Haki za Vijana na Wajibu wa kila Mmoja wao

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa Viumbe vyote anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آَمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى}

Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye peke yake asiye na mshirika wake. Na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad S.A.W, ni Mja na Mjumbe wake.Ewe Mola wetu tunakuomba umswalie na umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Na baada ya utangulizi huu:

Hakika kipindi cha Ujana ni katika vipindi Muhimu mno kwa Umri wa Mwanadamu; Ni kipindi cha nguvu za kimwili na ukomavu na uchangamfu, na kutoa, Matumaini Mapana, na kuwa wazi kimaisha. Hapana shaka Kwamba vijana ni Nguzo Kuu ya Uma na ni Moyo wake unaodunda na ni mkono wake wenye nguvu na hakuna yoyote anaeweza kuukana mchango wao muhimu katika ujenzi wa Mataifa na katika Maendeleo ya Uma na Kuimarika kwake.

Na Qurani Tukufu imekielezea kipindi hiki cha Ujana kama ni kipindi cha nguvu kati ya unyonge wa aina mbili, unyonge wa utotoni na unyonge wa Uzeeni. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{اللَّهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْ بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِنْ بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً}

Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe.

Utume na Risala vilikuwa wakati wa umri wa Ujana. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kisa cha Bwana wetu Yusufu A.S:

{وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ}

Na alipo fikilia utu uzima tulimpa hukumu na ilimu. Na kama hivi tunawalipa wanao tenda mema.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Bwana wetu Musa A.S:

{وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَى آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا  وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ}

Na Musa alipo fika utu-uzima baraabara, tulimpa akili na ilimu. Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema.

 Ibnu Abas R.A, amesema: Mwenyezi Mungu Mtukufu hajawahi kumtuma Mtume isipokuwa Kijana, na wala hajawahi kupewa Elimu Mtu isipokuwa akiwa katika umri wa Ujana.

Tunamuona huyu kipenzi cha Mwenyezi Mungu Mtukufu Nabii Ibrahim A.S, alipambana na Watu wanaoyaabudu Masanamu akiwa Kijana. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ}

Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.

Qurani Tukufu vilevile imeashiria juu ya Utambuzi na Akili pevu ya Bwana wetu, Mtume Suleiman A.S, tena akiwa katika kipindi cha Ujana wake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَفَهَّمْنَاهَا سُلَيْمَانَ وَكُلًّا آتَيْنَا حُكْمًا وَعِلْمًا}

Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Musa A.S, alipewa Utume na Mwenyezi Mungu Mtukufu alipokuwa katika kilele cha Ujana wake, nguvu na uaminifu ambavyo vilipelekea Binti wa Mja Mwema wavielezee kwa baba yao, kama isemavyo Qurani Tukufu:

{قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ}

Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amemsemesha Yahya A.S, ili asimame kwa amana ya Elimu na kulibeba jukumu la Ulinganiaji, kwa nguvu zote na azma ya Vijana, akasema:

{يَا يَحْيَى خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا}

Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa hikima angali mtoto.

Na kutokana na umuhimu wa kipindi hiki cha Ujana, Mtume S.A.W, amebainisha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atamuuliza Mja Wake swali maalumu Siku ya Kiama mpaka ajitahidi mtu kunufaika na Ujana wakena kuutumia vizuri kwa manufaa yake na ya Watu wote. Akasema Mtume S.A.W: Miguu ya Mja wangu siku ya Kiama haitapumzika mpaka aulizwe mambo manne; Aulizwe kuhusu Umri wake na ameumalizaje? Ujana wake aliumalizaje? na Mali yake aliichumaje na akaitumiaje? Na Elimu yake aliifanyia nini?

Na Uislamu umewahimiza sana vijana kwa himizo kubwa, na ukawajaalia majukumu, kwani wao wana haki ya kusomeshwa, Kuongozwa na kuandaliwa vizuri. Na Qurani Tukufu imelizungumzia jambo hili kwa yale aliyoyasema Luqmaani mwenye Hekima na Busara alipokuwa na mwanae. Ambapo yeye alipandikiza ndani ya kijana wake pande mbalimbali za Kidini na akamuasa awe mwema na mwenye kujitolea na ajipambe na Maadili mema. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ }

Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّهُ إِنَّ اللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ * يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ * وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ * وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ}

Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote. Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda.

Na hivyo ndivyo alivyokuwa Mtume S.A.W, anafanya anapokuwa na vijana. Akawa Mtume S.A.W, ana hima kwao kwa kiwango kikubwa mno na anapupia katika kuwawezesha kielimu na kuwaandaa vilivyo na alikuwa anapandikiza nyoyoni mwao na katika akili zao Misingi ya Dini Tukufu ya Uislamu na kupenda Elimu na Kujiwekea Sifa maalum. Kutoka kwa Ibnu Abas R.A, amesema: Nilikuwa nyuma ya Mtume S.A.W, Siku moja, akasema: Ewe kijana, mimi ninakufundisha maneno haya; Mlinde Mwenyezi Mungu Mtukufu naye atskulinda. Mlinde Mwenyezi Mungu Mtukufu utamkuta upande wako. Unapoomba basi mwombe Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na unapotaka msaada mwombe Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ujue kwamba kama Uma wote ungelikusanyika ili ukusfae kwa kitu chochote usingeliweza kukufaa isipokuwa kwa kitu alichokuandikia Mwenyezi Mungu Mtukufu na kama wangelikusanyika ili wakudhuru kwa kitu chochote wasingeliweza kukudhuru isipokuwa kwa kitu alichokuandikia Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kalamu zimekwisha nyanyuliwa, na vitabu vimekwisha kauka.

Na baada ya Elimu bora na Mafunzo yaliyokamilika, inafuatia haki ya vijana katika kuwawezesha na kuwapa msukumo – kila mmoja kwa mujibu wa uwezo na Sifa alizonazo – katika maeneo ya kazi au Uongozi na Majukumu. Na hivi ndivyo Mtume S.A.W, alivyofanya ampo aliwaajiri vijana wenye nguvu mbali mbali. Na akawasukuma ili waingie katika vita vya maisha; Mtume S.A.W, alimwamini kijana wakati wa Ulinganiaji wake, ambae Umri wake hauzidi miaka ishirini, nae ni Arqam R.A, ambae nyumba yake ilikuwa Makao Makuu yenye Usalama kwa Mtume S.A.W, na Maswahaba wake mwanzoni mwa Ulinganiaji wa Uislamu. Mtume vilevile, alimpa uongozi wa Jeshi la Waislamu, Usama bin Zaid R.A, na Umri wake Wakati huo ukiwa haujavuka miaka kumi na nane.

Omar bin Khatwab R.A, alikuwa akiwaita vijana katika makao yake pamoja na wazee katika kila jambo, na anasema: Hakatazwi yoyote miongoni mwenu kwa udogo wa Umri wake kutoa maoni yake, kwani hakika ya Elimu haimo kwa wadogo wala kwa wakubwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anaiweka atakapo. Na kwa hivyo katika Makao yake walikuwapo vijana akiwamo Abdullahi bin Abas R.A, ambaye Omar R.A, alikuwa akimzungumzia kwa kusema: Hakika Kijana huyu ana ulimi wenye kujitambua na moyo wenye akili.

Na jambo hili halijawahi kuishia kwa vijana wa kiume tu, bali na wa kike pia wana mchango wao usiopingika wa Ujenzi wa Ustaarabu wa Kiislamu, wao walikuwa na mchango wao Wakati wa amani na wakati wa vita. Miongoni mwao ni Bi Asmaa Binti Abuu Bakar Sidiiq, R.A, na mchango wake wa wazi katika Hijra ya Mtume S.A.W, na baba yake R.A, ambapo yeye Asmaa alikuwa anawaandalia chakula na vinywaji  Mtume na Baba yake Abu Bakar Wakati wa Hijra tukufu, bali wanawake walikuwa na mchango katika nyakati nzito na ngumu kuliko zote. Na Katika viwanja vya mapigano, Wanawake walikuwa wakiwanywesha maji wapiganaji na wakitoa huduma ya kwanza kwa wenye kujeruhiwa, na katika hilo ni kama ilivyokuwa katika siku ya vita vya Uhudi. Anasema Anas R.A: Nilimwona Aisha binti Abu Bakar R.A, na Umu Sula8m wakisambaza viriba vya maji migongoni mwao kisha wanavimaliza kwa kuwagawia watu maji hayo kisha wakarejea tena na kuvijaza viriba hivyo kisha kuja navyo na kuwagawia watu maji.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na nyinyi.

* * *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa Viumbe vyote, na ninashudia ya kwamba hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake asiye na mshirika wake, na ninashudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu mswalie, marehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Ndugu zangu Waislamu:

Hakika vijana wana majukumu mengi. Na la Kwanza: Kujiimarisha kielimu na kitamaduni, pamoja na kuendeleza kujielimisha huko kwani Elimu daima inasonga mbele kila dakika na hapana budi kwa vijana wetu kwenda sambamba na maendeleo na matukio ya Ulimwengu huu na kuchunga mahitaji ya soko la kazi, na mahitaji ya taifa, na kwa hivyo kujiongezea elimu kwa njia za mipango ya masomo na mafunzo na zoefu zinazohitajika mpaka vijana hawa wawe na uwezo wa kupambana na changamoto zilizopo. Na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hakumuamrisha Mtume wake S.A.W, kujiongezea chochote katika vitu vya duniani isipokuwa Elimu ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu, akimwambia Mtume wake S.A.W:

{وَقُلْ رَبِّ زِدْنِي عِلْمًا}

Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie ilimu

Tatu: Kujihimiza katika kunufaika na zoefu mbali mbali na kujihadhari na kudanganyika. Vijana wanapaswa wanufaike na hekima na uzoefu wa watangulizi wao wenye uzoefu kwani uhusiano baina ya vizazi vinavyofuatana sio uhusiano wa kupuuziana au kukinzana; bali ni uhusiano wa kushirikiana kikamilifu na Kunasihiana, na vijana wetu wajihadhari na majivuno ambayo huwa yanabomoa na wala hayajengi, bali humuangamiza muhusika. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kitabu chake Kitakatifu:

{وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولً}

Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.

Anasema Mtume wetu S.A.W: Mambo matatu huangamiza: Uchoyo wenye kunyenyekewa, na matamanio ya nafsi yanayofuatwa, na mtu kupendezwa mno na maoni yake, kupindukia.

Tatu: Kuweka nia upya kwa ajili ta kuitumikia Dini na Nchi. Mwanadamu hulipwa kwa mujibu wa Uzuri wa nia yake katika Kazi yake, na ukweli wa nia yake. Anasema Mtume S.A.W: Hakika matendo hutokana na Nia, na kila Mtu hukipata kile alichokinuia…

Nne: Ni Kuitumia fursa kwa kuongeza juhudi zaidi na kutambua kuwa Njia ni ndefu na Amana ni Nzito sana, kwa kuwa sisi tunaishi katika jamii inayoendelea kwa kasi kubwa mno na hakuna nafasi ya kwa wale wasio na bidii na wasiozijali kazi zao, na hasa katika kutekeleza kazi walizopewa wazitekeleze. Ili tuweze kufanikisha matarajio yetu na kuifikia nafasi yetu, ambayo sisi wenyewe tunaitarajia na kwa ajili ya taifa letu hapana budi tujitume kwa nguvu zote na juhudi zetu kwa mapana zaidi katika Kazi Zeru.

Tano: Kuurejesha wema kwa Taifa ambalo limetulea na sisi tukakulia ndani yake likatusomesha na kutuwezesha; Taifa lina haki kwa wananchi wake ambao wameishi ndani yake na wakalelewa na kujipatia uzoefu wake na wana wao ndani ya Taifa hilo kumbukumbu na historia zao na iwe nguvu yetu ni kuwa na msimamo na kuwa na nia isiyotetereka, na silaha yetu iwe Elimu na Ubunifu, na kauli mbiu yetu iwe Uzalendo na Kujitolea; kwa ajili ya kulitumikia taifa letu hili na kulilinda.

Ewe Mola wetu Mlezi wabariki vijana wetu, na uwalinde na kila ovu, na uwawafikishe katika Ujenzi na Uimarishaji wa nchi, na uwaongoze katika mambo yenye masilahi kwa Nchi yao na kwa. Watu wake, na Uilinde Nchi yetu na nchi zote Duniani.