Alama za Kiburi, Kujikweza na Kuizuia Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

     {سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِنْ يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِنْ يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لاَ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلاً وَإِنْ يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلاً ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ}

Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na wameghafilika nazo.

Na ninashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye pekee asiye na mshirika wake, Mwenye Nguvu na Mwenye kutoa Maamuzi, na ninashuhudia kuwa Bwana wetu Muhammad ni Mja na Mtume Wake. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake, na Maswahaba wake wote.

Na baada ya utangulizi huu:

Hakika mambo yalivyo, Mwisho wa wenye Kiburi ni mbaya sana, Duniani na Akhera, awe mtu mmoja mmoja au Mataifa. Kwani kuangamia kwa Mataifa na Vijiji vilivyo kuwa na Kiburi na ukaidi ni tukio la kawaida hapo zamani, kwa viumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wala hutaona mabadiliko yoyote ya kawaida ya Mwenyezi Mungu Mtukufu au mageuzi.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً  أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً  وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ * فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ لِّنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَى وَهُمْ لَا يُنصَرُونَ }

Ama kina A’di walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu! Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ عَتَتْ عَنْ أَمْرِ رَبِّهَا وَرُسُلِهِ فَحَاسَبْنَاهَا حِسَابًا شَدِيدًا وَعَذَّبْنَاهَا عَذَابًا نُّكْرًا* فَذَاقَتْ وَبَالَ أَمْرِهَا وَكَانَ عَاقِبَةُ أَمْرِهَا خُسْرًا}

Na miji mingapi iliyo vunja amri ya Mola wake Mlezi na Mitume wake, basi tuliihisabia hisabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali.Basi ikauonja ubaya wa mambo yake; na mwisho wa mambo yao ilikuwa khasara.

Na kiburi ni dhambi ya Kwanza kabisa kuwahi kutumika katika kumuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu, nayo ni pale Mwenyezi Mungu Mtukufu alipowaamrisha Malaika wamsujudie Adamu wakasujudu isipokuwa Ibilisi; anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلائِكَةِ اسْجُدُوا لآَدَمَ فَسَجَدُوا إِلاَّ إِبْلِيسَ أَبَى وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ}.

Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblisi, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.

Hakika Watu wenye kiburi watajulikana kwa alama zao za kuchukiza siku ya Mwisho kama walivyokuwa wanajulikana kwayo Duniani.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَنَادَى أَصْحَابُ الأَعْرَافِ رِجَالاً يَعْرِفُونَهُم بِسِيمَاهُمْ قَالُوا مَا أَغْنَى عَنكُمْ جَمْعُكُمْ وَمَا كُنتُمْ تَسْتَكْبِرُونَ}،

Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa alama zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho mlicho kuwa mnafanyia kiburi.

Na kwa ajili hiyo, Uislamu umeonya kuhusu mwisho mbaya wa kiburi, na ukakifanya kiburi kuwa ni mmoja wa milango ya kuwa mbali na Rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akawaonya wenye kiburi kuwa wana wao adhabu iumizayo.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا لاَ تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَلاَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ حَتَّى يَلِجَ الْجَمَلُ فِي سَمِّ الْخِيَاطِ وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُجْرِمِينَ}

Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyowalipa wakosefu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ}

Na Siku ya Kiyama utawaona walio msingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanaotakabari?

Anasema Mtume S.A.W: Pepo na Moto vilitoa hoja, Moto ukasema: Ndani yangu kuna Majabari na Wenye Kiburi. Pepo ikasema: ndani yangu kuna wanyonge na masikini wao, na Mwenyezi Mungu akatoa hukumu baina ya Moto na Pepo: Hakika ewe Pepo wewe ni rehma yangu ninamuhurumia kwayo nimtakaye, na hakika wewe Moto ni adhabu yangu ninayomuadhibia nimtakaye. Na kila mmoja kati yenu mimi ndiye mwenye kumjaza.

Na anasema Mtume S.A.W: Je nikupeni habari za watu wa Motoni? Wote ni wenye majivuno na kiburi.

Hapana shaka ya kwamba Kiburi ni tabia inaayokaa ndani ya moyo wenye maradhi. Mtu anaweza kuwa na hali mbaya ya kimaisha, anamiliki vitu vichache, na akawa katika wenye kiburi, na anaweza kuwa mtu tajiri aliyetandikiwa Dunia na Mwenyezi Mungu akawa ni katika wanyenyekevu na wenye heshima. Anasema Mtume S.A.W: Haingii peponi mtu mwenye chembe ya Kiburi katika Moyo wake. Akasema Mtu mmoja: Hakika Mtu anapenda nguo zake ziwe nzuri, na viatu vyake vizuri, akasema Mtume S.A.W: Hakika Mwenyezi Mungu ni Mzuri na anaupenda Uzuri. Kiburi ni adui wa Haki na na huwatenga watu. Na ni katika magonjwa yaliyo hatari mno kwa moyo na kwa jamii, ugonjwa ambao unauvunja moyo na unaivunja jamii, na mwenye kiburi ni mwenye kudanganyika moyoni mwake kwa kujikweza kwa wengine kwa kiburi chake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنْ فِي صُدُورِهِمْ إِلاَّ كِبْرٌ مَا هُمْ بِبَالِغِيهِ}.

Hakika ndani ya vifua vyao hakuna isipokuwa kiburi na wala hicho hawakifikii.

Ingawa kiburi hutulizana na kuuishi moyoni, kuna alama zake zinazojitokeza katika Mwenendo na Mtangamano wa mtu na watu wengine: miongoni mwazo ni: Kupandwa na mori wa Madhambi, na kutoinyenyekea haki. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{…. وَإِذَا قِيلَ لَهُ اتَّقِ اللَّهَ أَخَذَتْهُ الْعِزَّةُ بِالْإِثْمِ}

Na anapoambiwa; mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi…

Kwa hivyo mtu mwenye kiburi na majivuno huvutiwa na majivuno mabaya na kujikweza kwake kuovu kwa kuikana haki, na waka kumlingania katika haki hakumzidishii yeye isipokuwa majivuno na kujikweza, na akaitumbukiza nafsi yake katika maangamizi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {فَحَسْبُهُ جَهَنَّمُ وَلَبِئْسَ الْمِهَادُ}

Basi huyo inamtosha Jahannamu. Paovu mno hapo kwa mapumziko.

Na kuna anaetakabari dhidi ya amri ya Mtume S.A.W, na kisha akakutana na malipo ya kiburi na ukaidi wake.

Kutoka kwa Iyasu bin Salamah bin Ak-wau R.A, kwamba baba yake alimsimulia ya kwamba mtu mmoja alikuwa mbele ya Mtume S.A.W, upande wa kushotoni kwake, akasema S.A.W: Kula kwa mkono wako wa kulia, akasema: Siwezi, akasema S.A.W: Unaweza. Hakikumzuia isipokuwa kiburi chake. Akasema: Hakuunyanyua mkono wake na kuupeleka mdomoni. Na miongoni mwa alama hizo ni: kuwabeuwa watu kwa kiburi wakati wa kuangalia.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukataza kupitia kauli ya Lukmani alipomwambia mwanae:

 {وَلا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلا تَمْشِ فِي الأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتالٍ فَخُورٍ}. وَمِنْهَا: الاِخْتِيَالُ فِي الْمَشْيِ: وَيَعْنِي: التَّبَخْتُرَ وَالتَّعَالِيَ فِي الْمِشْيَةِ ، قال تَعَالَى:

wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anyejivuna na kujifaharisha.

Na miongoni mwa alama za kiburi ni kutembea kwa maringo: ina maana ya kujivuna na kujikweza wakati unatembea.  Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلاَ تَمْشِ فِي الأَْرْضِ مَرَحًا إِنَّكَ لَنْ تَخْرِقَ الأَْرْضَ وَلَنْ تَبْلُغَ الْجِبَال طُولاً كُل ذَلِكَ كَانَ سَيِّئُهُ عِنْدَ رَبِّكَ مَكْرُوهًا}.

Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima. Haya yote ubaya wake ni wenyekuchukiza kwa Mola wako Mlezi.

Na katika alama za kiburi ni kuringia mali na neema mbali mbali za Mwenyezi Mungu. Anasema Mtume S.A.W:

Kuna mtu mmoja katika waliokuwa kabla yenu, alitoka akiwa amevaa vazi lake anajigamba kwalo. Mwenyezi Mungu akaiamrisha ardhi ikammeza, nae anajitingisha tingisha ndani ya ardhi mpaka siku ya Kiama. Kwa kuwa kiburi huwa kinakuwa kwa mtu kuringia nguo zake, huwa pia kwa kuringia mashuka na matandiko ya nyumba, kwa kupanda magari, kwa kumiliki majumba ya kifahari kwa njia ya kujigamba nakujionesha kwa watu. Na vile vile kwa mengine mengi katika mali za duniani.

Na miongoni mwa alama za Kiburi ni kujiepusha na kukaa na Mafukara na Wanyonge kwa kuwadharau, kama vile washirikina wanavyojiepusha kukaa na Maswahaba Mafakiri, akina Salman, Suhaibu, na Bilali na wengine wengi R.A, mpaka baadh yao wakasema wakimwambia Mtume S.A.W: Wafukuze hawa watu wanajikweza Mbele yetu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha Wahyi akamwambia Mtume S.A.W:

{وَلاَ تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ}

Wala usiwafukuze wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake.

Na miongoni mwa sura za kujiepusha na watu vile vile: ni Ulinganiaji kuwa kwenye mialiko ya Chakula tu inayoitishwa na Matajiri na kuwaacha mafukara kwa ajili ya kuwadogesha. Anasema Abu Huraira R,A: Chakula kibaya kabisa kuliko vyote ni chakula cha mwaliko, huitwa matajiri na kuachwa masikini. Vile vile katika alama za Kiburi: kujiepusha na utoaji wa salamu au kupeana mikono na walio chini yake mtu kwa cheo au hadhi kama ni njia ya kuwadharau na kuwanyanyasa. Na Mtume S.A.W, alikuwa akianza yeye kutoa salamu kwa mkubwa na mdogo.  Na katika Hadithi ya Mtume S.A.W, Kwamba Mtume S.A.W, alipita kwa wavulana na akawasalimia.

Na miongoni mwa alama za Kiburi pia ni: Kupindukia katika Ugomvi na kuwa mwovu ndani yake, na hakuna hitilafu kwamba ni haramu kwa mwislamu kumuhama nduguye zaidi ya siku tatu; kwa kuwa katika ugomvi kuna kuukata undugu na kuna kuudhi na kuharibu, na kuna kuthibiti onyo la adhabu kali kwa nweye sifa hizi siku ya Mwisho. Anasema Mtume S.A.W:  Mtu yoyote atakaemuhama ndugu yake kwa zaidi ya siku tatu basi ataingia Motoni isipokuwa kwa utukufu wake Mwenyezi Mungu akimuwahi.

Anasema Mtume S.A.W: Haiwi halali kwa Mwislamu kumuhama ndugu yake zaidi ya siku tatu, wanakutana na huyu anamkwepa huyu na huyu namkwepa huyu, na mbora wao ni yule anaeanza kutoa Salamu.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Mambo manne mtu akiwa nayo basi anakuwa mnafiki wa kweli, na mtu atakaekuwa na moja kati ya mambo hayo atakuwa na sehemu ya unafiki mpaka ayaache: Anapoaminiwa hufanya hiyana, na anapozungumza husema uongo, na anapoahidi huvunja ahadi, na anapogombana na mtu huwa mwovu zaidi.

    Kiburi na Kujikweza vilikuwa sababu ya kujizuia kwa wengi miongoni mwa Washirikina katika kuingia Uislamu. Na kuhusu Kauli ya Mwenyezi Mungu, Hakuna mungu yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu; anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّهُمْ كانُوا إِذا قِيلَ لَهُمْ لا إِلهَ إِلاَّ اللَّهُ يَسْتَكْبِرُونَ}

Wao walipokuwa wakiambiwa; Hapana mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu tu, walikuwa wanajivuna.

Wakawa wanakana kuifuata Dini yoyote isipokuwa ya Baba na Mababu zao. Na kwa sababu ya Kiburi,, Mayahudi waliacha kumfuata Mtume Muhammad S.A.W, ingawa walikuwa na yakini juu ya Ukweli wake kuhusu Utume aliokuja nao.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ وَإِنَّ فَرِيقًا مِنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ}

Wale tuliowapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyowajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali ya kuwa wanaijua.

Nae vile vile ndiye aliyewabebesha jukulu wana wa Israili kwa kuwakadhibisha Manabii na kuwaua baadhi yao.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{أَفَكُلَّمَا جَاءَكُمْ رَسُولٌ بِمَا لاَ تَهْوَى أَنفُسُكُمُ اسْتَكْبَرْتُمْ فَفَرِيقاً كَذَّبْتُمْ وَفَرِيقاً تَقْتُلُونَ}.

Basi kila walipokufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha na wengine mkawaua.

Hakika Kiburi ni sababu inayopelekea kukufuru na kukukadhibisha kwa wenye kukadhibisha katika Mataifa yaliyopita. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِنِّي كُلَّما دَعَوْتُهُمْ لِتَغْفِرَ لَهُمْ جَعَلُوا أَصابِعَهُمْ فِي آذانِهِمْ وَاسْتَغْشَوْا ثِيابَهُمْ وَأَصَرُّوا وَاسْتَكْبَرُوا اسْتِكْباراً}

Na mimi kila ninapowalingania ili upate kuwasamehe walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno!

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu watu wa Mtume Hud A.S:

{فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً}

Ama kina Adi walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliyekuwa na nguvu kushinda didi?

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu watu wa Mtume Swaaleh A.S:

{قَالَ الْمَلأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُواْ مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُواْ لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ قَالُواْ إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ * قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُواْ إِنَّا بِالَّذِيَ آمَنتُمْ بِهِ كَافِرُونَ}

Waheshimiwa wa kaumu yake wanaojivuna waliwaambia wanaoonewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa.Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo yaamini.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Watu wa Shuaibu:

(قَالَ الْمَلأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُواْ مِن قَوْمِهِ لَنُخْرِجَنَّكَ يَا شُعَيْبُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَكَ مِن قَرْيَتِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا)

Waheshimiwa waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shua’ib! Tutakutoa wewe pamoja na wale walio kuamini katika mji wetu, au mrejee katika mila yetu.

Hakika mwisho wa kila Uma wenye Kiburi katika Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Maangamizi na Hasara kubwa. Ni ubaya ulioje wa Mwisho kama huo na ubaya ulioje wa Mwelekeo.

Hakika tiba bora kwa Mtu mwenye mtihani huu wa Kiburi ni kuutibu Moyo wake, kwa kujijua moyoni mwake akaangalia asili ya kuwepo kwake baada ya kutokuwepo kutokana na udongo, kisha tone la maji, kisha pande la Damu linaloning’inia, kisha pande la nyama, kisha akawa kitu kinachotajwa baada ya kutokuwepo kabisa. Na Mja mwenye kiburi anatakiwa ajue kwamba ataadhibiwa siku ya Malipo kinyume na kusudio lake. Na mtu yoyote atakayekusudia kujikweza na kujigamba dhidi ya wengine, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamfufua siku ya Kiama akiwa ndiye Dhalili na Mpungufu kuliko wote. Anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, S.A.W: Watu wenye kiburi watafufuliwa siku ya Mwisho mfano wa kitu kisicho na thamani, huku wakiwa na sura za Watu (wanaume), wamegubikwa na udhalili kila sehemu…

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

  {تِلْكَ الدَّارُ الْآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لَا يُرِيدُونَ عُلُوًّا فِي الْأَرْضِ وَلَا فَسَادًا وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ}.

Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasio taka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu.

Na ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

***

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye peke yake, na kwamba Bwana wetu Mtume Muhammad S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na MAswahaba wake wote.

Ndugu zangu Waislamu. Hakika miongoni mwa alama za kuizuia Njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kukinzana kwa kauli na vitendo, na kudai kuwa na ukamilifu na kusalimika na kasoro kwa wale wanaozingatia zaidi Umbile na Mwonekano, na wanaupa mwonekano wa Umbile Kipaumbile kisicho na mipaka, hata kama kufanya hivyo ni dhidi ya Uhalisia. Hata kama mwenye Mwonekano huo ni mtu duni kiutu na kimaadili yanayoweza kumfanya awe mfano wa kuigwa ulio na sifa; hivyo ni kwa kuwa mtu mwenye mwonekano wa juu juu mabaye mwenendo wake hauwi ni wenye kuendana na mafundisho ya Uislamu anazingatiwa ni moja ya njia kuu za kubomoa, kuwachukiza watu na kuwazuia na njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mfano wa watu hawa ni wale ambao wanathibitishwa na kauli ya Mtume S.A.W aliposema: Hakika miongoni mwenu kuna wanaowakimbiza watu katika Njia ya Mwenyezi Mungu.

Ikiwa Mwonekano ni wa wafuasi wa Dini pamoja na kufatiwa na mtangamano mbaya na watu, au uongo, au kuvunja ahadi, au hiyana, au kula mali za watu kwa njia ya haramu, basi kilichopo hapa ni hatari mno. Bali mwenye tabia hizi anafuata njia ya wanafiki, kama ilivyo hali ya Makundi yaliyotoka katika Misingi ya Dini yakiitumia Dini ya Mwenyezi Mungu kwa masilahi yao, ingawa yenyewe ndiyo yanayoufuga Ugaidi na ndiyo yanayouunga mkono, yakiwa na pupa ya kuziangusha nchi na kuzizorotesha kwa namna ambayo inwarahisishia wao – kwa mujibu wa madai yao – kufika madarakani katika nchi hizo, wanatumia kila aina ya njia huku wakizihalalisha njia zote. Na vile vile mtu yoyote anayeweka mipaka ya kufuata Dini katika mlango wa Ibada na Jitihada ndani ya ibada, pamoja na uelewa potofu wa Dini, na kupindukia katika kukufurisha watu na kubeba silaha pamoja na kutoka kwa ajili ya kupambana na watu, kama ilivyotokea kwa Makhawaarij ambao walikuwa watu wenyekusali sana, kufunga sana kuswali swala za usiku kwa wingi, isipokuwa wao hawakujifunza elimu za Sheria kwa kiwango cha kutosha ambacho kingewazuia kumwaga damu, wakatoka kwa ajili ya kupambana na watu kwa panga zao, na kama wangeliitafuta elimu na wakaipata basi ingewazuia kufanya hivyo

Uislamu ni Dini ya huruma kwa maana zake zote, na kila kinachokuweka mbali na huruma basi kinakuweka mbali na Uislamu. Na zingatio liko katika Mwenendo wa mtu ulionyooka sio kauli tu.

Wanasema wenye busara: hali ya Mtu katika maneno elfu moja ni bora kuliko Maneno elfu moja kwa mtu mmoja.

حَالُ رَجُلٍ فِي أَلْفٍ خَيْرٌ مِنْ كَلامِ أَلْفٍ لِرَجُلٍ .

Ewe Mola wetu Mlezi tunakuomba utuoneshe Haki kama ilivyo na utujaalie tuwe ni wenye kuifuata, na utuoneshe batili kama ilivyo na utujaalie tuwe ni wenye kuepukana nayo.