Mweleweko wa Ahadi ya Usalama katika zama zetu.

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa Viumbe vyote, anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْؤُولاً}

Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi ni yenyeuulizwa.

Na ninashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, asiye na mshirika wake, na ninashuhudia kuwa Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad, ni Mja wake na Mjumbe wake, anaesema katika Hadithi yake Tukufu: Hakika waja wa Mwenyezi Mungu mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaotekeleza ahadi zao na wanaofanya mazuri. Ewe Mola wetu, Mswalie na umpe rehma na amani na umbariki Mtume wetu S.A.W, na Ali zaki na Maswahaba wake, na kila mwenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

Na baada ya Utangulizi huu;

Hakika Uislamu ni Dini Usalama, amani, utendaji wa mazuri na wema; na hakuna shaka yoyote kwamba utekelezaji wa Ahadi una thamani kubwa ya kimaadili na kibinadamu inayounga mkono kujiamini na kuleta usalama na amani baina ya mataifa yenyewe kwa yenyewe, na kukuza mahusiano mazuri na upendo pamoja na kujenga na kusonga mbele kinaendeleo kwa wananchi wa taifa moja, na kwa hivyo, utekelezaji wa ahadi ni sehemu ya imani na ni dalili miongoni mwa dalili za ukweli na Wema, na ni Adabu ya kidini iliyo bora, na tabia njema pamoja na mienendo ya kiislamu iliyonyooka.

Hakika Uislamu umewaamrisha wafuasi wake umuhimu wa kuwa na tabia za kutekeleza ahadi zao na mikataba pamoja na makubaliano, na ukasisitizia hayo kwa nguvu zote pale aliposema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَأَوْفُواْ بِالْعَهْدِ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْؤُولاً}

Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi ni yenye kuulizwa.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَأَوْفُواْ بِعَهْدِ اللّهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلاَ تَنقُضُواْ الأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا وَقَدْ جَعَلْتُمُ اللّهَ عَلَيْكُمْ كَفِيلاً إِنَّ اللّهَ يَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ}

Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi, wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo.

Kwa maana ya kuwajibika na utekelezaji wa ahadi zote mlizojiwajibisha nyinyi wenyewe, iwe baina yenu au baina yenu na Mwenyezi Mungu Mtukufu, au baina yenu na watu wengine, na wala msitokwe na imani baada ya kuwa mmekwishajihakikishia ndani ya nyoyo zenu. Na mkamfanya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa ndiye mlezi wenu na mdhamini wenu pale mlipoahidi. Na yoyote atakayepitisha makubaliano basi anawajibika kuyaheshimu, na atakayetoa ahadi anawajibika kuitekeleza. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba watekelezaji wa Ahadi zao na mikataba yao wao ndio watu wa upendo na wao ndio watu wa ukweli na uchamungu kwa Muumba wao. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{بَلَى مَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ وَاتَّقَى فَإِنَّ اللّهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ}

Sivyo hivyo, bali anaye timiza ahadi yake na akamchamngu basi Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُواْ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاء والضَّرَّاء وَحِينَ الْبَأْسِ أُولَـئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَأُولَـئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ}

Na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha kwamba watu hao ndio wenye malipo makubwa, na ni warithi wa pepo. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَمَنْ أَوْفَى بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا}

Na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.

Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akabainisha malipo haya makubwa katika sehemu nyingine ya Qurani Tukufu aliposema:

 {وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ * وَالَّذِينَ هُمْ بِشَهَادَاتِهِمْ قَائِمُونَ * وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ * أُولَئِكَ فِي جَنَّاتٍ مُكْرَمُونَ}

Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao, Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao, Na ambao wanazihifadhi Sala zao. Hao ndio watakao heshimiwa Peponi.

Na Mtume S.A.W amenyanyua thamani ya kutekeleza ahadi na akaonya kwa mwenye kuivunja, au kutoitekeleza ipasavyo; ambapo katika kufanya uhaini wa kutoitekeleza ahadi kuna ufisadi katika jamii mbali mbali. Na kwa mujibu wa Imani baina ya watu, na upotezaji wa amana za watu, Mtume S.A.W anasema:

Alama za Mtu Mnafiki ni tatu: Anapozungumza husema uongo, na anapoahidi huenda kinyume na ahadi yake, na anapoamini hufanya hiana. Na anasema Mtume S.A.W: Waislamu hufuata Masharti yao waliojiwekea, isipokuwa sharti linaloharamisha kilichohalalishwa au kuhalalisha kilichoharamishwa. Na Mtume S.A.W ameonya kuhusu adhabu ya Mtu aliyevunja ahadi yake akasema: Mwenyezi Mungu atakapowakusanya Wa Mwanzo na wa Mwisho siku ya Kiama, patanyanyuliwa alama kwa kila Mvunja ahadi na patasemwa: Alama hii ni alama ya uvunjaji wa Ahadi wa Fulani bin Fulani. Anasema Ibnu Kathiir R.A: Na hekima iliyopo katika jambo hili ni kwamba kwa kuwa kwenda kinyume na ahadi hutokea kwa kificho, watu hawawezi kuona kinachoendelea, itakapofika siku ya Kiama, jambo hili litawekwa wazi kwa kuwekewa wazi muhusika kile alichokifanya, na hivyo ndivyo yatakapowadhihirikia watu yale yaliyokuwa yakifanywa kwa siri na wahusika, miongoni mwa vitimbi na uhaini, na Mwenyezi Mungu atawafedhehesha wahusika mbele ya viumbe vyote. Na kwamba katika jumla ya ahadi zilizoamrishwa na Sheria ya Uislamu iliyo tukufu zitekelezwe, na kuthibitisha utekelezaji wake, na kutozivunja, ni ahadi ya Usalama; nao ni kwa mujibu wa mweleweko wa zama hizi: Ni kile kinachotolewa na nchi, kama kibali au visa vya kuingilia nchi nyingine, au idhini ya kuingia nchini mwake kwa wananchi wa nchi nyingine, iwe ni kwa sababu za kitalii au matembezi  au kuishi, kwa mujibu wa taratibu na mikataba na makubaliano ya kimataifa ya kuamiliana na wanadiplomasia, na wanaokuwa katika hukumu ya wanadiplomasia, au kwa mujibu wa mikataba na makubaliano ya nchi mbili kwa njia yoyote miongoni mwa njia zilizopitishwa na zinazokubalika kisheria, na kutambuliwa na nchi yenye kupokea wageni kwa mujibu wa sheria zilizopo na baada ya mtu kupata kibali tu cha kuishi, au kibali cha kuingia nchi hiyo au idhini ya kuingia, basi mtu huyo atakuwa tayari ana haki na heshima katika nchi hiyo na anakuwa katika mkataba ambao umetolewa na nchi kwa ajili ya kila mwananchi na yoyote anayeishi ndani ya nchi hiyo kuwajibika na kuufuata ipasavyo, na haijuzu kuuvunja au kwenda nao kinyume, au hata kuuvuruga, haifai kisheria wala kikanuni. Na yoyote atakayeona katika watu jambo linalokiuka sheria na kuugusa usalama wa nchi yake au kinyume na mfumo wa serikali yake, hana budi isipokuwa kutoa taarifa kwa wahusika ili waweze kulishughulikia na kuchukua hatua zinazofaa, mpaka vyombo vya dola viweze kumchukulia hatua mtu huyo kwa yale aliyoyafanya, kwa mujibu wa sheria na taratibu zake, kwani hakuna mtu yoyote anayeweza kumchukulia hatua mtu huyo kwa yale aliyoyafanya au yaliyomkuta kwa kukiukwa haki yake na kama hatua haitachukuliwa basi jambo hili linaweza kupelekea machafuko na kutodhibitika tena.

Na miongoni mwa mambo yasiyo na shaka ndani yake ni kwamba, utekelezaji wa ahadi hii ni katika mambo ya wajibu na yenye kutekelezwa kisheria, kikanuni, kitaifa, na hata kibinadamu. Kama Dini yetu tukufu imenyanyua cheo cha Ahadi ya Usalama, kama ni jukumu la waislamu wote kwa pamoja, maana yake ni kwamba ahadi anayoiahidi mwislamu yeye mwenyewe inakuwa wajibu kwa wote waliopamoja naye, inakuwaje ikiwa ahadi hiyo ni mkataba unadhibitiwa na kupangiliwa na sheria pamoja na kanuni, kwa kushirikiana, kila mmoja kumtia nguvu mwingine na kumuunga mkono na kuwajibisha? Basi hapana shaka kwamba hiyo hupelekea katika utekelezaji wa  majukumu na mikataba ya ahadi, na wala sio kuivunja au kuipoteza, na hata kuigusa tu.

Hakika uislamu ni Dini inayolinda Ahadi za aina mbali mbali na mikataba, Dini isiyotambua udanganyifu, wala haitambui hadaa, au hiyana, na haikuthibiti wakati wa Mtume S.A.W,  – tangu mwanzo wa Ulinganiaji wake – wala kutoka kwa Swahaba wake yoyote kati ya maswahaba wake R,A, kwamba waliwahi kumnyima Usalama mtu yoyote, au waliwahi kuvunja ahadi walioitoa kwa mtu yoyote, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu akimsemesha Mtume wake S.A.W:

{وَإِمَّا تَخَافَنَّ مِن قَوْمٍ خِيَانَةً فَانبِذْ إِلَيْهِمْ عَلَى سَوَاء إِنَّ اللّهَ لاَ يُحِبُّ الخَائِنِينَ}

Na ukichelea khiana kwa watu Fulani basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hawapendi makhaini.

Na siku Bwana wetu Muawiya alipokuwa na Mkataba wa Ahadi baina yake na Taifa la Warumi, na Muawiya akataka kutoka karibu na mipaka ya Warumi, pindi mkataba utakapokwisha atawashambulia, Mtu mmoja miongoni mwa Maswahaba wa Mtume S.A.W akamuwahi huku akisema: Mwenyezi Mungu Mkubwa, Mwenyezi Mungu Mkubwa, Tunapaswa kutekeleza ahadi na wala sio kuivunja. Maswahaba wote wakamwangalia, alikuwa ni Amru bin Absah, R,A, Muawiya R.A, akamtumia mtu, akamuuliza, akasema: Nimemsikia Mtume S.A.W akisema: Mtu yoyote anaewekeana ahadi na watu, basi asiikaze ahadi yake au kuilegeza, mpaka atakapoitimiza jinsi ilivyopangwa, au akawatupia mkataba wao ni sawa na kuuvunja, Muawiya akarejea, bali utukufu wa Uislamu ukaonekana na kudhihiri wazi wazi katika sura zake za hali ya juu, katika amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mtume wake S.A.W. kusaidia mtu anayeomba msaada wa kuokolewa hata kama mtu huyo ni mshirikina, bali hata kama mtu huyo atakuwa ni adui wa Waislamu, ambapo

anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{و َإِنْ أَحَدٌ مِنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّى يَسْمَعَ كَلَامَ اللهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَعْلَمُونَ}

Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.

Mtume S.A.W amejenga misingi imara ya Maadili haya yanayoleta Usalama na amani kwa binadamu, kama asemavyo Mtume wetu S.A.W: Hana Imani Mtu asiyekuwa Mwaminifu, na wala hana Dini Mtu asiyekuwa Ahadi (kwa maana asiyetekeleza ahadi).

Na anasema Mtume S.A.W: Mtu yoyote atakayemuua Mtu aliyewekeana naye Ahadi, basi hata inusa harufu ya Pepo, na kwamba Harufu ya pepo inapatikana umbali wa mwendo wa miaka arubaini.

Na anasema Mtume S.A.W: Mwislamu ni Yule ambaye Watu wote wamesalimika na Ulimi wake na Mkono wake, na Muumini ni Yule ambaye maisha yao pamoja na mali zao vimesalimika naye. Na huyu hapa Mtume S.A.W anatujengea sisi kiutendaji mifano mizuri ya utekelezaji wa ahadi mpaka ile ahadi yake na maadui zake; Kutoka katika Siku ya Badri, anasema Hudhaifa bin Yamaan R.A: Hakikunizuia mimi kuishuhudia Badri isipokuwa mimi nilitoka nikiwa mimi na Baba yangu, tukawachukua makafiri wa Kikureshi, wakasema:  Hakika nyinyi mnamtaka Muhammad, tukasema: Hatumtaki yeye. Hatutaki isipokuwa Madina, Wakachukua kutoka kwetu ahadi ya Mwenyezi Mungu na miadi yake, kwamba: tutaelekea Madina, na wala hatutapigana tukiwa pamoja naye, tukaja mpaka kwa Mtume S.A.W, na tukamweleza habari hii, akasema S.A.W: Nendeni tunawatekelezea ahadi yao, na tunamwomba msaada Mwenyezi Mungu Mtukufu juu yao.

Na kwa kauli hiyo ya Mtume S.A.W, hakika sisi sote, tunawajibika kuzilinda ahadi tunazozitoa na kuwekeana na watu, pamoja na mikataba ambayo nchi inatuwajibisha tuitekeleze kwa kila mtu ndani ya nchi yetu na tuwe ni wenye kushirikiana katika kuyalinda maisha yake, heshima yake, na maisha yake binafsi, ambapo tuna wajibu pia wa kumkaribisha vizuri, na kumkirimu; ili aone katika sisi yale tuyapendayo ayaone katika macho yake na akili yake kuhusu utukufu wa Dini yetu, na undani wa Ustaarabu wetu, na utukufu wa utu wetu; kwa namna inayochangia katika kujenga picha ya kiakili tuitakayo sisi, na kwa Taifa letu, na Jamii yetu, nah ii ndio hali ya kila Umma na Mataifa yaliyo juu kiustaaranu.

Ninaisema kauli yangu hii, na nimamwomba Mwenyezi Mungu pamoja na kukuombeeni nyinyi msamaha.

*   *   *

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mola wa viumbe vyote. Na ninashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ninashuhudia kuwa Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad nMja wake na ni Mjumbe wake. Ewe Mola wetu tunakuomba umswalie Mtume na umpe rehma na amani na umbariki, yeye na Aali zake na Maswahaba wake wote, na kila atakayemfuata kwa wema mpaka siku ya Mwisho, siku ya Malipo.

 Ndugu zangu Waislamu.

Hakika Uislamu ni Dini ya Uadilifu, Usamehevu na kuishi kwa amani. Na Mwislamu daima anatakiwa kuishi katika amani na usalama, amani katika kila sehemu anayokuwapo, ndani ya nchi yake au nje ya nchi yake; na anapohama Mwislamu huyu na kwenda katika nchi nyingine, iwe nchi hiyo ni ya kiislamu au sio ya kiislamu, hakika ruhusa ya kuingina inayotolewa na nchi hiyo inakuwa ni kama mkataba wa usalama, ambapo atakuwa na amani na usalama huko aendako, na ruhusa hiyo ni kama mkataba wa Usalama wake kwa wenye nchi hiyo; wanampa usalama kamili, na wanasalimika naye kwa mali na nafsi zao, na unamuwajibisha mkataba huo kufuata sheria zote za nchi hiyo na kuwajibika kikamilifu na anatakiwa atekeleze wajibu wake wa usalama na ukweli. Anazuiwa kuchukua kitu chochote katika mali za watu kinyume na sheria, au kuishambulia heshima ya mtu yoyote, au kuvunja ahadi anayotakiwa kuitekeleza kwa njia yoyote miongoni mwa njia za kuvunja ahadi, mpaka awe balozi mzuri wan chi yake, Dini yake na Ustaarabu wake. Pindi anapoingia tu katika nchi hiyo, anakuwa tayari anawajibika na anakuwa ameshaweka ahadi na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atatekeleza, mpaka asije akajikuta katika hali aliyoisema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَالَّذِينَ يَنْقُضُونَ عَهْدَ اللَّهِ مِنْ بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّهُ بِهِ أَنْ يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ أُولَئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ}

Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.

Anasema Imamu Shafi Mwenyezi Mungu amrehemu, katika kitabu chake cha Ummu: Mwislamu anapoingia katika nchi isiyokuwa ya Kiislamu kwa kuwa na amani nao, basi hairuhusiwi kwake kuchukua chochote katika mali zao – ziwe nyingi au kidogo – hata kama wao walikuwa katika hali ya vita na waislamu; kwani yeye akiwa nao anakuwa katika usalama wao, na wao wanapokuwa naye pia wanakuwa nae katika usalama kama ilivyo yeye na wao. Na kwa kuwa haijuzu  kwake katika usalama wao isipokuwa vinavyokuwa halali katika mali za waislamu.

Nimetosheka na kuyataja maneno ya Imamu Shafi na kuyanasibisha na kitabu chake cha Ummu; kwa kuchelea kuingia katika upembuzi wa kifiqhi unaoweza kuwa na baadhi ya mambo yasiyokubaliwa na baadhi ya watu. Na ninaliacha jambo hili kwenu.

Anasema Mshairi:

Utekelezaji wa Ahadi ni katika Sifa za watu wema

Na uvunjaji wa ahadi ni katika sifa za waovu

Na kwangu mimi hakizingatiwi kitu kuwa katika mazuri

Isipokuwa kulinda upendo na kuzuia uchonganishi

Ewe Mola wetu tuongoze katika Tabia njema zaidi, hakuna wakutuongoza tukelekea kwenye bora zaidi isipokuwa wewe. Na tunakuomba utuepushe na ubaya wake, na hakuna wa kutuepusha nao isipokuwa wewe.