Maana ya Matendo Mema na Matendo Maovu

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote, anaesema katika Qurani tukufu:

{مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ}
Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja.
Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana Wetu na Mtume wetu Muhammad Ni Mja na Mjumbe wake, anaesema katika Hadithi aliyoipokea kutoka kwa Mola Wake Mtukufu: …enyi Waja wangu, hakika ni matendo yenu ninayoyahesabia kwa ajili yenu kisha nitakulipeni kutokana na matendo hayo, na atakayeikuta heri basi amhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu, na atakayekuta kinyume na hivyo basi asimlaumu yoyote isipokuwa nafsi yake mwenyewe.
Ewe Mola weyu Mlezi tunakuomba umswalie umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote na kila mwenye kuwafuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.

Na baada ya Utangulizi huu:
Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtukuza mwanadamu, na akamuumba kwa mikono yake na akamuumba kwa uzuri wa maumbile akiwa amenyooka, kisha akampulizia roho yake, na akamtofautisha kwa kumpa akili, na akawasujudisha Malaika kwake, kisha akakudhalilishieni vilivyomo ndani ya Ulimwengu huu, na akakufanyenyi muwe bora zaidi kuliko viumbe vyake vingi, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي ءَادَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ في الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُمْ مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلاً}
Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba.

Hayo ni kwa kuwa Mwanadamu ameibeba Amana nzito iliyotangazwa kwa Mbingu, Ardhi na Majabali na vyote vikakataa kuibeba na Mwenyezi Mungu Mtukufu akavionea huruma; hii ni amana ya kubeba majukumu ambayo yanapelekea Kuhangaika na Kufanya kazi kwa bidii, na kuijenga Ardhi pamoja na kutekeleza Ibada za Faradhi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ}.
Na itakapo kwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa.

Kwa hiyo, mwislamu anatakiwa ajue Kuwa kila anachokifanya katika maisha yake katika matendo basi kitakuwa katika mizani ya Mema yake au mabaya yake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{فَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَه * وَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَه}
Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona! Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُّحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِن سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ وَاللَّهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ}
Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya yamehudhurishwa, na pia ubaya ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako masafa marefu baina ya ubaya huo na yeye. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.

Na maana ya kazi inajumuisha: Kila kitu anachokifanya Mwanadamu, kiwe ni kauli au kitendo. Na Kitendo chochote chema sharti lake kiwe ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mtendaji atende kikamilifu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ}
Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anapenda pindi mmoja wenu anapofanya kazi basi aitekeleze ipasavyo.
Hakuna Shaka yoyote kwamba maana ya tendo jema katika Uislamu ni pana mno, na inakusanya yale aliyoyafaradhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Ibada kama vile; Sala, Kufunga, Zaka, Hija na nyingine nyingi mfano wa hizo, nazo ni katika misingi, Ibada ambazo mwislamu lazima azitekeleze. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ}
Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ}
Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt’iini Mtume, ili mpate kurehemewa.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Usafi ni sehemu ya Imani, na kusema Alhamdu lillah hujaza mizani, na kusema: Subhaanallah walhamdu lillaahi hujaza eneo la baina ya mbingu na ardhi, na Sala ni Nuru, na Sadaka ni alama ya Wema, na Subira ni mwangaza, na Qurani ni hoja yako au dhidi yako, Watu wote wataondoka kwa hivyo basi kuna anayeuza nafsi yake na kisha akaikomboa na kuipa uhuru, au akaiangamiza.
(الطُّهُورُ شَطْرُ الإِيمَانِ ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ تَمْلأُ الْمِيزَانَ ، وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ تَمْلآنِ – أَوْ تَمْلأُ – مَا بَيْنَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ ، وَالصَّلاَةُ نُورٌ ، وَالصَّدَقَةُ بُرْهَانٌ ، وَالصَّبْرُ ضِيَاءٌ ، وَالْقُرْآنُ حُجَّةٌ لَكَ أَوْ عَلَيْكَ ، كُلُّ النَّاسِ يَغْدُو ، فَبَائِعٌ نَفْسَهُ ، فَمُعْتِقُهَا ، أَوْ مُوبِقُهَا).

Na katika matendo Mema ambayo mwislamu anapaswa ajipambe nayo, ni: Ukweli, kauli nzuri, kusalimia Watu, na mengine mengi yanayomfanya mwanadamu awe anajongeleka na anawajongelea wenzake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَقُلْ لِعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ}

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{لَا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِنْ نَجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا}
Hakuna kheri katika mengi ya wanayo shauriana kwa siri, isipo kuwa kwa yule anaye amrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutakuja mpa ujira mkubwa.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا}
Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo.

Na hii inathibitisha kwamba wanaojishughulisha na kilimo, viwanda na biashara wana malipo makubwa zaidi kwa Kiwango cha juhudi wanazozitumia katika kazi zao pamoja na viwanda ambavyo ndio msingi wa maisha kama vile viwanda vya chuma cha pua. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَأَنْزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ}
Na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا}
Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu!

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika utengenezaji wa mavazi:
{وَمِنْ أَصْوَافِهَا وَأَوْبَارِهَا وَأَشْعَارِهَا أَثَاثًا وَمَتَاعًا إِلَى حِينٍ}
Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَجَعَلَ لَكُمْ سَرَابِيلَ تَقِيكُمُ الْحَرَّ وَسَرَابِيلَ تَقِيكُمْ بَأْسَكُمْ }
na amekufanyieni maskani milimani, na amekufanyieni nguo za kukingeni na joto lenu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika utengenezaji wa ngozi:
{وَجَعَلَ لَكُمْ مِنْ جُلُودِ الأَنْعَامِ بُيُوتًا تَسْتَخِفُّونَهَا يَوْمَ ظَعْنِكُمْ وَيَوْمَ إِقَامَتِكُمْ}
…na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu.

Matendo mema hayaishii katika kuwanufaisha Watu tu bali yanakusanywa pia manufaa kwa wanyama na vitu vingine vyote. Mtume S.A.W, alipo pita mbele ya ngamia anaeteseka na akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Wanyama hawa wafugwao, basi wapandeni kwa Wema na muwaachie kwa Wema.
Na anasema Mtume Wetu S.A.W: Mtu mmoja alipokuwa akitembea njiani alikuta tawi moja lenye miba likiwa njiani akaliondosha na kisha akamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu akamsamehe madhambi yake.
Na Mtume Wetu S.A.W, anasema: nimemuona Mtu akigeuka geuka peponi kwa sababu ya mti alioukata akiwa njiani, mti huo ulikuwa unawaudhi Watu.
Na upande wa matendo mabaya, ni yale yote yanayomuudhi Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yanamtoa mtu katika wigo wa kuwa utengenezaji kuelekea katika uharibifu, na akawa mtu huyo anaanza kujiweka mbali na Utiifu wa faradhi na kufanya yanayo katazwa na machafu kama vile kuwatendea ubaya wazazi wawili na kuzishambulia mali na heshima za Watu, na katika hayo: Mtu anajitoa katika majukumu yake kwa familia yake, na kuzembea katika kuwatunza watoto wake na kutowapa malezi bora. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا}
Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto…

Na anasema Mtume Wetu S.A.W: Inamtosha mtu kupata madhambi kwa kuwatelekeza wale anaowalea na kuwalisha.

Na miongoni mwa matendo maovu ni: Ufisadi ardhini, na kueneza fikra angamizi na vumi za uongo, na kuwatishia usalama Watu walio na amani. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَلاَ تُفْسِدُوا فِي الأَرْضِ بَعْدَ إِصْلاحِهَا}
Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الأَرْضِ فَسَادًا أَنْ يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُمْ مِنْ خِلافٍ أَوْ يُنفَوْا مِنَ الأَرْضِ ذَلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنيَا وَلَهُمْ فِي الآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ}
Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَلا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الأَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ}
Na wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.

Na anasema Mtume Wetu S.A.W: Mbora wenu ni yule ambaye Kheri yake inatarajiwa, na Shari yake inazuilika, na Mshari wenu ni yule ambaye Kheri yake haitarajiwi na watu hawasalimiki na Shari yake.
Na katika hilo katika hilo: Kuleta madhara barabarani. Kufanya hivyo ni Madhambi makubwa mno, ambapo anasema Mtume S.A.W: Hakuna kujidhuru au kuwadhuru watu wengine. Na anasema Mtume S.A.W: Mtu yoyote atakaye waudhi waislamu njiani basi laana yao itamwajibikia.
Na kuna mambo yansyopandikiza chuki baina ya Watu na kuwasababishia maudhi katika hali na mali zao, kama vile: Kuteta, kusengenya, Umbea na Utani uliopindukia, Kuitana majina mabaya, Kutukana na kutoa maneno machafu, na mengine mengi yaliyokatazwa na Uislamu na yanakinzana na Tabia za Kiislamu na Maumbile yaliyosalimika na mienendo yenye hadhi na ya kistaarabu. Anasema Mtume wetu S.A.W: Hakika Mtu ninayemchukia sana miongoni mwenu ni wale wenye kutembea na kusambaza maneno kwa Watu, wanaowatenganisha ndugu walio pamoja na wanaopendana
المُلْتَمِسُونَ لِلْبُرّاءِ العَنَتَ) .
Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni Nyinyi.
* * *
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye pekee asiye na mshirika wake na ninashuhudia ya kwamba Bwana Wetu na Mtume wetu ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola Mlezi tunakuomba umswalie umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote na kila atakayewafuata mpaka siku ya Kiama.

Ndugu zangu Waislamu:
Hakika kila amali anayoifanya mja humrejea yeye mwenyewe Duniani na Akhera. Na katika matunda ya amali njema ni: Maisha mazuri Duniani na Akhera, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ}
Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.

Na miongoni mwake: Ni kuendelea na Malipo baada ya kufariki Dunia. Anasema Mtume wetu S.A.W: Mambo saba Malipo yake huendelea kwa mja akiwa kaburini mwake: Atakayeifundisha elimu, au akauchimbua mto, au akachimba kisima, au akapanda mtende, au akajenga msikiti, au akarithisha Msahafu, au akaacha mtoto atakayemwombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kufa kwake.
Na kwa hayo mambo saba kuna kusamehewa madhambi ya mja na kuyageuza yakawa Mema yake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَحْسَنَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ}
Na walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.

Na miongoni mwake: Malipo Makubwa, na kuwa karibu na Manabii, Wasema kweli na Mashahidi, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{ إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا}
Hakika wale walio amini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{ وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا}
Na wenye kumt’ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!

Kwa kuwa matendo mema yana malipo yake, na matendo mabaya pia yana athari zake ambazo zinamwangukia muhusika wake Duniani na Akhera, na miongoni mwake ni: Upotofu na Mzubao na Kuchanganyikiwa. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{أَفَمَنْ زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا فَإِنَّ اللهَ يُضِلُّ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي مَنْ يَشَاءُ}
Je! Yule aliye pambiwa a’mali zake mbaya na akaziona ni njema – basi hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye. Na miongoni mwake: Maisha yenye mgongano na yasioyotulizana, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنْكًا}
Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki…

Na miongoni mwake: Ni mwelekeo mbaya siku ya Kiama. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَى ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا}
Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.

Na Mtume S.A.W, anasema: Mtu yoyote atakayechukua kitu chochote ardhini ambacho sio haki yake basi atadidimizwa nacho siku ya Kiama mpaka ardhi ya saba.
Basi ubora ulioje wa sisi kushikamana na kila jambo zuri lenye manufaa, na tujiepushe na kila jambo baya lenye madhara, na tukausiana na tukashirikiana katika Haki. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{وَالْعَصْرِ * إِنَّ الْإِنْسَانَ لَفِي خُسْرٍ * إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ}
Ninaapa kwa zama! Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika khasara, Ila wale walio amini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri.

Ewe Mola Wetu tunakuomba utujaaliwe tuwe watenda mema, tuyaache mabaya, tuwapende masikini, na uturuzuku moyo mkunjufu wa Imani na Kukubaliwa Dua, na uilinde Nchi yetu na kila jambo baya, na uzilinde Nchi zote Duniani.