Katika makaribisho ya Suratul Israa

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote ambaye  alimchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali. Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana Wetu na Mtume Wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu tunakuomba umswalie umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote na kila atakayewafuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo. Na baada ya Utangulizi huu,

Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu aliiunga mkono Mitume yake A.S, kwa Miujiza, na miongoni mwa Miujiza hiyo: Ni ule Muujiza wa Israa na Miiraji kwa Mtume Wetu Muhammad A.S.W, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آَيَاتِنَا إِنَّه هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ}.

 Ametakasika Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.

Na yoyote atakaezingatia akilini mwake Muujiza huu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuta kuwa unabeba mafunzo mengi, na katika hayo ni:

Kuubainisha Uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu usio na mipaka, kwani Utashi wake hauendani na kanuni zozote za Sababu, na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ}.

Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa. 

Na miongoni mwake ni:  Wepesi baada ya Ugumu na Faraja baada ya Dhiki, na baada ya kuvumilia Mtume S.A.W, aina mbalimbali za maudhi ya Washirikina, akiwa katika njia ya Ulinganiaji na Ufikishaji wa Risala ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ukaja Muujiza wa Israa na Miiraji kama ni kumkirimu na kumuunga mkono Mtume S.A.W, na ni Kigezo cha kumfariji Mtume baada ya kuwa na Mazito, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا *إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا}.

Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi, Hakika pamoja na uzito upo wepesi.

Na miongoni mwake ni: Utukufu wa Cheo cha Uja, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَأَوْحَى إِلَى عَبْدِهِ مَا أَوْحَى}

Na  (Mwenyezi Mungu) akamfunulia mja wake alicho mfunulia.

Kwa hiyo, Uja kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Utukufu na Heshima nalo ni lengo lake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Waja wake, na Risala ya Manabii wote.

Na miongoni mwake ni: Ubainifu wa Nafasi ya Msikiti wa Wasaa, kwani huko ndiko alikopelekwa Mtume S.A.W, na huko ndiko alikopandishwia Mbinguni katika Miiraji, na Msikiti huo ni moja ya Kibla mbili za Waislamu, na ni wa Tatu kwa Utukufu baada ya wa Makkah na wa Madina. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape msimamo wenye kuulinda Msikiti huo na aurejeshe kwa Waislamu kwa Wema.

Na miongoni mwake ni: Utukufu wa Cheo cha Sala, na ubainifu wa Fadhila zake na sifa zake maalumu, kwani Mtume Wetu S.A.W, alipopelekwa alifikishwa mpaka katika Eneo la Sidtstul Muntahaa; kwenye umbingu wa Sita… na akapewa mambo matatu: Sala tano, Aya za mwisho wa Suratul Baqarah, na kusamehewa kwa yule atakayekufa katika Umma wake bila kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na chochote.

Na miongoni mwake ni: Kubainisha Mafungamano ya pamoja baina ya Dini za Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambapo anasema Mtume Wetu S.A.W: … Manabii ni ndugu wa baba mmoja mama mbalimbali na Dini yao ni moja. Na hakika Mitume na Manabii wote walikusanyika Usiku wa Israa na Miiraji na Mtume S.A.W, akawasilisha kama imamu wao na wakamkarobisha na kumwombea dua kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na miongoni mwake ni: Kutumia sababu au njia za kufanikiwa. Mtume S.A.W, alipowasili Baitul Maqdis alimfunga kamba mnyama wake ajulikanaye kwa jina la Buraqu. Anasema Mtume S.A.W: Nikamfunga mnyama yule pale wanapowafungia Mitume Wanyama wao.

Na miongoni mwake ni: Humtofautisha mtu mwenye Imani ya kweli na yule asiye na Imani ya kweli.

Walipomwambia Bwana Wetu Abu Bakari Swiddiiq R.A: Hivi unazionaje habari za rafiki yako? Yeye anadai kuwa eti alipelekwa Usiku huko Baitul Muqadas? Abu Bakari Swiddiiq Akasema: Je ni yeye ndiye aliyesema hivyo? Wakasema: Ndio. Akasema: ikiwa yeye ndiye aliyesema hivyo basi hakika amesema kweli. Wakasema: Je wewe unamwamini kuwa yeye alipelekwa Baitul Muqadas usiku, na akarejea kabla hapajakucha? Akasema: Ndio. Hakika mimi ninamwamini katika yale yaliyo zaidi ya hayo; Ninamwamini kwa Wahyi wa Mbinguni nyakati za mchana na jioni. Na kwa ajili hiyo, akaitwa Abu Bakari Swiddiiq.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na akusameheni nyinyi.

* * *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola Mlezi wa viumbe vyote na rehma na amani zimfikie Mtume Wetu ambaye ni mwisho wa Mitume wote: Bwana Wetu Muhammad na Jamaa zake na Maswahaba wake wote na wafuasi wake.

Ama baada ya Utangulizi huu:

Ndugu zangu Waislamu,

 Suratul Israa imeizungumzia safari hii ya Mtume Wetu S.A.W, iliyobarikiwa na imezungumzia jinsi ya kuwatendea wema wazazi wawili kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا}

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amempa mama nafasi kubwa zaidi kutokana na kazi yake kubwa pamoja na uvumilivu wake wa kubeba ujauzito, kunyonyesha na kulea. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَوَصَّيْنَا الانسَـانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّه وَهْنًا عَلَى وَهْنٍ}

Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu…

Na Mtu mmoja alipomuuliza Mtume Wetu S.A: Ni nani mwenye haki zaidi kwangu mimi katika Watu katika kumtendea Wema? Mtume akasema: Ni Mama yako. Akauliza yule Mtu: Kisha nani? Mtume akasema: Kisha mama yako. Akauliza tena Mtu: Kisha nani? Mtume akamwambia: Kisha mama yako. Akauliza tena kisha nani? Mtume S.A.W, akasema kisha baba yako.

Na Sheria tukufu imeujaalia wema kwa wazazi wawili kama ni moja ya sababu muhimu sana za kujipatia radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtu mmoja alimwendea Mtume Wetu S.A.W, kwa ajili ya kumwomba idhini ya kwenda kupigana Jihadi. Mtume S.A.W, akamuuliza: Je, mama yako yuko hai? Akasema: ndio. Mtume akamwambia: Rejea nyumbani ukamtendee Wema. Alipotaka kuendelea kumuuliza swali hilo hilo, Mtume S.A.W, akamwambia: Ole wako, ushike mguu wake kwani mguu wake ni Pepo.

Na kumtendea wema mama ni kumkirimu na kumfurahisha. Na Wema huo kwa mama unaendelea baada ya kufariki kwake Dunia, kwa Dua na kumwombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na pia kumtolea sadaka pamoja na kuwatendea wema wale anaowapenda. Anasema Mtume Wetu S.A.W: Hakika Wema ulio na hadhi ya juu zaidi ni Mtoto kuwaunga vipenzi vya Baba yake.

Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu tunakuomba utujaalie msimamo katika Dini yako, na uwalinde wazazi Wetu na Nchi yetu, na Nchi zote .