na matumaini ewe Mfalme kwamba hatutadhulumiwa kwako. Mfalme Najashi akasema: Je una chochote katika alivyokuja navyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu? Akamsomea mwanzo wa surat Maryam, Mfalme Najashi akalia mpaka ndevu zake zikaloana kwa machozi, na Maaskofu wake nao pia wakalia pale waliposikia kile walichosomewa katika Qurani Tukufu, kisha Mfalme Najashi akasema: hakika haya, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyokuja nayo Mtume Isa A.S, nendeni, ninaapa sitakusalimisheni kwao kamwe.

Hakika mzingativu wa kina katika Hijra mbili kuelekea Uhabeshi atatambua vyema ya kwamba Kuhama kwa Waislamu wa mwanzo hakukua kutoka katika nchi ya Ukafiri kuelekea katika nchi ya Imani, kwani asili ya jambo hili ni ulinzi wa nchi na kutoziacha chini ya mikono ya Mabeberu au maadui, bali uhamiaji huu wa kuelekea Uhabeshi ulikuwa ni kutoka katika nchi ya hofu na kuelekea katika nchi ya Amani, kwani Mfalme Najashi kwa wakati huo hakuwa mwislamu, lakini alikuwa kiongozi mwadilifu anayewapa usalama watu wanaokuwa karibu yake kwa Dini zao, Mali zao, na Nafsi zao, na kwa ajili hii, anasemwa kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu huinusuru nchi yenye uadilifu hata kama ni ya kikafiri, na huiacha nchi yenye dhuluma hata kama ni ya kiislamu. Kwa hivyo Mlfame anaweza kudumu pamoja na kuwa ni kafiri lakini hawezi kudumu akiwa ni mwenye kudhulumu. Kwa upande wa nchi yenye kudhulumu, haiwezi kudumu hata kama inaongozwa na kiongozi mwislamu.   Na Mtume wetu S.A.W amempa Imamu mwadilifu, naasi ya juu, na cheo kikubwa siku ya Kiama kwa kuwa kwake miongoni mwa watu saba ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafunika na kivuli cha Arshi yake Siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli chake. Kwa hivyo, kwa uadilifu wake jamii yote inatengemaa na kwa ufisadi wa kiongozi, jamii yote inaharibika.

Na pindi Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomwidhinisha Mtume wake S.A.W, kuhamia Madina Munawarah Mtume S.A.W alitoka akiwa anaungwa mkono na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani uhamaji huo ulikuwa mageuzi makubwa mazuri ya kulijenga Dola la Uislamu, na kulifikia lengo la kuishi pamoja na kuwa ndugu, na kuleta umoja,ili Mtume S.A.W afanikiwe kuufikisha ujumbe wa Mola wake Mlezi kwa walimwengu wote, na kwa hayo, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُواْ ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللَّهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُواْ السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللَّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ}

Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.

Na katika mwaka wa Nane wa atangu kuhamia Madina, Mwenyezi Mungu Mtukufu anampa ushindi Mtume wake kwa kuifungua Makkah, ushindi wa wazi. Na watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukfu makundi kwa makundi, na maana ya Hijra inabadilika kutoka katika maana yake finyu na kuelekea katika maana mbali mbali ukaribisho mpana usio na mipaka na ambao unakusanya pande zote za maisha. Baada ya ufunguzi wa Makkah, Hijra ya kutoka katika nchi kuelekea nchi nyingine ilifikia ukingoni baada ya kuwa Uhamaji ni takwa la wakati wa unyonge, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنْفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنْتُمْ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا فَأُولَئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَسَاءَتْ مَصِيرًا}

Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha nao wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo? Basi hao makaazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa.

Hukumu ya Hijra au Uhamaji, ilibadilika baada ya Ufunguzi wa Makkah, kwa tamko lake Mtume S.A.W: Hakuna Hijra baada ya Ufunguzi wa Makkah, lakini kuna Jihadi na Nia.

Na aliposilimu Swafwaan bin Umayyah, akaambiwa huku akiwa katika maeneo ya juu ya Makkah: kwamba Mtu ambaye hakuhama hana Dini, akasema: Sifiki nyumbani kwangu mbapa niende Madina, na akaenda Madina, na kumwendea Bwana wetu Abaas bin Abdul Mutwalib R.A, kisha akaelekea kwa Mtume S.A.W, na akasema: Ni kipi kilichokuleta ewe Abu Wahab? Akasema: inasemekana: kuwa hana Dini asiyehama. Mtume S.A.W akasema: Ewe Abu Wahbi, rejea nyumbani kwako Makkah na kimbilieni katika Dini yenu. Hakika Hijrah imemalizika, lakini Jihadi na Nia bado vipo. Na anasema Mtume S.A.W: Mwislamu ni yule ambaye Waislamu wenzake wamesalimika na Ulimi wake na Mikono yake, na Mhamaji ni yule aliyeyahama yale aliyoyakataza Mwenyezi Mungu Mtukufu.

ingawa uhamaji wa kieneo, kutoka Makkah kwenda Madina umemalizika kwa Ufunguzi wa Makkah, maana zote nzuri za uhamaji bado zinaendelea kuwepo, nazo tunalazimika kuzitilia mkazo. Mtume S.A.W ametuwekea Misingi ya kwamba Uhamaji wa kweli ni mageuzi mazuri kuelekea katika ubora zaidi na uzuri kama vile mageuzi ya kutoka katika Ukosefu wa ajira na Uzembe kuelekea katika Bidii, Kazi na Utendaji wa uhakika, na kutoka katika kujipenda, uchoyo na Kasumba ya Kijahili, kuelekea katika kuwapendelea wengine na kuleta undugu wa kibinadamu ulio wa kweli, na kuamini uwepo wa wengine, na haki ya kibinadamu ya kujichagulia, na uhuru wa kuabudu, na mahusiano ya ujirani mwema, na kufanya kazi ya ujenzi wa Mwanadamu kiimani, kielimu, kifikra, kimwenendo, kitabia, kiuchumi na kijamii, kwa ujenzi ulio salama na wenye misingi imara, inayoijenga nchi na kutengeneza Staarabu, na inaleta masilahi ya kiutu kwa wote, na kuulinda utukufu wa ubinadamu, kama binadamu.

Hakika Maana sahihi ya Hijrah (Uhamaji) inaelekea kwamba Uhamaji usiomalizika katika zama zote ni mabadiliko ya kutoka katika Ujinga na kuelekea katika Elimu, kutoka katika Upotovu na kuelekea katika Uongofu, na kutoka katika Tabia chafu kuelekea katika Tabia njema, na kutoka katika Ufisadi na kuelekea katika Ubora na Ubora zaidi, kwa namna ambayo inachangia ujenzi wa Ustaarabu na Ulimwengu, kwa kuwa Dini yetu ni Dini ya Ujenzi na Uimarishaji wa Ulimwengu wote. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {هُوَ أَنْشَأَكُمْ مِنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا}

Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo.

Kwa hiyo Umma wetu ni Umma wa kazi na wala sio Umma wa uzembe. Huu ni Umma wa kujenga sio kubomoa au kuharibu. Ni Umma wa Ustaarabu. Na kamwe kuchelewa kimaendeleo hakujawahi kuwa moja ya alama za Umma huu. Kwa hivyo, ni juu ya kila Mwislamu kuipenda Dini yake na kujigamba kwayo, na atende kwa ajili ya kuinyanyua Dni yake, na utukufu wa nchi yake, mbali na kila aina ya ukengeukaji, upotoshaji, na siasa kali, kama vile kuhamia kwenye makundi ya kigaidi kwa fikra potovu ya kupigania jihadi ya wongo,  chini ya bendera za uwongo, au kama vile uhamiaji kinyume cha sheria  ambao hupelekea kuangamia, au kudhalilishwa na kunyanyasika, na ambao humfanya mtu kuwa mkosa kisheria na mwenyekupata madhambi kidini; kwa kuwa heshima ya nchi ni kama vile ilivyo heshima ya nyumba, na kama ambavyo haijuzu kuingia nyumbani kwa mtu isipokuwa kwa idhini yake, vile vile haijuzu kuingia nchi yoyote isipokuwa kwa njia za kisheria zilizokubaliwa na nchi zote, na pia kama ambavyo mtu hapendi mtu kupenya na kuingia katika nchi yake au aingine kinyume na njia za kisheria zinazotambulika, basi na yeye pia analazimika asifanye hivyo kwa nchi nyingine.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

*        *        *

Sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. Na ninashuhudia na kukiri kuwa hakuna mungu mwingine yoyote anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hana mshirika wake, na ninakiri na kushuhudia kuwa Bwana wetu Muhammad na Mtume wetu, ni Mja wake na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu msalie, mrehemu na umbariki yeye, na Jamaa zake, na Maswahaba wake wote, na kila atakayewafuata kwa wema hadi siku ya Malipo.

Ndugu zangu Waislamu.

Hatuachi kukumbuka katika Mnasaba huu mzuri kwamba Mwezi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambao ni mwezi wa Muharram ni mmoja kati ya miezi mitakatifu, na husuniwa kufunga zaidi ndani yake kwa ujumla. Anasema Mtume S.A.W: Swala iliyo bora baada ya Swala za Faradhi ni Swala inayoswaliwa usiku wa manane. Na Swaumu iliyo bora baada ya ile ya mwezi wa Ramadhani ni ile ya Mwezi wa Mwenyezi Mungu wa Muharram, na Siku ya Ashura kwa sifa maalumu; kwa kauli yake Mtume S.A.W: Funga siku ya Ashura huwa ninatarajia kwa Mwenyezi Mungu anisamehe Mwaka wa kabla yake. Mtume S.A.W alipoenda Madina aliwakuta Mayahudi wakiifunga siku ya Ashura na akasema: Ni siku gani hii? Wakasema: Hii ni siku ya nzuri, hii ni siku ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaokoa wana wa Israeli kutokana na adui yao na Musa akaifunga. Mtume akasema: basi mimi nina haki zaidi kwa Musa kuliko nyinyi. Kisha akaifunga na akaamrisha ifungwe. Anasema bin Abas R.A: Mtume S.A.W alipofunga siku ya Ashura na akaamrisha ifungwe, wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mambo yalivyo hii nisiku inayotukuzwa na Mayahudi na Manaswara, akasema S.A.W: Pindi utakapowadia mwaka ujao,  – kwa utashi wake Mwenyezi Mungu – tutaifunga siku ya tisa. Kwa maana ya siku ya tisa nay a kumi. Kwa hivyo basi katika Sunna ni kufunga siku ya kumi ya mwezi wa Muharram, na ukamilifu wake na utimilifu wake ni kufunga tarehe tisa na kumi za mwezi wa Muharam.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atuwafikishe kwa yale ayapendayo na kuyaridhia, na aujaalie Mwaka Mpya wa Hijiriya uwe mwaka wa Kheri na Baraka na nusura na Ushindi kwa nchi yetu na pia kwa nchi zote za Waislamu.