Maadili ya Kibinadamu katika Suratil Hujuraat

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ}

Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye kuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana Wetu na Mtume Wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake, anayesema: Hakika yangu mimi nimetumwa kwa ajili ya kuja kuyakamilisha Maadili Mema ya Tabia. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, tunakuomba umswalie umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote na kila atakayewafuata mpaka siku ya Malipo.

Na baada ya Utangulizi huu:

Qurani tukufu imejaa aya nyingi mno ambazo ni Msingi wa Tabia njema na Maadili ya hali ya juu, bali kuna sura kamili imekuja kama taasisi kwa ajili ya Jamii iliyopevuka, kama vile Suratul Hujuraat ambayo imeweka mkusanyiko wa misingi imara ya Maadili na Tabia njema, miongoni mwa Misingi hiyo: Kubainisha na na Kuthibitisha mambo yote kikamilifu, na hasa iwapo kuna kuna jambo linalohusiana na mambo ya Watu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَنْ تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَى مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ}

Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda.

Kwa hivyo, Uislamu unakijenga kila kitu kwa msingi wa kuwa na yakini nacho. Tumwangalie Mtume Wetu Suleiman A.S, alipoijiwa na Hudhud kwa habari inayowahusu Watu wanaoabudu Jua kinyume na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akaielezea kuwa ni habari ya yakini, Nabii Suleiman hakuyachukua maneno ya Hudhud kama yalivyo, bali aliyahakikisha Kwanza kama ni ya kweli na yakadhihirika kuwa ni ya kweli kama inavyosikulia Qurani tukufu, katika Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{قَالَ سَنَنْظُرُ أَصَدَقْتَ أَمْ كُنْتَ مِنَ الكَاذِبِينَ}

Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.

Mtume S.A.W, anasema: Inamtosha mtu kupata madhambi kwa kuhadithia kila anachokisikia.

Imamu Nawawiy Mola amrehemu, anasema: Hakika mtu kwa kawaida huwa anasikia maneno ya kweli na ya uongo, na iwapo atahadithia kila anachokisikia atakuwa amesema uongo kwa kutoa habari za mambo ambayo hayajatokea. Mtu mmoja alipoingia kwa Bwana Wetu Omar bin Abdul Aziiz R.A, na akamzungumzia mtu kuhusu kitu fulani, Omar akamwambia: ukitaka tutaliangalia Jambo lako kwa kina; na ukiwa muongo basi wewe utakuwa ni miongoni mwa Watu wa Aya hii:

{إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا}

Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni…

Na ukiwa mkweli basi utakuwa miongoni mwa Watu waliomo katika Aya hii ifuatayo:

{هَمَّازٍ مَشَّاءٍ بِنَمِيمٍ}

Mtapitapi, apitaye akifitini.

Na ukitaka tutakusamehe. Akasema yule mtu: Ninaomba msamaha Ewe Kiongozi wa Waumini, sitarejea tena kitendo hiki.

Kama kila mmoja wetu Atakuwa na pupa ya kutaka kuthibitisha jambo na kulijua undani wake kabla ya kuhukumu au kabla ya kusambaza kwa Watu kila kitu anachokipata, basi uvumi wa aina yoyote ungepoteza nguvu zake na athari yake, na wasambazaji wake wangezuilika kueneza kwa Watu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَا يَغْتَبْ بَعْضُكُمْ بَعْضًا أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَنْ يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ رَحِيمٌ}

wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.

Na kutoka kwa Abu Huraira R.A, kwamba Mtume S.A.W, amesema: Je mnajua Kuteta ni nini? Wakasema: Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake ndio wanajua zaidi. Akasema: Ni kumtaja ndugu yako kwa yale asiyoyapenda. Pakasemwa:  Je unaonaje kama niyasemayo ndugu yangu anayo? Akasema: ikiwa katika uyasemayo yamo yanayomuhusu utakuwa umemsengenye. Na kama hakuna utakuwa umemzushia uongo. Na mtu hauelekei usengenyaji isipokuwa kwa kujishughulisha na kasoro za Watu na kuziacha kasoro zake yeye mwenyewe. Anasema Mtume S.A.W: Mtu hukiona kasoro ndogo  katika jicho la Ndugu yake, na anasahau kasoro kubwa iliyo katika macho yake!

Bali hakika mtu anatakiwa awe tayari kuitetea heshima ya ndugu yake. Anasema Mtume S.A.W: Yoyote atakayeitetea heshima ya ndugu yake, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atauepusha uso wake na Moto Siku ya Kiama.

Na miongoni mwayo: ni kuepukana na kuvunjiana heshima. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ}

Wala msivunjiane hishima…

Kwa maana kwamba kila mmoja wenu asizitoe aibu za mwenzake, na huko kuaibishana kunaweza kukawa kwa Kauli au kwa Vitendo, na Qurani tukufu imekataza kuvunjiana heshima kwa aina zote mbili. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَيْلٌ لِكُلِّ هُمَزَةٍ لُمَزَةٍ}

Ole wake kila safihi, msengenyaji!

Na hao ni wale ambao wanawaaibisha Watu na kuwatia kasoro na wanawaita kwa sifa na majina mbalimbali wasiyoyaridhia. Na onyo hili ni kwa Watu wenyekuwavunjia heshima ndugu zao kwa kauli au kwa Vitendo, na ni kiasi cha Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwateketeza vikali wale wote watakaofanya hivyo. Na kutoka kwa Abu Masuud R.A, amesema: tulipoamrishwa tutoe sadaka tulikuwa tunatoa kwa uzito, akaja Abu Aqiil akiwa na Nusu ya kibamba, na akaja Mtu mwingine na ujazo wa nafaka zaidi ya Abu Uqail, wanafiki wakasema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni tajiri asiyehitaji Sadaka hii, na huyo mwingine hakufanya hivyo isipokuwa kujionesha tu. Hapo ndipo ilipoteremshwa aya hizi:

{الَّذِينَ يَلْمِزُونَ المُطَّوِّعِينَ مِنَ المُؤْمِنِينَ فِي الصَّدَقَاتِ وَالَّذِينَ لاَ يَجِدُونَ إِلَّا جُهْدَهُمْ فَيَسْخَرُونَ مِنْهُمْ سَخِرَ اللَّهُ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ}

Wale wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka nyingi na wasio nacho cha kutoa ila kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli. Mwenyezi Mungu atawakejeli wao! Nao watapata adhabu chungu!

Na miongoni mwayo ni: kutowadharau Watu na kuwatania: Muumini wa kweli hapaswi kuwatania Watu na kuwadharau. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَى أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَى أَن يَكُنَّ خَيْرًا}

Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao.

Didi yetu ya Uislamu imetukataza kila kitu kinachomuudhi mtu mwingine, kwani miongoni mwa sifa za mwislamu ni kutomuudhi mtu yoyote yule, na asifanye isiwafanyie Watu isipokuwa kheri tupu na manufaa kwa Watu hao.

Mtume S.A.W, alikuwa akizuia kila kitu kinachoweza kuziudhi hisia za mtu, iwe kitu hicho ni kauli au kitendo, au ishara. Mtume S.A.W, akawa anaingiza ndani ya mtu hisia zinazomuongezea mtu huyo hadhi yake na fadhila zake kwa Watu. Kutoka kwa Ummu Muda, amesema: Abdallah bin Masuud alitajwa kwa Ali R.A, na Ali R.A, akawa anazitaja fadhila zake kisha akasema: Kuna mara moja aliwahi kupanda juu ya mti akataka kuwachumia matunda wenzake, wenzake hao wakacheka sana kutokana na wembamba wa miguu yake, na Mtume Wetu S.A.W, akasema: Mnacheka nini? Miguu hiyo ni mizito zaidi katika mizani siku ya Kiama kuliko yoyote.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

  * * *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehma na amani zimfikie Mtume wa mwisho; Bwana Wetu Muhammad, yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote na wenye kuwafuata.

Ndugu zangu Waislamu:

Hakika Maadili yaliyo juu zaidi ni yale yaliyolinganiwa na katika Suratul Hujuraat, kwa ajili ya kuuinua juu Msingi wa Undugu na Kuwapatanisha watu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ}

Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.

 

Kwa hiyo kuwapatanisha watu ni katika Maadili bora zaidi yaliyolinganiwa na Suratul Hujuraat na ambayo, Dini yetu ya Uislamu iliyo Tukufu ambayo inaweka misingi kutoka katika Suratul Hujuraat, kwa ajili ya Jamii ya kibinadamu yenye mshikamano na Usamehevu, na inafanya kazi ya kuweka msingi wa Maadili ya kuishi kwa pamoja katika mazingira ya kuongelea ni na ukaribiano, mbali na ugomvi. Na hii ni tiba ya kila aina ya magomvi na mivurugano.

Na katika Mazingira ya familia, Qurani tukufu inatulingania pale inapotokea migongano baina ya wanandoa, na wakashindwa kupata suluhisho, basi wanatakiwa kutuma mtu atakayeweza kuwasaidia miongoni mwa ndugu wa kila upande, ili kuwatafutia ufumbuzi wa Suala lao. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِنْ أَهْلِهَا إِنْ يُرِيدَا إِصْلاحًا يُوَفِّقِ اللَّهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا}

Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye khabari.

 

Na Moyo huu wa kusuluhisha unapanuka zaidi na kuelekea katika Jamii ili Jamii hiyo iwe ni yenye kusameheana. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{لاَ خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِنْ نَجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلاَحٍ بَيْنَ النَّاسِ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاةِ اللَّهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا}

Hakuna kheri katika mengi ya wanayo shauriana kwa siri, isipo kuwa kwa yule anaye amrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutakuja mpa ujira mkubwa.

 

Na Mtume S.A.W, amebainisha malipo ya kusuluhisha watu na Athari ya uharibifu, katika kauli yake: Je nikuambieni daraja bora kuliko sala na Sadaka? Wakasema: Ndio Ewe Mtume Wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akasema: Ni kuwasuluhisha waliogombana. Na ubaya wa ndugu waliogombana hunyoa. Sisemi kwamba hunyoa nywele bali huinyoa Dini yenyewe.

 

 

Kwa hiyo, Muumini wa kweli hukuweka kusuluhisha kama mfumo wa maisha yake. Hapo tunakuta kuna kheri nyingi. Anasema Mtume Wetu S.A.W: Hakika wapo miongoni mwa Watu wana funguo za kheri na kufuli za Sharo, na miongoni mwa Watu wapo wenye funguo za shari na kufuli za kheri. Uzuri ulioje kwa wale wenye funguo za kheri mikononi mwao, na ole wake yule ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu amemjaalia awe na funguo za shari mikononi mwake.

 

Ewe Mola Wetu tunakuomba utuongoze tuzifikie Tabia zilizo njema zaidi, kwani hakika mambo yalivyo hakuna wa kutuongoza kuelekea katika tabia njema zaidi isipokuwa wewe, na tunakuomba utuepushie Tabia mbaya, kwani hakika hakuna wa kutuondoshea Tabia mbaya isipokuwa wewe. Na tunakuomba utuilinde Nchi yetu na Nchi zote Ulimwenguni.