Fadhila za masahaba (radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie)
na mifano ya historia yao njema
16 Jamad Akhar 1437H. sawa na 25/3/2016

awkaf-

Kwanza: vipengele

 1. Nafasi za masahaba na kupanda vyeo vyao.
 2. Fadhila za masahaba ndani ya Qurani Tukufu.
 3. Kuwapenda masahaba ni katika imani.
 4. Mahimizo ya kuwaiga masahaba watukufu.
 5. Makatazo ya kuwatusi au kuwasema vibaya.
 6. Mifano katika historia yao.

Pili: dalili

Ndani ya Qurani Tukufu

 1. Mwenyezi Mungu anasema { Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wana hurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao katika nyuso zao,  kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katikaTaurati. Na mfano wao katika Injili ni  kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.}(Alfathi. 29)
 2. Mwenyezi Mungu anasema { Na wale walio tangulia, wa kwanza, katikaWahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema,Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake,wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.}(Atawba. 100).
 3. Mwenyezi Mungu anasema {Na wa mbele watakuwa mbele. 11. Hao ndio watakao karibishwa 12. Katika Bustani zenye neema. 14. Na wachache  katika  wa mwisho. 13. Fungu kubwa katika wa mwanzo, }(alwaqia. 10-14)
 4. Mwenyezi Mungu anasema { Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye – hao ndio wenye kufanikiwa.}(Alaaraf. 157).
 5. Mwenyezi Mungu anasema {Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari waliomfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu}(Atawaba.117)
 6. Mwenyezi Mungu anasema {Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa.89. Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa.}(Atawaba.88-89)
 7. Mwenyezi Mungu anasema { Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa ushindi wa karibu.}(Alfathi.18)
 8. Mwenyezi Mungu anasema {Wapewe mafakiri Wahajiri walio tolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli. 9. Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao,wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake,basi hao ndio wenye kufanikiwa.} (Alhashri.8-9)

Ndani ya hadithi

 1. Kutoka kwa Abdala bin Masud (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) kutoka kwa Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema: “bora ya watu ni waliopo katika wakati wangu, kisha wanaowafuatia, kisha wanaowafuatia, kisha watakuja watu shahada ya mmoja wao itatanguliwa na kiapo na kiapo chake kwa shahada yake.” (Muslim na Bukhari).
 2. Kutoka kwa Abi hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema: amaesma Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie): “ Msiwatusi masahaba zangu, msiwatusi masahaba zangu, naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake lau kama mmoja wenu angelitoa dhahabu mfano wa jabali la Uhud basi asingelifikia kwa utoaji huo wala nusu yake.” (Bukhari na Muslim).
 3. Mtume (rehma na amani zimshukie) anasema: “Tahadharini, tahadharini kuhusu masahaba wangu. Tahadharini, tahadharini kuhusu masahaba wangu. Msiwavunjie heshima baada yangu, mwenye kuwapenda basi kwa mapenzi yangu nitampenda, na mwenye kuwachukia basi kwa chuki yangu nitamchukia, na mwenye kuwakera basi kwa hakika amenikera mimi, na anikeraye hakika huwa amemkera Mwenyezi Mungu, na amkeraye Mwenyezi Mungu pana wasiwasi wa kuchukuliwa.” (Ahmad).
 4. Kutoka kwa Abi Hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema: amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie) nani kaamka hali ya kuwa amefunga? Abu Bakar akasema: “Mimi”. Akasema: “Ni nani kati yenu aliyeshindikiza jeneza?” Abu Bakar akasema: “Mimi” akasema: “Ni nani kati yenu aliyelisha masikini?” Abu Bakar akasema: “Mimi” akasema: “Ni nani kati yenu aliyetembelea mgonjwa?” Abu Bakar akasema: “ Mimi” Mtume (rehma na amani zimshukie) akasema mambo haya yakikusanyika kwa mtu basi ataingia peponi.” (Muslim).

Tatu: maudhui

Mwenyezi Mungu Mtukufu amemchagulia Mtume wake (rehma na amani zimshukie) watu wasafi, masahaba walio wema, waliomuamni na kumuunga mkono na kumnusuru, waliosoma na kupasi kutoka katika chuo cha Nabii Muhammad (rehma na amani zimshukie), waliolelewa katika mikono yake, waliokunywa kinywaji cha chemuchemu safi ambayo inatoa maji ya imani, wakawa watu wenye imani ya kweli, na wenye elimu kubwa, na ufahamu wa kina, na matendo mema zaidi. Waliibeba bendera ya dini katika ulimwengu wote, hawakuwa wakiogopa lawama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kwa ajili hiyo, wakafanikiwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Naye akawasifu ndani ya Qurani Tukufu kwa kusema { Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema,Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhikanaye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake,wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.}(Atawbah. 100). Hao ndio masahaba wa Mtume (rehma na amani zimshukie) ambao Mwenyezi Mungu amewateua kwa Mtume wake wa mwisho.

   Kizazi kilichoweza kubadilisha mwenendo wa maisha, waliibeba nuru aliyokuja nayo bwana wetu, Mtume Muhammad (rehma na amani zimshukie) kwa ulimwengu wote. Na kadiri tutakavyojaribu kuwafukuzia basi hatutaweza, na inatosha kuelewa kuwa lau kama tutatoa sadaka ya dhahabu kila siku mfano wa jabali la Uhudi hatofikia mmoja wenu thamani ya kile walichokitoa masahaba wala nusu yake. Hivi ni kama alivyoashiria Mtume (rehma na amani zimshukie) aliposema… “Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake lau kama mmoja wenu angelitoa dhahabu mfano wa jabali la Uhud basi asingelifikia kwa utoaji huo wala nusu yake.” (bukhari na Muslim). Na hii ni kwa sababu walihimili matatizo ya kueneza hii dini na kufikwa yaliyowafika, wakajitolea kinafsi zao, roho zao na mali zao katika njia ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na kumnusuru Mtume wake (rehma na amani zimshukie), akasema Mwenyezi Mungu { Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu – wanauwa na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyo jilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur’ani. Na nani atimizae ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa,}(Atawbah.111).

Na iwapo ni katika haki zetu kwa Mtume (rehma na amani zimshukie) kuisoma historia yake na mwenendo wake na kufuata uongofu wake na kutenda kwa mujibu wa sheria yake, basi pia katika haki zetu kwa upande wa masahaba ni kuelewa ubora wao na nafasi zao na kusoma historia zao ili tuweze kufanana nao katika kuwa na maadili mazuri, katika kumtii na kumuabudu Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu wote, na tuchukue mazingatio na mawaidha katika maish yao. Kwani wao wamechaguliwa na Mwenyezi Mungu ili wawe pamoja nae (rehma na amani zimshukie) na kueneza ujumbe baada ya kuondoka kwake, kwani wao ni watu bora katika umma huu kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewasifu kwa sifa za ukamilifu na kuwasafisha, hakuna katika watu aliyeweza kuelewa mfano wa uchaji Mungu kama walivyokuwa hawa wakimcha Mungu . Mwenyezi Mungu amewasifu na akaweka wazi ni kipi alichowaandalia katika malipo makubwa, akasema { Na wa mbele watakuwa mbele. 11. Hao ndio watakao karibishwa 12. Katika Bustani zenye neema. 14. Na wachache katika wa mwisho. 13. Fungu kubwa katika wa mwanzo,}(Alwaqiah. 10-14).

    Na kwa kuweka wazi nafasi zao na kupanda kwa cheo chao Mwenyezi Mungu akawapa sifa miongoni mwa sifa zake ndani ya Qurani Tukufu, si hivyo tu, bali pia wamesifiwa katika Taurati na Injili akasema { Muhammad ni  Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wana hurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katikaTaurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa} (Alfathi.29). Mwenyezi Mungu akawasifu kuwa wao ni wenye nguvu mbele ya makafiri pasi na kudhulumu na weney kuoneana hurumu kati yao, wakimuabudu Mwenyezi Mungu mmoja bila ya kumshirikisha na chochote, wakirukuu na kusujudu, hawatafuti fadhila na radhi isipokuwa zitokazo kwa Mwenyezi Mungu, na ibada imewaathiri mpaka ikadhihiri alama zake katika viungo vyao, ukimuona mmoja wapo basi utaelewa tu ni katika wale wamuogopao Mwenyezi Mungu na kumcha. Hivyo, masahaba (radhi ziwe juu yao) ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja wake, akasema { Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu.}(Alfathi 18) .

Na tukiusoma mwenendo wa Mtume (rehma na amani zimshukie) tutaona kuwa umejaa masimulizi yenye kuonyesha ubora wao na kukuwa kwa nafasi zao, kwa mfano, kukiri kwake Mtume (rehma na amani zimshukie) kuwa wao ni katika watu wa karne (wakati) bora na bora ya umma. Kutoka kwa  Abdala bin Masud (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) kutoka kwa Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema: “bora ya watu ni waliopo katika wakati wangu, kisha wanaowafuatia, kisha wanaowafuatia, kisha watakuja watu shahada ya mmoja wao itatanguliwa na kiapo na kiapo chake kwa shahada yake.” (Muslim na Bukhari). Na wamekuwa watu bora kwa kuwa walimuamini Mtume (rehma na amani zimshukie) wakati watu wengine walipomkanusha, na kumsadiki wakati wengine walipomuona muongo, na kumnusuru kwa mali zao na nafsi zao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu . imepokewa katika kitabu cha imam Ahmad, kutoka kwa Abdalla bin Masud (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema: “Mwenyezi Mungu ameangalia katika nyoyo za waja akaona moyo wa Muhammad (rehma na amani zimshukie) ni bora kati ya nyoyo za waja, akamchagua yeye, na akampa ujumbe wake, kisha akaangalia nyoyo za waja baada ya moyo wa Muhammad akaona nyoyo za masahaba ni nyoyo bora kati ya nyoyo za waja, akawafanya kuwa ni mawaziri wa Mtume wake (rehma na amani zimshukie) wenye kuipigania dini yake, na kile waonacho waisilamu ni jema basi na kwa Mwenyezi Mungu pia ni jema, na walionalo kuwa si jema basi kwa Mwenyezi Mungu pia si jema.”

   Pia katika ubora wa masahaba ni kama alivyosema Mtume (rehma na amani zimshukie) kuwa wao ni amana ya umma, Mtume (rehma na amani zimshukie) anasema: “nyota ni amana kwa mbingu, na nyota ziondokokapo basi mbigu huleta kile kilichoahidiwa, na mimi ni amana kwa masahaba zangu nikiondoka basi masahaba zangu wanaleta kile walichoahidiwa, na masahaba zangu ni amana kwa umma wangu wakiondoka basi umma wangu wataleta kile walichoahidiwa.” (Muslim) . Ikawa kuwepo kwa masahaba (radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie) ni amana kwa umma ya kutokuwepo kwa uzushi, lakini pia kutokana na Baraka zao zimeenea na kufika hadi katika kizazi cha pili baada yao. Kutoka kwa Saad Alkhudriy (rehma na amani zimshukie) kwamba Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema: “watakuja watu watawapigana vita na kundi jengine, watasema: “yupo katika nyie aliyekuwa na Mtume (rehma na amani zimshukie)?” watasema: “ ndio” basi watafunguliwa. Kisha watakuja watu watapigana vita na kundi jengine, itasemwa ““yupo katika nyie  aliyekuwa na waliokuwa na Mtume  (rehma na amani zimshukie)? Watasema: “ndio” watafunguliwa. Kisha watakuja watu watapigana vita na kundi jengine, itasemwa, “yupo katika nyie aliyekuwa na waliokuwa pamoja na waliokuwa na Mtume  (rehma na amani zimshukie)? Watasema “ndio” watafunguliwa. (Bukhari naMuslim).

Pia Mwenyezi Mungu amewashuhudia kuwa ni watu waliokuwa na moyo wa kujitolea, ukarimu na juhudi za kutafuta radhi na mafanikio kwa Mwenyezi Mungu. Naye akawaandalia kutokana na hili pepo ya milele yenye neema. Akasema {Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa 89. Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa. }(Atawbah88-89). Umar (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) anasema: “siku moja Mtume (rehma na amani zimshukie) alituamrisha tutoe sadaka, ikawa ninazo mali, nikasema: “ leo nitamshinda Abu Bakar nikishindana naye, nikaja na nusu ya mali yangu. Mtume (rehma na amani zimshukie) akasema: “ watu wako umewabakishia kitu gani? Nikasema: “mfano wake. Akasema: “akaja Abu Bakar (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) na kila alichonacho, Mtume akamwambia. “watu wako umewabakishia kitu gani? Akasema: “nimeaachilia Mwenyezi Mungu na Mtume wake, nikasema (Umar) siwezi kushindana na wewe kwa kitu chochote milele..” (Tirmidhi).

Na iwapo hii ndio nafasi ya masahaba wa Mtume (rehma na amani zimshukie) basi kuwapenda kwao (radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie ) na kukiri ubora wao kuliko wengine ni katika imani ya lazima juu ya kila muisilamu. Kwani ni ishara ya kumpenda Mtume (rehma na amani zimshukie) ambaye aliwapenda na kuwachagua kuwa ni masahaba wake. Muumini hupenda kila apendacho Mtume (rehma na amani zimshukie) wakiwemo masahaba zake. Imepokewa na Abdalla bin Mugh-qal (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema: amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie) “tahadharini, tahadharini kuhusu masahaba wangu. tahadharini, tahadharini kuhusu masahaba wangu. Msiwavunjie heshima baada yangu, mwenye kuwapenda basi kwa mapenzi yangu nitampenda, na mwenye kuwachukia basi kwa chuki yangu nitamchukia, na mwenye kuwakera basi kwa hakika amenikera mimi, na anikeraye hakika huwa amemkera Mwenyezi Mungu, na amkeraye Mwenyezi Mungu pana wasiwasi wa kuchukuliwa.” (Ahmad). Na katika kitabu cha imam bukhari na muslim kutoka kwa Bara`a ibn A`zib, kutoka kwa Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema kuhusu Maanswar; hawapendi hao (Maanswar) isipokuwa ni muumini, na wala hawachukii isipokuwa ni mnafiki, atakaewapenda basi atapendwa na Mwenyezi Mungu, na mwenye kuwachukia atachukiwa na Mwenyezi Mungu. Kuwapenda ni dalili ya imani na ni kumtii Mwenyezi Mungu, na kuwachukia ni unafiki na uasi. Imepokewa na Anas bin malik (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) kutoka kwa Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema: “dalili ya imani ni kuwapenda Maanswari, na dalili ya unafiki ni kuwachukia Maanswari.” (Bukhari).

Uisilamu umeharamisha kuwasema vibaya masahaba (radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie) kwani aliowachagua ili wawe na Mtume –naye ni Mwenyezi Mungu – amewasifu na kuwaridhia. Na kama alivyotukataza Mtume (rehma na amani zimshukie) juu ya kuwatusi. Kutoka kwa Abi Hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie), hakika ya Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema: Musiwatusi masahaba wangu, musiwatusi masahaba wangu naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake lau kama mmoja wenu angelitoa dhahabu mfano wa jabali la Uhud basi asingelifikia kwa utoaji huo wala nusu yake.” (Muslim). Na kutoka kwa Abdalla bin Umar (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema. Musiwatukane masahaba wa Mtume Muhammad (rehma na amani zimshukie), kwani kisimamo cha ibada ya mmoja wao cha saa moja ni bora kuliko ibada ya miaka arobaini ya mmoja wenu.” (ubora wa masahaba, Imam Ahmad). Kwa ajili hiyo ni wajibu wetu kuwapa heshima na kuelewa vyeo vyao.

Na mwenye kuangalia maisha ya masahaba (radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie) ataona kiwango kikubwa sana cha imani waliyokuwa nayo, na kufuata amri za Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehma na amani zimshukie), atakutia kuwa kuna ufasiri wa kiuhakika wa utendaji matendo mazuri, walikuwa ni viongozi wema walioonyesha mfano wa utoaji, elimu, utendaji, kujitolea muhanga kwa ajili ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, mpaka wakateremshiwa aya { Wapewe mafakiri Wahajiri walio tolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli.}(Alhashri.8) .

Na mfano wa wazi kabisa ni, sahaba Ali bin Abi Twalib (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) alipojitolea kulala katika kitanda cha Mtume (rehma na amani zimshukie) usiku wa kuhama kwa Mtume ili ajitoe muhanga kwa nafsi yake na roho yake hali ya kuelewa kuwa washirikina wanamsaka kwa mapanga kwa ajili ya kumuua.

Pia sahaba Suhayb Ruumi alijitolea muhanga wa mali zake kwa ajili ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, na kumnusuru Mtume (rehma na amani zimshukie) wakati alipotaka kuhamia Madina. Makafiri wa kikuraish wakamwambia: “ulikuja kwetu huna kitu, ukaupata utajiri kutoka kwetu, na kufikia ulipofikia kisha unataka kutoka wewe na nafsi yako, hiyo haiwezekani. Akawaambia: “Mnaonaje iwapo nitakupeni mali zangu mutaniachia? Wakasema: “ ndio” akasema: “ninakuwekeni mashahidi kuwa mali yangu nimewaachilia nyinyi.” Ikamfika hilo Mtume (rehma na amani zimshukie) akasema: Suhayb amepata faida, suhayb amepata faida.” (Ibn Haban).

Mfano mwengine ni Abu bakar (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) anatupa mfano mzuri wa maadili mema, na sifa nzuri mpaka akawa ni kigezo cha kila jema. Na Mtume akamshuhudia kwa hili kuwa ni katika watu wa peponi. Kutoka kwa Abi Hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema: amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukie) nani kaamka hali ya kuwa amefunga? Abu Bakar akasema: “mimi”. Akasema: “ni nani kati yenu aliyeshindikiza jeneza?” Abu Bakar akasema: “mimi” akasema: “ni nani kati yenu aliyelisha masikini?” Abu Bakar akasema: “mimi” akasema: “ni nani kati yenu aliyetembelea mgonjwa?” Abu Bakar akasema: “ mimi” Mtume (rehma na amani zimshukie) akasema mambo haya yakikusanyika kwa mtu basi ataingia peponi.” (Muslim).

Nae sahaba Umar (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) siku moja alikuwa akitembea usiku, tahamaki kuna mwanamke ana watoto na chungu kipo motoni na watoto wamejikunyata. Umar akasema: Amani juu yenu enyi watu wa mwangani, alichukia kusema enyi watu wa motoni, mwanamke  akasema: “nawe amani iwe juu yako”. Akasema (Umar) je nikaribie? Akasema (mwanamke) ikiwa kwa heri karibia na kama kwa shri usikaribie, akakaribia, akasema: “ muna nini? Akajibu: “usiku umekuwamfupi kwetu pamoja na baridi. Akasema: “na hawa watoto wana nini mbona wamejikunyata? Akasema: ‘ni njaa. Akasema: “ndani ya chungu hiki muna kitu gani?” Akasema: “cha kuwadanganyia mpaka walale, na Mwenyezi Mungu yupo pamoja nasi juu ya Umar. Akasema “Mungu akurehemu, munamjuaje Umar?” akasema: “Umar unatuongoza kisha anatusahau.” Zaid – mpokezi wa hadithi- anasema: “ akanikabili kisha akaniambia tuondoke, tukaondoka huku tunakazana mpaka tukafika nyumba ya unga (nyumba ya hazina), akatoa kiwango cha unga na kopo la mafuta, akasema: “ nibebeshe: “ nikamwambia: “ mimi nitakubebea: “je nawe utanibebe mzigo wa madhambi yangu siku ya kiyama? Nikambebesha, akaondoka nami nikaondoka nae hali yakukazana. Tulipofika kwa Yule mwanamke tukautua akampa unga, akawa anamwambia tupa juu yangu na ninakutetemeka mimi mwenywe,  akawa anapuliza chungu. Akasema: “ nipe kitu chochote (cha kupakulia) akapewa na kupakuwa ndani yake huku akisema: “walishe na mimi nitawashikia, akawa katika hali hiyo mpaka wakashiba, na baadae wakamuacha akaondoka nami (Zaid) nikaondoka nae. Naye Yule mwanamke akawa nasema Mungu akulipe kila la kheri, jambo hili ulilolifanya ni jema kuliko afanyavyo kiongozi wa waumini: ‘nikamwambia “ sema mema pindi kiongozi wa waumini atakapokujia, na nisimulie kuhusu yeye akipenda Mungu, kisha akajiweka upande na baadae akamsogelea na kukaa  kitako ,na kumpokea tukamwambia: “ tuna jambo jengine lisilo hili na akawa hatuzungumzishi mpaka nilipowaona watoto wamelala na kutulizana, akasema : amani, hakika njaa imewafanya wasilale na kuwafanya walie na nilipendelea kuwa nisiondoke mpaka nione niliyoyaona. (ubora wa masahaba, imamu Ahmad).

Na hata masahaba wa kike (radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie) nao wana fadhila na misimamo ya kujitolea muhanga kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano: –

Msimamo wa Mama wa waumini Khadija (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) alivyokuwa na msimamo wa kueneza dini ya Mwenyezi  Mungu pale aliposimama wima na mumewe na kujitolea muhanga kwa mali zake na nafsi yake, na kumtuliza kutokana na hofu aliyokuwa nayo (rehma na amani zimshukie) wakati alipoteremshiwa wahyi katika jabali la Hiraa,na kumwambia kwa kujiamini, na wala kutetereka: “ hakika Mwenyezi Mungu hakuhuzunishi katu, wewe utaunga ukoo, na kubeba yote na kumpata asiyekuwepo, na kumtuliza mgeni na kusaidia kwenye haki. (Bukhari) akawa ni katika wake wema sana mwenye kujua wajibu wake na haki. Vilevile Mtume (rehma na amani zimshukie) alikuwa akimtaja sana na kumsifia, kutoka kwa Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu) amesema: Mtume (rehma na amani zimshukie) alikuwa akitajwa Khadija huwa anamsifia,, akasema: “ nikawa na wivu siku moja, nikasma: “mbona unamtaja sana huyu mwenye uso mwekundu  yaani khadija ,na Mwenyezi Mungu amekubadilishia mbora kuliko yeye. Mtume akasema (rehma na amani zimshukie) Mwenyezi Mungu hajanibadilishia mbora zaidi yake, kwani yeye aliniamni wakati watu wakinipinga, na kuniona ni mkweli wakati watu wakiniona ni mwongo, na kuniliwaza kwa mali zake wakati watu walinitenga, na Mwenyezi Mungu amenipatia kutoka kwake watoto wakati sikupata watoto kutoka kwa wanawake wengine.” (Ahmad)

Na mfano mwengine mwema na wa kuigwa wa masahaba wa kike (radhi za Mwenyezi Mungu  ziwashukie) ni Mama Umarah nasiybah bint Ka`ab Al answari ambaye Mtume (rehma na amani zimshukie ) alisema kuhusu yeye: “ mimi katika vita ya Uhud sikuwa nikigeuka upande wa kulia wala wa kushoto isipokuwa nilikuwa nikimuona Umu Umarah akipigana pamoja nami.”  Mpaka  mtu akitaka kumuua Mtume (rehma na amani zimshukie) anamuona Umu Umrah yupo mbele yake, na hupigana naye kwa panga mpaka bega lake likajawa na damu kutokana na mapigo ya mapanga. Mtume akamwambia: “ ni adhabu gani uipatayo ewe umu umarah, akajibu”: “lakini ninaweza kuivumilia, ninaweza, ninaweza ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Mtume (rehma na amani zimshukie) niombe ewe Umu Umarah” akasema: “naomba niwe nawe peponi ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Mtume (rehma na amani zimshukie) akasema sio wewe peke yako bali na watu wa nyumba yako pia. Akasema (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) sijali kwa yanipatayo duniani.” Kitabu cha Siyra A`alam Anubalaa)

Na iwapo tunataka kuendelea na kuokoa na matatizo na kufanikiwa kwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu hapa duniani na kesho akhera, basi hatuna budi tufuate mwangaza tuliomurikiwa kwa nuru ya masahaba wa Mtume (rehma na amani zimshukie) na kufuata mwenendo waona tabia zao, wao ni kigezo cha waumini na waislamu wote. Mtume (rehma na amani zimshukie ) katuhimiza kuwafuata na kushikamana na mwenendo wao pia, kutoka kwa Urbaadh bin Sariyah kuwa Mtume (rehma na amani zimshukie) amesema: “ jilazimisheni kufuata mwenendo wangu na mwenendo wa makhalifa walioongoka, na chukueni kwa kukaza magego, na tahadharini na yenye kuzuka, kwani kila la uzushi ni upotofu.” (Ibn Majah).

Na juu yetu kujifunza na watoto wetu na wake zetu juu ya mwenendo wa masahaba watukufu, ni namna gani walikuwa wakimfuata Mtume (rehma na amani zimshukie) na kujitolea kwao muhanga kwa ajili ya kuinusuru dini na kumnusuru Mtume (rehma na amani zimshukie) kwani waliziuza nafsi zao kwa ukweli na kwa uyakini hii yote ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu.