Habari Muhimu Zilizotufikia
 

Wajibu wetu kwa upande wa Kurani tukufu
3 jamad-Awal 1437H. / 12-2-2016AD

awkaf-

Kwanza: Vipengele

Kurani Tukufu ni miujiza wa kiisilamu wa milele.

Nafasi ya Kurani Tukufu na fadhila zake.

Nafasi za wenye kuitendea Kurani Tukufu hapa duniani na akhera.

Wajibu wa waisilamu kwa upande wa Kurani Tukufu.

  1. kuitukuza na kuisoma na kuzingatia aya zake.
  2. Adabu tuwapo na Kurani Tukufu na kujiweka kitabia za Kurani Tukufu.
  3. kuzifanyia kazi amri zake na makatazo yake.

Pili: dalili ndani ya Kurani Tukufu na hadithi

Dalili ndani ya Kurani Tukufu

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa }Zumar. 23.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur’ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeli uona ukinyenyekea, ukipasuka kwa khofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo mifano tunawapigia watu ili wafikiri }Al hashri. 21.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Na namna hivi tumekufunulia Qur’ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka 53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo mbinguni na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu }Ash shuraa 52-53.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Hakika hii Qur’ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa }Al israa. 9.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda }Al hijri.9.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? }Al qamar. 17.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Na tunateremsha katika Qur’ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara. }Al israa. 82.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli }Al baqara.23.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.} S`aad. 29.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao }Al Isaraa. 88

Dalili ndani ya hadithi

Kutoka kwa Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) alipoulizwa kuhusu tabia za mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “Tabia zake zilikuwa ni kurani.” (Imam Ahmad).

Kutoka kwa Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) kutoka kwa mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “ambae husoma kurani naye anaijua vyema basi huwa na malaika wema, na ambaye huisoma kurani hali ya uzito basi ana malipo mara mbili.” (Imam Abi Daudi)

Kutoka kwa Anas bin Malik (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema; amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie juu yake) “Mwenyezi Mungu ana watu wa aina mbili, wakasema, ni akina nani hao ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Akasema: “hao ni watu wa kurani, watu wa Mwenyezi Mungu na ndio aliowatenga maalumu.” (Ibn Majah)

Kutoka kwa Ibn Masuud (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema; amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu(rehma na amani zimshukie juu yake) “mwenye kusoma herufi moja ndani ya kitabu basi atapatwa kwayo jema, na jema moja ni huzidishwa mfano wake mara kumi, sisemi Alif Laam miim  ni herufi, lakini Alif ni herufi, Laam ni herufi na Miin ni herufi. (Imam Tirmidhy)

Kutoka kwa Ibn Masuud (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema; mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) ameniambia: “Nisomee” akasema: nikamwambia nikusomee na kwako imeteremshwa? Akasema “ hakika mimi ninapenda kuisikia ikisomwa na mwengine. Akasema: nikasoma Annisai mpaka nilipofika: { itakuwaje tutakapouleta kila umma na shahidi, kisha ukaja wewe kama ni shahidi wa hawa} akaniambia inatosha. Nikayaona macho yake yanatokwa na machozi.” (Imam Bukhari na Muslim)

Kutoka kwa Abi Malik Al ashaariy (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: amesema mjumbe (rehma na amani zimshukie juu yake) “… kurani ima ni hoja kwako au dhidi yako… (Imam Muslim)

Na kutoka kwa Abi Mussa Al ashariy (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie juu yake) “mfano wa muumini asomae kuran ni mfano wa mtunda  harufu yake ni nzuri na ladha yake ni nzuri. Na mfano wa muumini ambae hasomi kurani ni mfano wa tende, haina harufu (lakini) ladha yake ni tamu. Na mfano wa mnafiki ambae anasoma kurani ni mfano wa mrehani harufu yake ni nzuri na ladha yake ni chungu. Na mfano wa mnafiki ambae hasomi kurani ni sawa na mfano wa mtango mwitu halina harufu na ladha yake ni chungu.” (Bukhari na Muslim)

Na kutoka kwa Ukubah bin Amir Aljuhaymiy amesema: mtume wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie juu yake) alitujia tulipokuwa tumekaa kivulini akasema: “ hivyo ni nani kati yenu angependa kwenda Kuthan au Al akiyk akachukua ngamia wawili walio wazuri bila ya kupata madhambi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wla kukata ukoo?” wakasema: sote tunataka ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Akasema: “ aendapo mmoja wenu msikitini kila siku akajifunza aya mbili ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu ni bora kwake kuliko ngamia wawili, na akisoma aya tatu (basi bora kwake) kuliko ngamia watatu na mfano wa idadi za aya kwa idadi za ngamia.” (Abi Daudi)

Kutoka kwa  Abi Umamah (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu akisema: “Kurani italetwa siku ya kiyama na watu wake ambao walikuwa wakiitendea, itatangulia sura ya Al baqara na Al imran.” Na mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) akazipigia mfano sitoisahau milele, akasema: mfano wake (hizo sura) ni kama mawingu mawili au vivuli viwili vyeusi kati yao ni mwanga kama kwamba ni makundi ya ndege waliopiga safu zitamuombea shifaa waliokuwa wakizisoma.” (Muslim)

Na kutoka kwa maneno ya wanazuoni (waliotangulia)

Abu Abdulrahman Assalamiy (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) anasema: “tulikuwa tukijifunza aya kumi za kurani na wala hatukuwa tukijifunza aya kumi (nyengize) zijazo isipokuwa baada ya kujifunza halali zake na haramu zake na amri zake na makatazo yake.” (Utunzi wa Abdu Razak)

Tatu: Maudhui

Kurani Tukufu ni mwujiza mkubwa wa kiisilamu kwa nyakati zote, majini na wanadamu walishindwa kuileta kama hiyo. Akasema Mwenyezi Mungu  { Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao }Al Isaraa. 88. bali pia wameshindwa kuleta sura kumi tu mfano wake au sura moja mfano wake, Mwenyezi Mungu amesema {Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.} Hud.13. na akasema Mwenyezi Mungu { Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli }Al baqara.23.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameiteremsha ndani ya moyo wa mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) iwe ni uongofu kwa watu katika njia iliyonyooka, iwaangazie maisha, na kuongoa wasiokuwa na uongofu. Ni katiba ya waislamu kwani kwayo nyoyo huuishwa pia nafsi hufanywa kuwa safi na kwayo tabia huwa njema, Mwenyezi Mungu anasema {1. Alif Lam Mim. 2. Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu 3. Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika tuliyo wapa} Albaqara. 1-3. na Mwenyezi Mungu anasema { Hakika hii Qur’ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa }Al israa. 9. mwenye kushikamana nayo ataokoka na fitina, kwani ni mwanga kwa waumini na ni roho ya uongofu wake. Mwenyezi Mungu anasema {Na namna hivi tumekufunulia Qur’ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka 53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo mbinguni na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu }Ash shuraa 52-53.

Na kutokana na uzuri wake kundi la majini walipoisikia waliiamini na kuitukuza, wakapata uongofu wa njia iliyonyooka, kisha wakaenda kuwaonya wenziwao, na hivi ni kama alivyosimulia Mwenyezi Mungu Mtukufu, {Na wakati tulipo waleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza Qur’ani. Basi walipo ihudhuria walisema: Sikilizeni! Na ilipo kwisha somwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya. 30. Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho teremshwa baada ya Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka. 31. Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na muaminini, Mwenyezi Mungu atakusameheni, na atakukingeni na adhabu chungu. 32. Na wasio mwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hao hawatashinda katika ardhi, wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhaahiri.} Al ahqaf 29-32.

Na iwapo hii ndio ilivyokuwa hali ya majini juu ya Kurani Tukufu basi na malaika ni hivyo hivyo. Kutoka kwa Usayd bin Hudhayr, amesema: alipokuwa yeye akisoma usiku sura albaqara na farasi wake amemfunga pembeni mwake, farasi wake akataharaki naye akanyamaza (kusoma), akaendelea kusoma, farasi wake akataharaki, akanyamaza kusoma naye (farasi) akaacha kutaharaki, kisha akaendelea kusoma nae farasi akataharaki baadae akaondoka zake. Na mwanawe yahya alikuwa karibu naye akaogopa asijwe kufikwa na tatizo na alipocheua (farasi wake) alinyanyua kichwa chake juu kuangalia. Ilipofika asubuhi nikamueleza mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) akasema: Soma ewe ibn Hudhayr, akasema niliogopa ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu asije kumkanyaga yahya kwani alikuwa nae karibu, nikanyanyua kichwa changu na kumuondoa kisha nikanyanyua kichwa juu mbinguni, tahamaki mfano wa kivuli mifano ya taa, nikaondoka ili nisiendelee kutazama, akasema “Unafahamu hicho kilikuwa ni kitu gani?” akasema: “hapana”. Akasema “ hao ni malaika walikaribia kwa sababu ya sauti yako na lau kama ungeliendelea basi watu wangeliwaona bila ya kificho.” (Bukhari). Na namna hii ndio huwa athari ya kurani inaposomwa.

Ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ambae maajabu yake hayapungui, naye amedhamini kuitunza kuepukana na kuharibiwa na kubadilishwa, akasema : { Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda }Al hijri.9.

Asemae kupitia kurani basi amesema kweli, aitendeaye basi hulipwa, afanyae hukumu kupitia kurani basi hufanya uadilifu, na ailinganiaye basi huongozwa katika njia iliyonyooka nae Mwenyezi Mungu ameifanya kuwa ni tiba na rehema akasema: { Na tunateremsha katika Qur’ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara. }Al israa. 82.

Kutoka kwa Abdillah (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) kutoka kwa mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “hakika kurani hii ni karamu ya Mwenyezi Mungu basi ipokeeni karamu hii kadiri muwezavyo, hakika kurani hii ni kamba ya Mwenyezi Mungu, na nuru iliyo wazi na matibabu yenye manufaa na ngao kwa wanaoshikamana nayo, uokovu kwa waifuatayo, haipotoshi na wala haiendi kombo na maajabu yake hayaishi na wala haina majibizano. Isomeni kwani Mwenyezi Mungu hukulipeni kwa kuisoma kwake kwa kila herufi thawabu kumi kwani mimi sisemi Ali Laam Miin ni herufi lakini Alif ni herufi Laam ni herufi na Miim ni herufi. (Alhakim)

Mwenyezi Mungu ameinyanyua cheo na kuisifu kwa sifa njema na kuitaja kwa majina mazuri sana ili watu waelewe nafasi na cheo chake, Mwenyezi Mungu akaisifia kwa kusema { Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari} Hud. 1. na aliposema { na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu. 42. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.} Fusilat41-42. na sifa nyengineze zenye kujuulisha cheo na nafasi yake iliyotukuka.

Na mtume wetu (rehma na amani zimshukie juu yake) ametueleza fadhila nyingi sana juu ya Kurani Tukufu ambazo manufaa yake humrudia yeye mwenyewe mwanadamu hapa duniani na kesho akhera, na katika fadhila hizo ni:-

Ubora kwa mwenye kuisoma: Hadithi ya Othmani Bin Affan (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) kutoka kwa mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “mbora wenu ni mwenye kujifundisha kurani na kuifundisha” (Bukhari?)

Kupandishwa cheo: imepokewa hadithi kutoka kwa Amru (Mwenyezi Mungu awawie radhi) amesema, amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie juu yake) “itasemwa kuambiwa msomaji wa kurani: soma na panda cheo, na soma kama ulivyokuwa ukiisoma duniani, kwani cheo chao ni mwisho wa aya utakayoisoma) (Abi Daudi)

Kumuombea msomaji: imepokewa hadithi kutoka kwa Umama Albahiliy (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie juu yake) akisema: “ someni kurani kani hiyo itakuja siku ya kiyama kama ni mwombezi kwa wasomaji wake” (Muslim)

Malipo makubwa kwa msomaji wake: imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn Mas uud (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie juu yake)  “Mwenye kusoma herufi moja ndani ya kitabu basi atapatwa kwayo jema, na jema moja ni huzidishwa mfano wake mara kumi, sisemi Alif Laam miim  ni herufi, lakini Alif ni herufi, Laam ni herufi na Miin ni herufi.” (Imam Tirmidhy)

Kuhifadhiwa nyumba zisomwazo kurani:  imepokewa na Abi Hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) kwamba mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “ musizifanye nyumba zenu makaburi, hakika ya shetani hukimbia nyumba ambayo husomwa ndani yake sura ya Albaqara.” (Muslim) na fadhila nyenginezo ambazo hazimaliziki. Kwa mfano hadithi ya Ibn Siyriyn, amesema: “nyumba ambayo husomwa ndani yake kurani malaika huwa wanahudhuria na mashetani hutoka, na wasomi wake huombewa na kheri zake huzidi. Na nyumba ambayo kurani haisomwi, huhudhuria mashetani na malaika hutoka na huwapo katika simanzi waktu wake na kheri zake huwa ni chache.” (Ibn Abi Shaybah)

Na tukizingatia hali za masahaba wakarimu (Mwenyezi Mungu awawie radhi)juu ya kurani tukufu tutaona kuwa wao hawakutosheka kuisoma tu na kuisikiliza, lakini waliisoma na kuizingatia nyonyo na nafsi zao zikashikamana nayo, wakawa wanaitekeleza kimaneno na kimatendo na kufuata amri zake na kujiepusha na makatazo yeke. Kwa ajili hiyo wakafikia vyeo vikubwa sana walivyofikia kwa sababu ya kuitikia wito wa Kurani Tukufu. Sayidna Omar aliihifadhi sura ya Albaqara kwa muda wa miaka minane si kwa sababu ya uzito wa kuhifadhi isipokuwa alikuwa na pupa ya kupata elimu na kuitendea elimu hiyo. Abu Abdu rahman As salamiy (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) anasema:   “tulikuwa tunapojifunza aya kumi ndani ya Kurani Tukufu huwa hatujifunzi aya kumi nyengine zijazo mpaka (tunahakikisha) tumejifundisha halali yake na haramu na amri zake na makatazo yake” (Abdu Razzak)

Na kwa kuwa masahaba (Mwenyezi Mungu awawie radhi) walikuwa wakijielimisha na kisha kuitendea kwa ajili hiyo wakawa wako mbele katika kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujiepusha na makatazo yake. Na wakati zilipoteremshwa aya za makatazo ya kunywa ulevi, muitaji akaita: “ Tambueni kuwa ulevi umeharamishwa”, basi wote wakaitikia wito wa kurani. Aliyekuwa na ulevi mkononi basi akaurembea, na aliyekuwa ulevu imo kinywani akaucheua, na aliyekuwa na ulevi kwenye chombo akaumwaga hii yote ni kwa ajili ya kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu, – na mpaka njia za mji wa Madina zilijaa pombe- wakawa wanasema “tumeacha ewe Mola wetu”. Na kwa namna hiyo ilipoteremka aya { Kabisa hamtafikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua} Al imran 92. Sayidna Abu Dahdah alisimama kwenye bustani aipendayo zaidi akaitoa sadaka. Kwa hivyo, masahaba (Mwenyezi Mungu awawie radhi) waliweza kuhifahi kitabu cha Mwenyezi Mungu kwani kao hakikua kama kitabu cha kawaida, lakini ni mwongozo wa kimalezi, kimaadili na kiimani iliyodhihiri katika maisha yao ya kila siku na kwa wengine.

Kwa ajili hiyo cheo ambacho Mwenyezi Mungu amewapa wasomao Kurani Tukufu na kuitendea kazi ni kikubwa mno. Imepokea kutoka kwa Anas bin Malik (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu ““Mwenyezi Mungu ana watu wa aina mbili, wakasema, ni akina nani hao ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Akasema: “hao ni watu wa kurani, watu wa Mwenyezi Mungu na ndio aliowatenga maalumu.” (Ibn Majah). Asomae Kurani Tukufu amenasibishwa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni cheo kikubwa kilichoje!

Ama wajibu wetu kuhusu kurani inakusanya:-

* Kujifundisha na kuifundisha, na kuendelea kuisoma na kuifundisha, kwani walio bora ni wale wenye kujifundisha na kuifundisha, imepokewa katika hadithi (mbora wenu ni yule ajifundishae kurani kisha kuifundisha. Na mtume wetu (rehma na amani zimshukie juu yake) ametuamrisha kuisoma na kuishikilia akasema: “shikamaneni na kurani ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu ipo mikononi mwake ni rahisi sana kuponyoka kuliko ngamia aliye katika kamba yake.” (Bukhari)

Kurani Tukufu ni chanzo madhubuti chenye kutengeneza nafsi ya mwisilamu, kupitia Kurani Tukufu hupata mafunzo na tabia njema. Hivyo basi, juu ya muisilamu awe na pupa katika kuisoma vizuri, na jambo hili si gumu, kwani tunakutia watu huwa wanajifunza lugha za kigeni, na hutumia juhudi za namna tafauti ili wawe na maarifa mengi kwa ajili ya kupata kipato kingi. Itakuwaje basi kuzembea katika kujifunza maneno ya Mwenyezi Mungu mtukufu iwe ndio tabu? Imepokewa kutoka kwa Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) kutoka kwa mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “ambae husoma kurani naye anaijua vyema basi huwa na malaika wema, na ambaye huisoma kurani hali ya uzito basi ana malipo mara mbili.” (Imam Abi Daudi) na Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuahidi kuwa ametufanyia kuwa ni chepesi kwa kukisoma na kwa kuabudia akasma { Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? } Alqamar;17.

Kuzingatia aya zake kama kwamba bdio zinashuka kwa msomaji wake, kwani katika wajibu wetu juu ya Kurani Tukufu isiwe ni kuisoma tu lakini hakuna budi kuizingatia ili tupate ladha yake na kuihisi utukufu wake, Mwenyezi Mungu anasema { Je! Hawaizingatii hii Qur’ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?}Muhhamad;24. na akasema pia, { Hebu hawaizingatii hii Qur’ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi} Anisaa;82.

Kwa wasomi wa Kurani Tukufu wanaopata malipo makubwa sana ni wale waisomao kwa ndimi zao na kuzingatia nyoyoni mwao na akilini mwao, Mwenyezi Mungu anasema, { Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili } Saad;29. na Mwenyezi Mungu amemsifu asomaye aya zake kwa kuzingatia zikawa zinamzidishia imani akasema, { Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi }Al anfaal;2. Ibn Abbas amesema: “Mwenyezi Mungu amechukua dhamana kwa aisomae Kurani Tukufu kuwa hatapotea hapa duniani na wala hatokuwa na tabu kesho akhera, na dalili ya hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu, {basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika 124. Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu 125. Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona? 126. (Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa } Taha;123-126.

Na mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) ametupigia mfano kwa mwenye kuathirika na Kurani Tukufu na kutekeleza kama aya zake zisemavyo. Siku moja alisema kumwambia Abdullah bin Masuud (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake): “Kutoka kwa Ibn Masuud (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema; mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) ameniambia: “Nisomee” akasema: nikamwambia nikusomee na kwako imeteremshwa? Akasema “ hakika mimi ninapenda kuisikia ikisomwa na mwengine. Akasema: nikasoma Annisai mpaka nilipofika: {itakuwaje tutakapouleta kila umma na shahidi, kisha ukaja wewe kama ni shahidi wa hawa} akaniambia inatosha. Nikayaona macho yake yanatokwa na machozi.” (Imam Bukhari na Muslim). Fahari ya muumini ni kuenda sambamba na neno la Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenyezi Mungu anasema {Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa}Azzumar;23.

Adabu (heshima) za kuwa na Kurani Tukufu na kujipamba kwa tabia zake, miongoni mwa wajibu wa msomi wa Kurani Tukufu ni kuwa na heshima na kujipamba kwa mwenendo wa Kurani Tukufu, ashikamane na mafunzo yake. Kwani kupitia tabia za kurani mwanadamu anajikinga na ufuataji wa matakwa yake na matamanio yake na nafsi yake huwa madhubuti katika maadili mema, Mwenyezi Mungu anasema, { Hakika hii Qur’ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa }Al israa;9. na kigezo chetu juu ya hili ni bwana mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) kwani alikuwa kama kurani ikitembea juu ya mgongo wa ardhi, alijipamba kitabia kama kurani itakavyo, akiridhia kile ambacho Kurani Tukufu imeridhia,na kuchukia kile kilichochukiwa na Kurani Tukufu. Bibi Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) aliulizwa kuhusu tabia za mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) akasema: “tabia zake ni kurani.” (Ahmad)

* kufuata maamrisho yake na makatazo yake, wajibu wetu juu ya Kurani Tukufu hautakiwi uwe ni vifuani au hata kuizingatia pekee lakini itabidi kufuata maamrisho yake na makatazo yake. Ili tabia na matendo yetu yaonekane kama alivyokuwa mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) na masahaba wake. Hivyo, wajibu wa muisilamu afuate amri za kurani na kuacha makatazo yake kwani  mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) anasema: “kurani ima ni hoja kwako au dhidi yako.” (Muslim) Itakuwa ni hoja dhidi yako pindi iwapo haitofika masikioni mwako na wala haitoathiri kitu katika mwenendo wa maisha yako na huenda msomaji wake ikawa inamlaani.

* Na miongoni mwa wajibu wetu juu ya Kurani Tukufu ni kupambana na wanaoipotosha na kuifasiri visivyo na kuizungumzia kisiasa au kiitikadi (sizo) ili kupata manufaa na chumo. Kurani Tukufu inabidi ielezwe kimaneno na kimaana kwa wasomi wake wa umma wenye kuamninika na waliobobea katika fani hiyo, wawafundishe watu mafunzo sahihi na itikadi ndiyo ya kiisilamu ama kwa wale wasioijua hawatakuwa na cha kufanya zaidi ya masilahi yao na matamanio yao.

* Na ulimwengu wetu wa sasa unahitajia zaidi uongofu wa Kurani Tukufu, matatizo yaliyopo sasa ni matatizo ya kimaadili na hakuna kitabu kilicholingania maadili kwa watu wote mfano wa Kurani Tukufu. Na iwapo kosa la waislamu kwa wakati huu kujiweka mbali na mwenendo wa Kurani Tukufu sasa itawalazimu wairudie na kufuata mifano ya kivitendo ya Kurani Tukufu na kwa aliyeteremshiwa hii kurani (mtume Muhammad rehma na amani zimshukie juu yake). Kwani yeye ndiye aliyesifiwa na Mola wake kuwa ni mwenye tabia njema kabisa kwakuwa tu ameifuata kurani kimarefu na mapana. Alikuwa ni kiumbe mwenye tabia nzuri kwa kule kuifuata katika nyanya zote, Mwenyezi Mungu anasema {Hakika wewe ni mwenye tabia nzuri} Alqalam,4. na kama ilivyoelezwa katika hadithi ya Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) akasema “tabia zake ni kurani.”

* Nasi hatutoacha kuelezea Kurani Tukufu ili iwe ni mwongozo mwema utakaotukinga siku ambayo hatutokuwa na mkingaji wala muokoaji, imepokewa kutoka kwa Abi Umamah (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: “nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu akisema: “Kurani italetwa siku ya kiyama na watu wake ambao walikuwa wakiitendea, itatangulia sura ya Al baqara na Al imran.” Na mtume (rehma na amani zimshukie juu yake) akazipigia mfano sitoisahau milele, akasema: mfano wake (hizo sura) ni kama mawingu mawili au vivuli viwili vyeusi kati yao ni mwanga kama kwamba ni makundi ya ndege waliopiga safu zitamuombea shifaa waliokuwa wakizisoma.” (Muslim)

Waisilamu wakiendelea kuisoma, kuzingatia maana yake na kuitendea pia kujifunza na kuifundisha watakuwa na manufaa makubwa sana, kwani rehema na uadilifu utaenea, nyoyo zitakuwa njema kheri zitakuwa nyingi na shari na maafa yatatoweka.