Kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu na Athari yake katika Kuinyoosha Nafsi ya Mwanadamu

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu

{الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّهِ أَلَا بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ}

Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu Mlezi tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki Mtume wetu na Jamaa zake na Maswahaba wake na kila atakayewafuata hadi siku ya Malipo.

Na baada ya Utangulizi huu:

Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamrisha waja Wake wamtaje kwa wingi na akawaahidi Malipo Makubwa kwa kumtaja yeye.

Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّهَ ذِكْرًا كَثِيرًا * وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا}

Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru… Na mtakaseni asubuhi na jioni.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَالذَّاكِرِينَ اللَّهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّهُ لَهُمْ مَغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا}

…na wanao mtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ *الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ *أُولَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَهُمْ دَرَجَاتٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ}

Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidishia Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale tunayo waruzuku. Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira, na riziki bora, kwa Mola wao Mlezi.

Mtume S.A.W, amesisitiza Uma uzidishe kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuuasa kwa jambo hili. Anasema Mtume S.A.W: Je niwaelezeni habari za matendo yenu? Na yaliyo bora zaidi kwa Mola wenu? Na yaliyo na daraja la juu kwenu, na bora zaidi kwenu kuliko kutoa Dhahabu na Fedha na ni bora zaidi kwenu kuliko kukutana na adui zenu na mkazipiga shingo zao na wao wakazipiga shingo zenu? Wakasema: ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akasema S.A.W: Ni kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na alipokuja mtu kwa Mtume S.A.W, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakika Sheria za Kiislamu zimekuwa nyingi mno kwangu mimi, basi niambie katika hizo jambo ambalo nitalishikilia zaidi, akasema S.A.W: Ulimi wako uendelee kuwa mbichi kwa kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hakika kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ibada yenye daraja kubwa, nyepesi kuifanya, fadhila zake ni nyingi na hazihesabiki, kwa yale yaliyopokelewa katika kubainisha fadhila zake, na utukufu wa daraja lake, nia yale yaliyokuja kutoka kwa Abu Saidil Khudriy R.A, amesema: Muawiya alikiendea kikao cha mduara msikitini akasema: ni kipi kilichokukalisheni hapa? Wakasema: tumeketi ili tumtaje Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hakuna kilichokukalisheni hapa isipokuwa Mwenyezi Mungu? Wakasema: Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu hakijatukalisha isipokuwa hicho hicho. Akasema Muawiya R.A: hakika mimi sikuapisheni kwa kuwatuhumu, na hakuwa yoyote mwenye nafasi kama yangu kuliko Mtume S.A.W, mwenye maneno machache kutoka kwake kuliko mimi, na kwamba Mtume S.A.W, alikiendela kikao cha maswahaba wake akawauliza: Ni kipi kilichowakalisheni hapa? Wakasema: tumekaa kwa ajili ya kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu na tunamuhimidi kwa kutuongoza katika Uislamu, na akatujaalia neema yake. Akasema Mtume S.A.W: Hakuna kilichokukalisheni hapa isipokuwa Mwenyezi Mungu? Wakasema: Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu hakuna kilichotukalisha hapa isipokuwa hicho hicho tu. Akasema Mtume S.A.W: hakika mimi sikukuapisheni kwa kukutuhumuni, lakini mambo yalivyo, amenijia Jiburilu na akaniambia mimi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anajigamba kwa Malaika kwa kuwa na nyinyi.

Na kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ni uhai wa Moyo, na ni maneno yampendezayo mno Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kutoka kwa Abu Musa R.A, amesema kwamba Mtume S.A.W: anasema: Mfano wa yule anayemtaja Mola wake Mlezi na yule asiyemtaja Mola wake Mlezi ni mfano wa aliye Hai na Maiti. Na katika tamko jingine la Muslim kwamba Mtume S.A.W, anasema: Mfano wa nyumba ambayo ndani yake anatajwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na nyumba ambayo hatajwi Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni mfano wa aliye Hai na Maiti.

Na kutoka kwa Abu Dhari R.A, kwamba Mtume S.A.W, alimtembelea siku moja, na akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, unaona ni maneno gani yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu? Akasema S.A.W: aliyowachagulia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Malaika wake:

(سُبْحَانَ رَبِّي وَبِحَمْدِهِ، سُبْحَانَ رَبِّي وَبِحَمْدِهِ)

Ametakasika Mola wangu Mlezi na kuhimidiwa ni kwake, Ametakasika Mola wangu Mlezi na kuhimidiwa ni kwake.

Na kutoka kwa Samuratu bin Jundabi, amesema: Amesema Mtume S.A.W: Maneno yapendwayo mno na Mwenyezi Mungu ni manne:

(سُبْحَانَ اللهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، وَاللهُ أَكْبَرُ، لَا يَضُرُّكَ بِأَيِّهِنَّ بَدَأْتَ).

Ametakasika Mwenyezi Mungu, na Sifa zote njema za Mwenyezi Mungu, na hakuna mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.

Na hakuna ubaya kwa kuanza na uradi wowote kati ya hizo nne.

Anasema Mtume wetu S.A.W: …wametangulia Mufariduuna. Maswahaba wakamuuliza: ni akina nani hao Mufariduuna ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Ni wale wamtajao Mwenyezi Mungu kwa wingi, wanawake na wanaume.

Na kwa ajili hiyo, kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu kulikuwa wasia wa Mtume S.A.W, kwa Bwana wetu Muadh R.A, ambapo Mtume S.A.W, alimwambia siku moja: Ewe Muadh hakika mimi ninaapa kwa Mwenyezi Mungu ninakupenda. Akasema Muadh kwa baba yangu na mama yangu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na mimi ninakupenda. Akasema: Ninakuusia ewe Muadh, kamwe usiache kusema kila baada ya Sala: Ewe Mola wangu nisaidie mimi niweke kukutaja wewe na kukushukuru wewe na uzuri wa kukuabudu wewe.

Hakika kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ibada inayoamlazimu Mja katika hali zake zote. Na Mwislamu anaamrishwa kuitekeleza ibada hii kila wakati na katika hali yoyote awayo.

Na ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ* الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَى جُنُوبِهِمْ}،

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili, Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala…

Maisha yote ya Mwislamu ni kumtaja Mwenyezi Mungu katika Ibada zake na katika matendo yake. Sala yote kwa ujumla ni utajo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي}

…na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi…

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَأَقِمِ الصَّلَاةَ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَى عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنْكَرِ وَلَذِكْرُ اللَّهِ أَكْبَرُ}

…na ushike Sala. Hakika Sala inayazuia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa…

Kwa maana: Hakika Sala ndani yake kuna makusudio mawili matukufu; La kwanza: Ni kwamba Sala humzuia mtu kufanya mambo machafu na maovu, na Lengo la pili: Ni Utajo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na la pili: ambalo ni Kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ni jambo kubwa na tukufu mno.

Na Mtume S.A.W, alituwekea nyiradi nyingi ambazo Mwislamu anapaswa kuzipupia. Kutoka kwa Abu Huraira R.A, amesema: Mtume S.A.W, alikuwa pindi anapoamka husema:

(اللَّهُمَّ بِكَ أَصْبَحْنَا ، وَبِكَ أَمْسَيْنَا ، وَبِكَ نَحْيَا ، وَبِكَ نَمُوتُ ، وَإِلَيْكَ النُّشُورُ)

Ewe Mola wetu kwa ajili yako wewe tumepambazzukiwa, na kwa ajili yako pamekuchwa, na kwa ajili yako tunaishi, na kwa ajili yako tutakufa na kwako tunafufuliwa na kukusanywa. 

Na panapokuchwa alikuwa anasema:

(اللَّهُمَّ بِكَ أَمْسَيْنَا ، وَبِكَ أَصْبَحْنَا ، وَبِكَ نَحْيَا ، وَبِكَ نموت ، وإليك المصير)

Ewe Mola wangu kwa ajili yako pamekuchwa, na kwa ajili yako pametupambazukia, na kwa ajili yako tunaishi, na kwa ajili yako tunakufa, na kwako tutarejea. 

Na Mtume S.A.W, amesema: Mtu yoyote atakaesema:

(اللَّهُمَّ مَا أَصْبَحَ بِي مِنْ نِعْمَةٍ أَوْ بِأَحَدٍ مِنْ خَلْقِكَ فَمِنْكَ وَحْدَكَ لَا شَرِيكَ لَكَ ، لَكَ الْحَمْدُ وَلَكَ الشُّكْرُ)

Ewe Mola wangu sikupambaukiwa mimi nikawa na neema yoyote au kwa yoyote katika viumbe vyako isipokuwa ni kutoka kwako wewe peke yako usiye na Mshirika wako, wewe ndiwe wa kuhimidiwa na wewe ndiwe wa kushukuriwa. 

Atakuwa ametekeleza shukurani zake za siku hiyo kwa Mola wale Mlezi. Na atakefanya mfano wa hivyo panapokuchwa basi atakuwa ametekeleza shukurani za usiku huo kwa Mola wake Mlezi. Na uzuri ulioje wa mtu anayeianza siku yake kwa kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akaimaliza siku yake pia kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, naye baina ya nyiradi hizo akawa anadumu katika kumtaja Mola wake Mlezi.

Vile vile kuna nyiradi zisemwazo wakati wa kutoka nyumbani na wakati wa kuingia nyumbani ambapo Mtume S.A.W, anasema: Mtu yoyote atakaesema urasi huu wakati anatoka nyumbani kwake:

(بِسْم اللَّهِ توكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ ، وَلا حوْلَ وَلا قُوةَ إلاَّ بِاللَّهِ)

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu mimi ninamtegemea Mwenyezi Mungu, hakuna hila wauwezo isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 

Basi ataambiwa na Malaika: Umeongoka, na uzuiliwa na shari, na umekingwa na mabaya, na pia Shetani atajiepusha nae. Na kutoka kwa Umu Salama R.A, amesema: Mtume S.A.W, hajawahi kutoka nyumbani kwangu kamwe isipokuwa aliinyanyua mikono yake mbinguni na kisha akasema:

(اللَّهُم اني أعوذُ بِكَ أن أَضِلَّ أو أُضَلَّ، أو أَزلَّ أو أُزَلَّ، أو أَظْلِمَ أو أُظلَمَ، أو أجهَل أو يُجْهَل عَلىَّ).

Ewe Mola wangu hakika mimi ninajikinga kwako na kumpoteza mtu au kupotezwa, kuingia katika dhambi au kumwingiza mtu, kudhulumu au kumdhulumiwa, kutenda vitendo viovu au kumtendea mtu vitendo kiovu.  

Na katika Uradi wa kuingia nyumbani, anasema Mtume S.A.W: Mtu anapoingia nyumbani kwake basin a aseme:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ خَيْرَ الْمَوْلَجِ ، وَخَيْرَ الْمَخْرَجِ ، بِسْمِ اللَّهِ وَلَجْنَا ، وَبِسْمِ اللَّهِ خَرَجْنَا ، وَعَلَى اللَّهِ رَبِّنَا تَوَكَّلْنَا

Ewe Mola wangu ninakuomba kheri za kuingia nyumbani kwangu na kheri za kutoka nyumbani kwangu, kwa jina la Mwenyezi Mungu tumeingia na kwa jina la Mwenyezi Mungu tumetoka, na kwa Mwenyezi Mungu Mola wetu Mlezi tunamtegemea. 

Kisha awasalimie watu wake.

Na anasema Mtume S.A.W: Hivi miongoni mwenu mtu anashindwaje kujichumia kila siku mema elfu moja? Muulizaji akamuuliza katika walioketi nae: Vipi mmoja wetu anaweza kujichumia mema elfu moja? Akasema S.A.W: Amsabihi Mwenyezi Mungu mara mia moja, ataandikiwa mema elfu moja, au atafutiwa madhambi elfu moja.

Pia kuna nyiradi zitumiwazo wakati wa kula na kunywa kama vile kusema Bismi lllaahi unapoanza kula, na kusema Alhamdulillahi unapomaliza kula.

Kutoka kwa Omar bin Abii Salamah R.A, amesema: Nilikuwa kijana katika malezi ya Mtume S.A.W, na mkono wangu ulikuwa unakosea kosea katika sahani ya chakula, Mtume S.A.W, akasema: Ewe mvulana, Mtaje Mwenyezi Mungu, na ule kwa mkono wako wa kulia, na ule upande wako. Na Mtume S.A.W, alikuwa anapomaliza kula chakula husema:

(الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَطْعَمَنَا ، وَسَقَانَا ، وَجَعَلَنَا مُسْلِمِينَ).

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametulish, na akatunywesha na akatujaalia sisi tukawa ni miongoni mwa Waislamu.

Mtume S.A.W, ametuwekea utaratibu wa kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu wakati tunapoingia Sokoni na akatuwekea wazi ukubwa wa malipo ya kufanya hivyo, akasema S.A.W: Mtu yoyote atakaesema wakati anaingia Sokoni:

(لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ ، يُحْيِي وَيُمِيتُ ، وَهُوَ حَيٌّ لَا يَمُوتُ ، بِيَدِهِ الْخَيْرُ كُلُّهُ ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ).

Hapana mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika wake, Ufalme wote ni wake na yeye ndiye wa kuhimidiwa, anahuisha na anafisha, naye Ndiye aliye Hai na asiyekufa, Mikononi mwake kuna kheri zote, naye juu ya kila kitu ni Mweza.

Basi Mwenyezi Mungu atamwandikia mema  milioni moja, na atamfutia makosa milioni moja, na atamjengea nyumba milioni moja Peponi. 

Mwislamu vile vile anapaswa kumtaja Mwenyezi Mungu anapokiona kitu kinachomfurahisha, na aseme:

Maa Shaa Allah! Hakuna nguvu zozote isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{ولولا إذ دخلت جنتك قلت ما شاء الله لا قوة إلا بالله}

Na lau kuwa ulipoingia kitaluni kwako ungelisema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.

Ma vile vile wakati anapowaona watu wenye mitihani, Mwislamu anatakiwa kumhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu kimoyo moyo. Anasema Mtume Wetu S.A.W: Mtu yoyote atakaemwona mtu aliyepewa mtihani na akasema:

الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي عَافَانِي مِمَّا ابْتَلَاكَ بِهِ ، وَفَضَّلَنِي عَلَى كَثِيرٍ مِمَّنْ خَلَقَ تَفْضِيلًا)

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye amenipa afya njema na amekutahini kwayo ewe Mja wake, na akanipendelea mimi juu ya vingi miongoni mwa viumbe vyake kwa kunipendelea.

Basi ataepushwa na balaa hilo mtu yoyote awae.

Pia Muumini huwa anarejea kwa Mola wake Mlezi kwa kumtaja kwa wingi anapofikwa na balaa lolote. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَى فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ * فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ وَكَذَلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ}

Na Dhun-Nun alipoondoka akiwa ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhaanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa Waumini.

Na Mtume S.A.W anatuambia tunapofikwa na mitihani na balaa tuseme:

 (لاَ إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ العَظِيمُ الحَلِيمُ ، لاَ إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ رَبُّ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ ، وَرَبُّ العَرْشِ العَظِيمِ) .

Hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mpole. Hakuna mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa Mbingu na Ardhi, na Mola Mlezi wa Arshi Tukufu.

Hizi ni jumla ya njia za kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu zlizowekwa na Mtume S.A.W, na yoyote atakaejizoesha na akaendelea nazo, zitakuwa kwake ni mwongozo na zitamwokoa na  hali ya kughafilika, na zitamuepushia na kumkinga na Shetani. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{اللَّهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُتَشَابِهًا مَثَانِيَ تَقْشَعِرُّ مِنْهُ جُلُودُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ ثُمَّ تَلِينُ جُلُودُهُمْ وَقُلُوبُهُمْ إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ ذَلِكَ هُدَى اللَّهِ يَهْدِي بِهِ مَنْ يَشَاءُ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ}

Mwenyezi Mungu ameteremsha Hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَاذْكُرْ رَبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُنْ مِنَ الْغَافِلِينَ}

Na mkumbuke Mola wako Mlezi katika nafsi yako kwa unyenyekevu na khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni. Wala usiwe miongoni wwa walio ghafilika.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَمَنْ يَعْشُ عَنْ ذِكْرِ الرَّحْمَنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ}.

Anaye yafanyia upofu maneno ya Mwingi wa Rehma, tunamwekea Shet’ani kuwa ndiye rafiki yake.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

*        *        *

Sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na ninashuhudia kwamba hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia kuwa Bwana wetu Muhammad na Mtume wetu, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mwenyezi Mungu mswalie, mrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote, na kila atakaewafuata wao mpaka siku ya Malipo.

Ndugu zangu Waislamu:

Hakika kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Maswahaba kulikuwa ni mfumo wa Maisha yao waliotekeleza kivitendo, jamii yao ikawa imejengeka kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujiepusha na kuchupa mipaka yake, na kutokana na hali hiyo, ndivyo ilivyo jitokeza wakati wa Bwana wetu Abu Bakar R.A, alipompa Ukadhi Bwana wetu Omar bin Khatwaab R.A, na Bwana wetu Omar akakaa Mwaka mzima hakuna mtu yoyote anaemfuata kwa lolote, na hapo ndipo alipomtaka Bwana wetu Abu Bakar R.A, amwachishe kazi hiyo ya Ukadhi. Abu Bakar R.A, akasema: Ewe Omar unataka kuacha kazi kutokana na Uzito unaoupata? Omar R.A, akasema: Hapana ewe Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu; Milionini hakuna haja ya kuwapo kwangu kama Kadhi kwa Waumini, kila mmoja miongoni mwao anazijua haki zake, na wala hahitaji zaidi ya hivyo, na kila mmoja anaujua wajibu wake na hapuuzi katika kuutekeleza kwake, kila mmoja wao anampendelea ndugu yake kile anachokipenda yeye mwenyewe, na mmoja wao anapotoweka wao humtafuta, na anapoumwa wao humtembelea, na anapofilisika wao humuinua, na anapohitaji wao humsaidia, na anapofikwa na msiba wao humhani na kuomboleza nae na humliwaza, Dini yao ni Kunasihiana, na Tabia zao ni Kuamrishana Mema na Kukatazana Mabaya. Wagombanie nini? Wagombanie nini?

Hakika Mja Mwislamu anapozoea kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu moyoni mwake na ulimi wake uyakariri kisha viungo vyake vikayatekeleza, basi nafsi yake itakuwa na msimamo wa kuendelea Kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu na atazipata radhi zake na atambariki katika riziki yake na atamkunjuli huzuni zake na  nafsi yake itajawa na Utulivu na Upole.

Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, tunakuomba utujaalie tuwe ni wenye kukutaja kwa wingi, kukushukuru, na kukuabudu wewe uzuri wa kuabudu, na tunakuomba uzilinde Nchi zetu na uzijaalie ziwe na Usalama, Amani na Maisha bora.