Haki za Wazazi Wawili na Ndugu

.

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa Viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا * وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا}

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.

Na ninashuhudia kuwa hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye pekee asiye na mshirika wake. Na ninashuhudia kuwa Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu mjaalie rehma na amani na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Na baada ya Utangulizi huu:

Uilsamu umekuja kwa risala ya usamehevu, inayowalingania watu tabia njema, na kuwawekea misingi mizuri na kuwaongoza katika kila mwenendo ulionyooka, na kuyafanya maadili na ruwaza za hali ya juu kuwa ndio mfumo wa maisha, unaodhibiti kipimo cha kuishi pamoja baina ya watu wote, kwa uadilifu, huruma, upendo na utu, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {إِنَّ اللَّهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَى وَيَنْهَى عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ}

Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.

Na miongoni mwa alama za Utukufu wa Uislamu ni kwamba wenyewe umeweka misingi na masharti na haki za kuwatendea wazazi wawili na ndugu; kwani wazazi wawili wana haki zaidi ya kuheshimiwa katika watu, na kuwajali na kuwatunza. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamrisha katika Kitabu chake Kitukufu kuwatendea wema wazazi wawili, na kuwa mwema kwao, na Mwenyezi Mungu Mtukufu, akakusanya baina ya hili na amri ya kumwabudu yeye na kutomshirikisha na kitu chochote, ambapo anasema:

 {وَاعْبُدُوا اللَّهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا  وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا}

Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili.

Kama ambavyo ameamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kumshukuru yeye kwa neema zake, na akaambatanisha kuwashukuru wazazi wawili na kumshukuru yeye, kutokana na fadhila zao na nafasi ya juu waliyonayo wazazi wawili, na kiwango cha juu cha uzito wao. Anasema Bwana wetu Abdullahi bin Abas R.A: Aya tatu zimeteremka zikiambatana na mambo matatu, hakuna chochote kinachokubaliwa bila ya kinachoambatana nacho, na miongoni mwa aya hizo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{أَنْ اُشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ}

(Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.

Na yoyote atakayemshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akawa hajawashukuru wazazi wake, basi hatakubaliwa.uislamu umenyanyua juu heshima ya wazazi wawili na kuamrisha watendewe wema, na kulelewa vyema, na kuwa nao kwa upole. Kutoka kwa Abdullahi bin Amru R.A, anasema: Mtu mmoja alikuja kwa Mtume S.A.W, anamwomba idhini ya kwenda kupigana Jihadi. Mtume S.A.W, akamwambia: Je? Wazazi wako wako hai? Akasema: ndio. Basi kwao wao kapigane jihadi.

Na mabinti wawili wa Mtu Mwema katika Kisa cha Nabii Musa A.S, walikuwa ni mfano mzuri katika kumtendea wema na kumlea vyema baba yao. Kwani baba yao alikuwa Mtu mzima hajiwezi, na hana uwezo wa kufanya kazi, wao wawili wakawa wanafanya kazi badala ya baba yao, bila ya kunung’unika au kuchoshwa. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِّنَ النَّاسِ يَسْقُونَ وَوَجَدَ مِن دُونِهِمُ امْرَأَتَيْنِ تَذُودَانِ قَالَ مَا خَطْبُكُمَا قَالَتَا لَا نَسْقِي حَتَّى يُصْدِرَ الرِّعَاءُ وَأَبُونَا شَيْخٌ كَبِيرٌ}

Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana.

Na kutoka kwa Jabir R.A, anasema: Mtu mmoja alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakika mimi nina mali na watoto, na baba yangu anataka kuivamia mali yangu. Mtume S.A.W, akasema: Wewe pamoja na mali yako ni mali ya baba yako.

Na sisi tuna ruwaza njema kwa Bi Fatuma R.A, katika mapenzi yake, na heshima yake, na kuwa kwake mpole na baba yake Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, S.A.W; Bi Fatuma alikuwa Mtume S.A.W, anapoingia pale alipo, alikuwa Bi Fatuma akinyanyuka alipokaa, akambusu na kumkalisha baba yake pale alipokuwa ameketi yeye, kwa ajili ya kuwa mpole kwa baba yake na kwa furaha alio nayo, na pia kwa ajili ya kumpa cheo chake S.A.W.

Uislamu vile vile umetuamrisha tuwanyenyekee wazazi wawili na tusiwaudhi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا}

Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amemkataza Mwanadamu kusema hata neno dogo mno linaloashiria kukemea, hata kama ingekuwa kuna neno dogo kuliko neno “ah” basi Mwenyezi Mungu angelilizuia na kulikataza lisisemwe, kwa hivyo, ni bora kwa mtu kutosababisha maudhi kwa wazazi wawili, au kuwafanyia vitendo vibaya vya aina yoyote iwayo. Bwana wetu Abu Hurairah R.A, alimwambia mtu mmoja – alipokuwa akimpa mawaidha – Usitembee mbele ya Baba yako, na wala usikae kabla yake, na wala usimwite kwa jina lake, na wala usimsababishie kutukanwa. Kwani haifai kwa Mwislamu kuwasababishia wazazi wake maudhi ya aina yoyote. Anasema Bwana wetu Muhammad S.A.W: Hakika miongoni mwa madhambi makubwa ni mtu kuwalaani wazazi wake. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, vipi mtu annawalaani wazazi wake? Akasema: Mtu anamtukana mtu mwingine, kasha mtu huyo aliyetukanwa, anamtukana baba yake, na Mtu anamtukani mtu mwingine mama yake, kasha aliyetukaniwa mama yake nay eye anamtukana mama yake.

Na Uislamu umeusia kuwatendea wema wazazi wawili na kuwa nao kwa wema, hata kama watakuwa kinyume na Uislamu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَى أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا}

Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat’ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani.

 وهذا ما كان من سيدنا إبراهيم (عليه السلام) في دعوته مع أبيه ،  وفي ذلك يقول الحق سبحانه:

Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana wetu Ibrahim A.S, katika kumlingania Baba yake, na katika hili, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِبْرَاهِيمَ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا * إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا * يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا * يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَنِ عَصِيًّا * يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا}

Na mtaje katika Kitabu Ibrahim. Hakika yeye alikuwa mkweli, Nabii. Alipo mwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyo sikia, na visivyo ona, na visivyo kufaa chochote? Ewe baba yangu! Usimuabudu Shet’ani. Hakika Shet’ani ni mwenye kumuasi Mwingi wa Rehema. Ewe baba yangu! Hakika mimi naogopa isikupate adhabu inayo toka kwa Mwingi wa Rehema ukaja kuwa mwenziwe Shet’ani.

Tunaona kuwa Mtoto wa Abu Bakar R.A, Bi Asmaau binti Abu Bakar R.A, anajiwa na mama yake – akiwa mshirikina – anataka kuonana nae: Bi Asmaau akamuuliza Mtume S.A.W, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mama yangu alinijia akitaka kuonana na mimi, je? Ni unge nae undugu? Mtume S.A.W, akasema: Ndio. Unga undugu na Mama yako.

Hakika wema kwa wazazi wawili una athari nyingi na una faida kubwa na fadhila nzuri anazozipata mja Duniani na Akhera; miongoni mwa faida hizo ni: Sababu ya kupata radhi za Mola wake. Amesema Mtume S.A.W: Radhi za Mwenyezi Mungu ziko katika Radhi za Wazazi wawili, na hasira za Mwenyezi Mungu ziko katika kuwakasirisha wazazi wawili.

Na miongoni mwa matunda hayo ni kwamba hii ni sababu ya kuondoshewa magumu na mazito. Mtume S.A.W, ametutajia kisa cha Watu watatu ambao mvua ilipelekea wakimbilie pangoni kwenye jabali. Na jiwe kubwa likaangukia kwenye mlango wa Pango hilo na likauziba. Wakasema: Hakika mambo yalivyo, hakuna wa kukuokoeni na hili jiwe isipokuwa kumwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mema katika Matendo yenu. Akasema mmoja wao: Ewe Mola wangu Mlezi, hakika mimi nilikuwa nina wazazi wangu wawili waliozeeka mno, na nina watoto wadogo na nilikuwa nikiwachungia wanyama, na nilikuwa ninapowaendea nilikamua maziwa, na nikaanza kwa kuwapa Wazazi wangu, nikawa ninawanywesha maziwa hayo kabla ya watoto wangu, na Siku moja mimi nilichelewa na sikwenda kwao isipokuwa baada ya kufikiwa na jioni nilienda na nikawakuta wamelala, na nikakamua maziwa kama kawaida na nikasimama upande wa kichwani kwao nikichelea kuwaamsha na nikawa ninachukia kuwanywesha watoto wangu huku watoto wakilia kutokana na njaa huku wakiwa miguuni kwangu mpaka alfajiri ikachomoza. Ewe Mola wangu Mlezi ikiwa mimi nilifanya hivyo kwa ajili kutafuta radhi zako, tunakuomba utufungulie hili jiwe kiasi cha kuiona mbingu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawafungulia. Na wakaiona mbingu… hadi mwisho wa Hadithi. Kwa hiyo wema wake kwa wazazi wake ukawa ndio sababu ya kuondoshewa uzito na kuokoka kwake.

Na miongoni mwa matunda yake ni kwamba kuwatendea wema Wazazi wake ni kuwafanya watoto wake wamtendee yeye wema; kwani malipo hutokana na kazi iliyofanywa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alimzawadia Bwana wetu Ibrahim A.S, kwa Tabia zake njema kwa baba yake na kwa kumlingania kwake na kumtendea Wema, akajakutendewa wema na mwanae Ismail A.S. Na Qurani imetutajia hayo katika moja ya Sura za juu ya utiifu na Wema kwa Baba. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ}

Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.

Kuwatendea wema Wazazi Wawili pia kuna matunda yake hapa hapa duniani, kwani huwa sababu ya kuleta furaha kwa Mwislamu na Kesho Akhera huwa sababu ya kuingizwa Peponi. Mtu mmoja alimjia Mtume S.A.W, akimwomba idhini ya kwenda kwenye Jihadi. Mtume S.A.W, akasema: Je wewe una mama? Akasema: Ndio. Mtume akamwambia: Basi endelea kuwa nae karibu kwani Pepo iko miguuni mwake. Na anasema Mtume S.A.W: Mzazi ni Mlango wa kati katika Milango ya Peponi, ukitaka basi ulinde mlango huo au upoteze. Na amesema Bin Omar R.A akimwambia mtu: Je Wewe unauogopa Moto na unapenda uingizwe Peponi? Akasema: ndio, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ninapenda. Je? Wazazi wako wako hai? Akasema: Nina mama. Akasema: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, lau wewe ungeweza kuwa na kauli nzuri kwake, na ukamlisha chakula, basi hakika utaiingia Pepo iwapo utaendelea kujiepusha na Madhambi Makubwa.

Na sisi tunathibisha ya kwamba vyovyote vile mtu atakavyoweza kuwafanyia wazazi wake wawili katika wema basi hawezi kuwatoshelezea haki yao kamili na wala hawezi kuwalipa wema wao kwake. Anasema Mtume S.A.W: Mtoto hawezi kumlipa Mzazi wake isipokuwa labda akimkuta ni mtumwa akamnunua na kisha akwachoa huru.

Ninaisema kauli yangu hii, na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

* * *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mola wa Viumbe vyote. Na ninashuhudia ya kuwa Hakuna mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, asiye na mshirika yoyote, na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetuMuhammad, ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu mswalie, mrehemu na umbariki Mtume wetu, na Jamaa zake na Maswahaba wake wote, na kila mwenye kuwafuata wao kwa wema mpaka siku ya Malipo.

Ndugu zangu Waislamu,

Uislamu umeusia juu ya Wazazi Wawili na Ukausia pia kuhusu Ndugu, nao ni wale ambao mtu ana mfungamano nao kiundugu, na akawawekea haki zao.

Kama ulivyousia juu ya wazazi wawili, Uislau umeusia pia juu ya ndugu. Na ndugu ni wale ambao mtu anakaribiana nao kiundugu. Mwenyezi Mungu amewawekea haki zao. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَى بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّهِ}

Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu

Na Mtume S.A.W, anasema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameumba Viumbe na alipomaliza kuviumba, Kizazi kilisimama na kikasema: Hii ni nafasi ya Kisimamo cha anayejikinga kwako kutokana na kuukata undugu, akasema: Ndio. Je wewe huridhiki mimi nikakuunganisha na aliyekuunga wewe na nikamkata aliyekukata wewe? Kizazi kikasema: Ndio. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi nimekupa Jambo hilo. Kisha Mtume S.A.W, akasema: Mkipenda isomeni aya hii:

 {فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ تَوَلَّيْتُمْ أَنْ تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ * أُولَئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَى أَبْصَارَهُمْ}

Basi yanayotarajiwa kwenu mkitawala ndio mfanye ufisadi katika nchi a mwatupe ndugu zenu? Hao ndio Mwenyezi Mungu aliowalaani, na akawatia uziwi, na akawapofua macho yao.

Na anasema Mtume S.A.W: Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

Mimi ni Mwenyezi Mungu, na Mimi ni Rahmani, nimekiumba kizazi na nikakipa jina kutoka katika Majina  yangu, na yoyote atakaeunga undugu na mimi nitamuunga yeye, na atakaeukata undugu na mimi nitamkata.

Na kuunga undugu kinapatikana kwa kuwatembelea, na kuzijua hali zao, na kuwasaidia. Anasema Mtume S.A.W: Sadaka kwa Masikini ni Sadaka, na kwa ndugu ni maradufu; kuunga undugu ni Sadaka. Vilevile hupatikana kwa kuukubali mwaliko wao, na kumtembelea mgonjwa wao na kuhudhuria mazishi yao na pia kumuheshimu mkubwa wao na kumhurumia mdogo wao, na kusalimika na kuwa na nia njema kwa ajili yao, na kuwaombea dua.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia kuunga undugu kama ni sababu ya baraka katika Umri, na Ongezeko la riziki ambapo anasema Mtume wetu S.A.W: Anaependa kuongezewa Umri wake au aongezewe riziki yake basi awetendee wema Wazazi wake na aunge undugu.

Mtume S.A.W, ametuambia kwamba kuunga undugu ni sababu ya kusamehewa madhambi. Mtu mmoja alimjia Mtume S.A.W, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakika mimi nimefanya dhambi kubwa, je ninaweza kutubu? Mtume S.A.W, akamwambia: Je wewe una mama? Akasema: Hapana. Sina mama. Mtume akasema: Je wewe una Mama mdogo? Akasema yule Mtu: Ndio. Ninae Mama mdogo. Mtume akasema: basi mtendee wema.

     Kila mtu anapaswa kujihadhari na kukata undugu na asilipe ovu kwa ovu, bali asamehe na alipuuzie ovu alitendewa. Anasema Mtume S.A.W: Mwenye kuunga Undugu sio mtoa zawadi lakini muunga Undugu ni yule ambaye undugu wake unapokatika yeye huuunga.

Mtu mmoja alimjia Mtume S.A.W, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakika mimi nina ndugu huwa ninawaunga na wao hunikata, na huwatendea wema na wao hunitendea mabaya, mimi ninawajali na wao hawanijali. Mtume S.A.W, akasema: Ukiendelea kuwa kama ulivyo basi utakuwa kama vile umewamwagia majivu nyusoni mwao na Mwenyezi Mungu Mtukufu ataendelea kukunusuru kama utaendelea kufanya hivyo.

Uislamu umekataza kuukata undugu na ukatoa onyo kali juu ya mwisho wake mbaya Duniani na Akhera, ambapo anasema Mtume S.A.W: hakuna dhambi mbaya inayomfanya Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe kutoa adhabu kwa muhusika hapa hapa Duniani, pamoja na adhabu anayomwekea Akhera kuliko dhuluma na kukata undugu. Na anasema Mtume S.A.W: Haingii Peponi mtu mwenye kuukata undugu.

Tumche Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Wazazi wetu wawili, na tuunge undugu na tuwafanyie wema Watu wote.

Ewe Mola wetu Mlezi tuwafikishe katika kuwatendea wema wazazi wetu, na utujaalie tuwe ni wenye kuunganisha Undugu wetu, na uwalinde Watu wetu, na uijaalie Nchi yetu iwe na Amani, Utajiri na Maisha bora, salama Amani, pamoja na Nchi zote Duniani.