Miongoni mwa Mafunzo yatokanayo na Hijra ya Mtume S.A.W, ni Ujenzi wa Dola

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mola Mlezi wa Viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{ إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ أُولَئِكَ يَرْجُونَ رَحْمَتَ اللَّهِ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ}

Hakika wale walioamini na wale waliohama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, hao ndio wanaotaraji rehema za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye mwenye kusamehe na mwenye kurehemu.

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa hali isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, peke yake asiye na mshirika wake, yeye ndiye, Mfunguzi wa milango ya neema kwa waja wake, na ni Mjuzi, na ninashuhudia ya kuwa Bwana wetu Muhammad, ni mja wake na ni mjumbe wake, mwenye maadili matukufu. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu mswalie na umrehemu na umbariki yeye na jamaa zake na Maswahaba wake, Wenye kung’aa mapaji ya nyuso zao na waliobarikiwa, na kila mwenyekuwafuata mpaka siku ya Malipo.

Na baada ya utangulizi huu,

Hakika Hijra ya Mtume S.A.W, kutoka Makkah na kuelekea Madina ni tukio la kihistoria lililo kubwa na ambalo limeibadilisha historia ya Binadamu, na sisi tuna haja ya kuyapokea kutoka katika Hijra hiyo, kila aina ya maana ambazo zinaweza kuchangia katika makuzi ya Jamii yetu na kujenga Ustaarabu wake. Hijra hii ilikuwa na inaendelea kuwa ni kitenganishaji kikuu cha baina ya Haki na Batili, na mageuzi mazuri kuelekea katika ujenzi wa Nchi ya kiraia kwa misingi imara ya uadilifu, usawa, uhuru wa kuabudu, ulinzi wa Heshima ya binadamu, na kuweka misingi imara ya Fiqhi ya kuishi kwa pamoja na kwa amani, na kuweka msingi wa maisha ya kibinadamu ya kushirikiana na kuwa na mfungamano wa kijamii baina ya wananchi wa nchi moja na kushiriki katika changamfu za kiuchumi kwa sura zake mbali mbali. Na Mtume S.A.W amejenga nchi kwa misingi mingi na nyenzo za aina mbali mbali, na muhimu miongoni mwazo ni: Ujenzi wa Msikiti: Ujenzi wa Msikiti ulikuwa ndio jambo la kwanza alilolifanya Mtume S.A.W baada tu ya kuwasili Madina; kwa kuwa uhusiano wa binadamu na Mola wake Mlezi ndio kinga ya Usalama wa kila kitu. Kuwa na Dini sahihi ni moja katika ya njia muhimu za ujenzi wa Utu uliokamilika na ambao unajenga na wala haubomoi, na unaimarisha na wala hauharibu. Na kwa kiasi cha kukengeuka na Dini sahihi au kiasi cha ufahamu potovu wa Dini, husababisha mianya katika uundaji wa Utu, kama ambavyo Msikiti una risala yake muhimu ya kielimu na kijamii ambayo inayajenga na kuyaimarisha yaliyo thabiti pamoja na Maadili mema katika Jamii, na kuchangia pia katika kuitumikia jamii hiyo.

Jambo lingine ni ujenzi wa Uchumi: Hakika mambo yalivyo, Uchumi wenye nguvu ni katika Nguzo imara zinazoisaidia nchi, na ni katika misingi yake mikuu ambayo nchi kamwe haiwezi kusimama au kujenga isipokuwa kwayo; kwa hivyo uchumi wenye nguvu na utulivu unaiwezesha nchi kutekeleza majukumu yake ipasavyo, yawe majukuu hayo ni ya ndani au ya kimataifa, ukiongezea na kwamba huleta maisha mazuri kwa wananchi wake. Na pale uchumi wan chi unapodhoofika, basi ufukara huenea pamoja na magonjwa, na maisha kukosa utulivu pamoja na kuzuka kwa migogoro isiyokwisha, na kupelekea kuharibia kwa Tabia za watu na kuongezeka kwa uhalifu wa aina mbali mbali. Na hii huwa ni fursa nzuri kwa maadui wanaozinyemelea nchi, ambao lengo lau kubwa ni kuziangusha na kuingiza machafuko yasiyomalizika.

Mtume S.A.W alikuwa na shime ya kuifanya Jamii ya Madina iwe na nguvu za kiuchumi zinazoiwezesha kutelekeza mahitaji ya wananchi wake, na kujilinda na kutuma ujumbe wa amani na usalama kwa wote na kuujenga ulimwengu ulioletewa Dini ya Uislamu iliyo tukufu. Mtume S.A.W alifanya juhudi pevu ya kuunda soko kubwa la Madina ili liwe chanzo kikuu cha uchumi halali na biashara, ma kituo kikuu cha wakuu wa viwanda na kazi mbali mbali za mikono, na soko hili alilolianzisha Mtume S.A.W, linaitwa soko la Manakha. Kutoka kwa Atwaau bin Yasaar amesema: Mtume S.A.W alipotaka kuanzisha soko la Madina alienda katika soko la Banuu Qainukaa, kisha akaja katika soko la Madina na akapiga kwa miguu yake na akasema: hili ni soko lenu hakuna wa kukunyanyaseni. Maswahaba wakubwa walishiriki katika changamfu mbali mbali za biashara, na hawakukubali kuishi kwa kutegemea misaada ya kifedha kutoka kwa ndugu zao wa Madina. Kutoka kwa Abdulrahman bin Aufi R.A, amesema: Walipoenda wao Madina, Mtume S.A.W aliwaunganisha undugu baina ya Abdulrahman bin Aufi na Saad bin Rabiiu, ambapo alimwambia Abdulrahma: Mimi ni Answaar niliye na mali nyingi mno, ninaweza kuigawa mali yangu mara mbili… akasema: Mwenyezi Mungu akubariki katika watu wako na mali yako. Soko lenu liko wapi?

Kwa hiyo, umma wowote usioweza kumiliki chochote wala kuzalisha chakula chake cha kutosha, nguo zake, madawa yake na silaha zake, basi haujiwezi kwa lolote, na hauna amri, utashi, tamko, hadhi na utukufu wake. Wanasema wenye busara: Mtendee wema umtakae, utakuwa kwake bwana kwake, na jitosheleze na uepuke cha mtu yoyote utakuwa kama yeye, na muhitaji umtakae utakuwa mtumwa wake. Na Dini yetu Tukufu imetufundisha ya kuwa; Mkono ulio juu ni bora kulliko mkono ulio chini, ambapo anasema Mtume S.A.W: Mkono ulio juu ni bora kuliko mkono ulio chini. Na anasema Mtume S.A.W: Mkono unaotoa ndio ulio juu, na mkono unaoomba ndio mkono ulio chini. Na hakuna shaka yoyote kwamba kipimo hiki kinatumika pia kwa Umma, Taasisi mbali mbali, Familia na kwa kila mtu. Kwa hiyo hakuna anayeweza kuukana umuhimu wa mali katika kurahisisha maisha kwa ujumla, na kumuinua kila mtu pamoja na umma, ili kuzifikia njia bora za maisha mazuri, na kupanda ngazi mbali mbali za maendeleo.

Anasema Mshairi, Ahmad Shauki:

Kwa elimu na Mali, watu huujenga ufalme wao

                            Haujengwi ufalme kwa ujinga na umasikini.

Mtume S.A.W ameweka masharti yaliyopangika katika Miamala mbali mbali, na akatuasa tuwe na usamehevu na roho safi katika kuuza na kununua, akasema S.A.W: Mwenyezi Mungu anamrehemu mja msamehevu pale anapouza, anaponunua na anapotoa hukumu. Na akatuamrisha Mtume S.A.W, tuwe wakweli na waaminifu, akasema:  Mfanyabiashara Mkweli, Mwanifu, atakuwa pamoja na Manabii na Mashahidi. Na Mtume S.A.W ameuharamisha ulanguzi akasema: Mtu yoyote atakaefanya ulanguzi wa chakula kwa muda wa siku arubaini basi atakuwa amejiepusha na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atakuwa amejiepusha nae. Bali Mtume S.A.W alikuwa yeye mwenyewe akipita pita sokoni na kufuatilia Uuzaji na ununuaji, na alikuwa akiwaelekeza watu kwa yale yanayowanufaisha. Kutoka kwa Abu Huraira R.A, kwamba Mtume S.A.W alipitia katika sehemu ya nafaka iliyowekwa mezani, kisha akaingiza vidole vyake katika nafaka hiyo na kuhisi unyevunyevu akasema S.A.W: Ewe Muuza chakula, hiki ni kitu gani? Akasema: nafaka hii ilinyeeshewa na mvua ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema Mtume S.A.W: kwanini usikiweke juu ili watu waone? Kisha akasema S.A.W: mtu yoyote atakaetudanganya sio mwenzetu.

Mkataba wa Madina: Mtume S.A.W alijenga nchi yenye nguvu baada ya Hijra, na akaweka misingi yake katika Mkaraka wa Madina, na Mtume wetu hakuishia katika kuwaunga undugu watu wa Makkaha na wa Madina (Muhajirina na Answaar) kutokana ni hitilafu walizokuwa nazo, bali alihamia katika maana ya kiutu zaidi kupitia uundaji wake wa Waraka wa Madina na amabao unazingatiwa kuwa ni Waraka Bora mno kuwahi kuundwa na binadamu katika Historia ya yote; ambapo ulizipitisha na kuzikubali haki na majukumu kwa watu wote, na na kuweka misingi ya kuishi pamoja kwa amani baina ya wanachi wote kwa upande mmoja, na kati ya Utu kwa upande mwingine, kwa namna inayoufanya waraka huo uwe bora zaidi kihistoria na wa kipekee katika nyaraka za kibinadamu katika Fiqhi ya kuishi pamoja. Na alama ya hayo: ni Mkataba alioupitisha Mtume S.A.W na Mayahudi wa Madina na wengine wao, ambapo aliwapa mayahudi haki zote  za waislamu katika Usalama na amani, uhuru na ulinzi wa pamoja. Na miongoni mwa vipengele muhimu, ni: Mayahudi watoe pamoja na waislamu kama wataendelea kuwa wanashambuliwa, na kwamba mayahudi wa Banu Aufi ni umma ulio pamoja na Waumini, mayahudi wana Dini yao na Waislamu wana Dini yao, watumwa wao na nafsi zao isipokuwa atakaedhulumu au kufanya madhambi. Na ndani ya Waraka huo, kuna kuhakikishiwa uhuru kamili wa Dini, Usalama, Ulinzi wa pamoja dhidi ya adui yoyote anayeishambulia Madina.

    Na hii inamaanisha kuwa nchi ya kiraia katika Uislamu inatosha kwa wote, waislamu na wasio kuwa waislamu. Wote wana haki na majukumu na kila mmoja wao ana juu ya mwingine wajibu kamili. Kwa sharti la kufuata kikamilifu Masharti ya Kijamii yanayozilinda haki za watu wote na Majukumu yao, na katika yaliyo mbele ni: Amani na kutomshambulia mtu, na kutovunja katiba inayopangilia Uhusiano baina ya watu wote.

Hakika mambo yalivyo, kuishi pamoja na kwa amani baina ya watu wote ni faradhi ya kidni, na jambo muhimu kijamii linaloulazimu uhalisia anaouishi mwanadamu. Na haiwezekani kulifikia lengo hili isipokuwa watu wote watakapohisi kuwa wao ni wananchi wan chi moja pekee, wana haki sawa na majukumu yanayolingana, bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote iwayo, kwa misingi ya kidini au kikabila au vinginevyo. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ قَدْ تَبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ}

Hakuna kulazimisha katika dini kwani uongofu umekwisha pambanuka na upotovu.

Mtume S.A.W na Maswahaba wake waliyatekeleza haya kivitendo na hawakuwahi kumlazimisha mtu yoyote kuingia katika Dini hii ya Mwenyezi Mungu, na hawajawahi kulibomoa kanisa lolote au hekalu au jumba lolote la ibada, bali maeneo yote ya ibada yaliheshimika na kulindwa na waislamu ipasavyo. Ni kwa sababu Uislamu unaulinda Uhuru wa kuabudu wa watu wote, na hakuna yoyote aliye miliki au anaemiliki uwezo wa kubadilisha uaina huu na tofauti hii; kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na utashi wa Mwenyezi Mungu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَآمَنَ مَنْ فِي الْأَرْضِ كُلُّهُمْ جَمِيعًا أَفَأَنْتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّى يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ}

Angelitaka Mola wako Mlezi wangeliamini wote waliopo katika ardhi. Je wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe waumini?

Kwa hiyo, kuheshimu Itikadi, Haki na Wajibu wa kila mtu, ni nguzo kuu ya ujenzi wa Dola, na ina athari yake ya mfungamano wa mahusiano baina ya Mataifa na Jamii. Kwani kila taifa lina Itikadi yake na Misingi yake inayoheshimiwa na kufuatwa, na kuzingatiwa kuwa ni bora kuliko zingine zozote. Na Uislamu umetukataza kuwafanyia watu wa Dini zingine yale yanayowakashifu wao au Dini zao, kwani Dini zote zimekuja kwa ajili ya kumletea furaha mwanadamu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{ وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ فَيَسُبُّوا اللَّهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ كَذَلِكَ زَيَّنَّا لِكُلِّ أُمَّةٍ عَمَلَهُمْ ثُمَّ إِلَى رَبِّهِمْ مَرْجِعُهُمْ فَيُنَبِّئُهُمْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ} .

Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda. Vile vile Uislamu umeweka katika nafsi za wafuasi wake msingi imara wa Wema na Ujirani mwema na wasio kuwa waislamu. Na kuna aya iliyokuja kwa ajili ya kuusisitizia msingi huu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {لَا يَنْهَاكُمُ اللَّهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُمْ مِنْ دِيَارِكُمْ أَنْ تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ} .

Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.

Uislamu umewaamrisha wafuasi wake kulinda mtangamano mwema na wasiokuwa waislamu na kuchunga hisia zao hata katika maongezi na mijadala, pamoja na kuhimiza maongezi yawekwa yale mambo mazuri zaidi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ وَقُولُوا آمَنَّا بِالَّذِي أُنْزِلَ إِلَيْنَا وَأُنْزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَهُنَا وَإِلَهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ}

Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.

Na kwa ajili hii, Mkataba wa Madina ulikuwa mfano wa kuigwa katika kulinda utukufu wa kibinadamu, mkataba ambao unafanya kazi ya kuungana na kuwa bega kwa bega kitaifa kwa ajili ya ujenzi wa Dolan a kujenga Staarabu mbali mbali, na kuyafikia masilahi ya binadamu wote.

Ninayasema haya, na nimamwomba Mwenyezi Mungu anisamehe mimi na nyinyi.

***

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote. Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye pekee asiye na mshirika wake. Na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad S.A.W ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki Mtume wetu S.A.W, yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote, na kila atakaemfuata kwa wema hadi siku ya Mwisho.

Na baada ya utangulizi huu,

Hakika Taifa lina thamani kubwa mno na lina hadhi kubwa sana na nafasi ya juu. Kuipenda nchi na kuwa mzalendo kwa nchi yako pamoja na kuilinda ni jambo la kimaumbile ambalo nafsi ya binadamu iliyosalimika imeumbiwa kwalo, na ni wajibu uliowekwa kimsingi na Dini tukufu ya uislamu, na wajibu huu unawajibishwa na Utaifa na Uzalendo. Na Sheria zote za Mwenyezi Mungu zimeuthibitisha. Na Mtume S.A.W, ametoa mifano mingi mikubwa katika kuipenda nchi na kufungamana nayo pamoja na kuwa na uzalendo nayo, ambapo alisema S.A.W wakati alipokuwa katika Hijra yake ya kuelekea Madina, akiisemesha nchi yake ya kwanza ambayo ni Makkah Tukufu: Uzuri wako ulioje wan chi, na Mapenzi yaliyoje kwangu, kama watu wako wasingenitoa basi nisingetoka. Na Mtume S.A.W alipohamia Madina Munawara na kuishi huko, alimwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amjaalie mapenzi ya kuipenda nchi yake ya pili, na alete Usalama na Amani ndani ya nchi yake hiyo ya pili. Akasema S.A.W: Ewe Mola wetu Mlezi tunakuomba utupe mapenzi ya kuipenda nchi yetu ya pili, ya Madina, kama tunavyoipenda Makkah au zaidi yake.

Hakika uhusiano kati ya Dini na Nchi ni kukamilishana na wala sio wa kukinzana. Na kuzilinda nchi ni moja ya Makusudio Makuu nay a Muhimu ambayo tunapaswa kuyalinda na kuyahifadhi. Na hakuna uchumi tulivu bila ya usalama wa uhakika na endelevu. Na ulinzi wa nchi na kuilinda kwake pamoja na kujitolea, ni kwa ajili ya takwa la kisheria, na ni wajibu wa kitaifa kwa kila anaeishi na kutulizana ndani yak echini ya ardhi ya nchi hiyo na kivuli chake; kwa hivyo kuipenda nchi hakuishii katika hisia na mihemko pekee, bali kunatafirika kivitendo na kwa mwenendo mzuri wenye manufaa kwa kila mtu na kwa Jamii nzima; na kwa ajili hiyo, hapana budi kujitolea kwa ajili ya kuiendeleza nchi huku ikiendelea kuwa na nguvu na yenye kupendwa na wananchi wake.

Hakika uzalendo wa kweli sio tu alama zinazonyanyuliwa juu na watu, au maelezo yanayokaririwa na watu; bali uzalendo wa kweli ni Imani, Mwenendo na kujitolea, uzalendo ni mfumo wa Maisha na hisia zinazotokana na uhai wan chi na changamoto ambazo zinaielekea nchi hiyo, na kuhisi uchungu kwa machungu ya nchi hiyo, na kuwa na furaha kwa kuyafikia matumaini yake na kuwa tayari daima kwa ajili ya kujitolea kwa ajili ya nchi. Kongole kwa wanaume waliokuwa wakweli kwa ahadi walizotoa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kujitolea kwa roho zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa ajili ya kuzinyanyua juu nchi zao.

      Ewe Mola wetu Mlezi tunakuomba uilinde nchi yetu, wananchi wake, majeshi yake ya Ulinzi na Usalama, kutokana na kila ovu, na tunakuomba ujibu vitimbi vya wenyekufanya vitimbi, na chuki za wenye chuki, na Husda ya wenye kuhusudu.