Tunayojifunza kutokana na Hotuba ya Kuaga ya Mtume S.A.W.

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa viumbe vyote, asemaye katika Kitabu chake Kitukufu:

{الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الإِسْلامَ دِينًا}

Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.

Na ninashuhudia kuwa hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni yeye pekee asiye na mshirika wake, na ninashuhudia kuwa Bwana wetu na Mtume Wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola Wetu mswalie, mrehemu na umbariki Mtume Wetu na Jamaa zake, na Maswahaba wake na kila mwenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

Na baada ya Utangulizi huu:

Hakika mwenyezi Mungu Mtukufu amemtuma Mtume wake S.A.W, kwa Uongofu ili awatoe Watu katika giza na kuwapeleka katika vyao mwanga na awachukue kwa nywele zao za mbele ya vichwa vyao kutoka katika upotofu na kuelekea katika uongofu na anawapitisha katika njia ya Uokovu na Furaha Duniani na Akhera. Mtume S.A.W ameyalingania Maadili bora na Ruwaza ya hadhi ya juu, na ameufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika sura ya ukamilifu wake na iliyotimia, na akawa katika zama za Uhai wake anaweka misingi imara ya kibinadamu kwa maneno yake, vitendo vyake na upitishaji wake wa yale anayoyaona kuwa yanafaa

   

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomuidhinishia Mtume Wake S.A.W, utekelezaji wa Nguzo ya Tano katika Nguzo za Uislamu, Mtume S.A.W alisimama katika eneo la Milima ya Arafaat katika Mawe, katika Mjumuiko mkubwa wa watu kwa wakati huo, akizichambua Ibada mbalimbali za Hija kwa Maswahaba wake na kwa umma ujao baada yao, na akiweka misingi imara ya Maadili ya Kibinadamu na ya Kitabia ambayo aliendelea kuyalingania katika maisha yake yote, huku akihisi kukaribia kifo chake na kumalizika kwa umri wake. Na kwa hivyo, hotuba yake ilikusanya mambo mengi muhimu ya kujifunza na mazingatio ya hali ya juu ambayo yanazingatiwa kuwa ni Mfumo wa Maisha ya Watu wote

Na miongoni mwa mafunzo ya hotuba yake ni: Kujenga Misingi imara ya Uadilifu na Usawa baina ya Watu wote. Anasema Mtume S.A.W: Enyi Watu:Hakika Mola wenu Mlezi ni Mmoja. Na Hakika Baba yenu ni Mmoja. Tambueni kwamba hakuna ubora wowote wa mwarabu kwa muajemi, wala muajemi kwa mwarabu, wala mwekundu kwa mweusi, wala mweusi kwa mwekundu, isipokuwa kwa Uchamungu. Hakika Mbora wenu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mchamungu…

Mtume S.A.W aliufanya Uchamungu na Matendo mema kuwa ni kigezo cha mtu kuwa bora zaidi ya mwingine kwa kuitekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ}

Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari

Kwa hiyo, Watu wote ni sawa kwa upande wa haki na wajibu bila ya kumbagua yoyote kimatabaka, kasumba ya kikabila, na haya yanatokana na Uadilifu ambao ndio kipimo cha kusimamisha haki na Uuwianifu wa Mataifa.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُواْ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَى}

Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُواْ بِالْعَدْلِ}

Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى}

Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu.

Na katika faida hizo pia: ni Ulinzi wa Maisha na Mali pamoja na Heshima za watu. Kutoka kwa Abdurahman bin Abuu Bakra R.A, kutoka kwa Baba yake anasema: Mtume S.A.W alikuwa ameketi juu ya ngamia na mtu mmoja alikuwa ameushika utepe wa kumswagia ngamia kisha akasema S.A.W: Leo ni siku gani? Tukanyamaza mpaka tukadhani kwamba Mtume aipa siku hiyo jina jingine. Akasema Mtume S.A.W: Je leo sio siku ya kuchinja? Tukasema: Ndio. Akasema: Kwani huu ni mwezi gani? Tukanyamaza mpaka tukadhani kwamba Mtume S.A.W, ataupa mwezi huu jina jipya. Akasema Mtume S.A.W: Je mwezi huu sio wa Dhulhijah? Tukasema: Ndio. Akasema: Hakika Damu zenu, Mali zenu na Heshima zenu ni Haramu kama ilivyo Haramu ya siku yenu hii katika mwezi wenu huu na katika Mji wenu huu. Aliyekuwepo amfikishie asiyekuwepo. Kwani huwenda aliyekuwepo akamhadithia aliye mtambuzi zaidi kuliko yeye.

Katika jambo hili, Mtume S.A.Waliwazindua Maswahaba wake na akaziamsha zaidi akili zao kwa maneno haya bobezi ambayo yamekusanyika katika mwenendo huu wa Mtume S.A.W wenye mtazamo wa kina unaoonesha uzito wa kuyaheshimu maisha ya binadamu, mali na heshima yake na Ulinzi wake, na kwamba haiwi halali kumshambulia mtu kwa ushambuliaji wa aina yoyote. Uislamu unalingania Usalama na Amani, Utulivu na Salama. Na Uislamu unawataka Watu wote waishi maisha ya utulivu bila ya ubaguzi au utofautishaji baina ya mtu na mwingine bila kujali jinsia yake, rangi yake au hata Dini yake kwani Sheria ya Uislamu imemlindia yote haya kila mtu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ذَلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ}

 Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekufanya kuiua nafsi moja bila ya haki ni sawa na kuwaua Watu wote. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {مَن قَتَلَ نَفْساً بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الأرض فَكَأَنَّمَا قَتَلَ الناس جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا}

Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote.

Kwa kuthibitisha uharamu wa kuua na kumtia hatiani muhusika, Mtume S.A.W ameonya onyo jingine katika hotuba yake hii, onyo ambalo linahusika na uharamu wa kuua ambapo anasema Mtume S.A.W: Msirejee tena kwenye Ukafiri baada yangu mimi, mkauana wenyewe kwa wenyewe. Kama ambavyo Uislamu umeharamisha kuishambulia nafsi, umeharamisha pia kushambulia mali za Watu kwa aina yoyote ya mashambulizi, ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

 {يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُمْ بَيْنَكُمْ بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَنْ تَكُونَ تِجَارَةً عَنْ تَرَاضٍ مِنْكُمْ}،

Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe.

 Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

 {وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُمْ بَيْنَكُمْ بِالْبَاطِلِ وَتُدْلُوا بِهَا إِلَى الْحُكَّامِ لِتَأْكُلُوا فَرِيقًا مِنْ أَمْوَالِ النَّاسِ بِالْإِثْمِ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ}

Wala msiliane mali zenu kwa baat’ili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.

Kwa ajili ya kuzilinda Mali za Mali kwa ujumla, Sheria ya Kiislamu imeuharamisha wizi na kuuwekea adhabu kali ikemeayo.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ}

Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Na Sheria ya Uislamu imeharamisha pia upokonyaji wa aina zote wa Ardhi za Watu, ambapo Mtume S.A.W, anasema: Mtu yoyote atakayedhulumu kiasi cha upana wa vidole kumi na mbili moja ya ardhi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamtwisha shingoni kwa ardhi hiyo siku ya Kiama uzito wa ardhi saba.

    Na vile vile Uislamu umeharamisha uadui wa heshima za Watu au hata kuzigusa vyovyote iwavyo, na hakuna tofauti kati ya mwislamu na asiye mwislamu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَا إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا}

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.

Uislamu pia umeharamisha kuwatuhumu uzinzi Wanawake wenyekujiheshimu na ukazingatia kuwa hili ni katika Madhambi Makubwa. Na Mtume S.A.W anasema: Jieousheni Mambo saba yaangamizayo. Akaulizwa: Ni yepi hayo Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu? Akasema: … Kuwatuhumu uzinzi Wanawake wanaojiheshimu, walioghafilika, Walio Waumini…. Na Mtume S.A.W amekataza Matusi na kutukana kwa ujumla na akaiita Tabia hii ya kutukana kama Uovu akasema Mtume S.A.W: Kumtukana Mwislamu ni Uovu na kupigana nae ni Ukafiri.

Na miongoni mwa ya kujitunza ni: Ulinganiaji wa Umoja na kuonya juu ya migawanyiko ambapo anasema Mtume S.A.W katika hotuba yake ya kuaga: Hakika Shetani amekata tamaa ya kuabudiwa katika Nchi yenu hii, katika zama za mwisho. Na amekuridhieni kutoka kwenu matendo maovu basi tahadharini nae katika Dini yenu… Kwa hiyo tuungane na tushikamane kwa kamba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Sisi sote, kwa kuiitikia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu anaposema:

 {وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُواْ}

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَأَطِيعُواْ اللّهَ وَرَسُولَهُ وَلاَ تَنَازَعُواْ فَتَفْشَلُواْ وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ}

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.

Na tutambue kwamba Dni ya Uislamu haina uhusiano wowote na mparaganyiko pamoja na mgawanyiko.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُواْ دِينَهُمْ وَكَانُواْ شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ }

Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano wowote nao. Kwa hivyo, Uislamu unalingania Umoja na unaharamisha Gomvi na Mgawanyiko.

Na katika tunayonufaika nayo: Ni Wajibu wa kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunna ya Mtume S.A.W, ambapo anasema Mtume S.A.W: Na hakika nimekuachieni ambapo hamtapotea kamwe iwapo mtashikamana nacho, Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na nyinyi ndio mnajukumu la kunifikishia…

Na kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Muujiza kudumu Milele, haujiwi na Batili kwa mbele au kwa nyuma yake, haubadiliki wala haugeuki miaka na miaka inayopita. Na karne na karne ziendazo. Mwenyezi Mungu ameondosha kwayo na kwa Sunna ya Mtume S.A.w, Matamanio, na kumaliza kwavyo aina zote za hitilafu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ فَإِنْ تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ إِنْ كُنْتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا}

Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.

Na kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunna ya Mtume S.A.W ni alama ya Imani na ni Dalili ya Uchamungu, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّى يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنْفُسِهِمْ حَرَجًا مِمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا}

La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenyekee kabisa.

Ninaisema kauli yangu hii na ninamwomba Msamaha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili yangu na kwa ajili yenu.

*        *        *

Sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu Bwana Mlezo wa viumbe vyote, na ninashuhudia na kukiri kuwa hapana mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye Mwenyezi Mungu Mmoja asiye na Mshirika wake, na ninakiri na ninashuhudia kuwa Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu mswalie, mrehemu na Umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote. Hapana Shaka kuwa Hotuba ya Hija ya Kuaga aliyoitoa Mtume S.A.W, ndio kumbukumbu ya kwanza na azimio la kimataifa la ulinzi wa Haki za Binadamu, kutokana na maadili iliyoyakusanya ndani yake ambayo yanaulinda utukufu wa Mwanadamu na kumletea udalama na amani yake. Na katika faida muhimu za mafunzo zinazopatikana ndani ya Hotuba hiyo: ni ubainifu wa sheo cha mwanamke na nafasi yake katika Sheria ya Uislamu. Mtume S.A.W ameusia kuhusu Mwanamke kwa kumpa uzito wake, na akaweka wazi nafasi yake. Wanawake ni ni ndugu wa wanaume, na Haki na Majukumu ni ya pande mbili baina yao. Anasema Mtume S.A.W: Hakika mna nyinyi juu ya wanawake wenu Haki na wao wana juu yenu haki. na Uislamu umempa heshima kubwa Mwanamke, awe ni mama, dada, binti au mke. Na kumfanya awe na Haki zinazoidhamini furaha yake ya Duniani na Akhera, na kumlinda pamoja na kuuhifandhi utukufu wake wa kibinadamu. Na Mtume S.A.W alipoulizwa: Ni nani mwenye haki zaidi ya kuwa naye katika watu? Mtume S.A.W akasema: Ni mama yako. Kisha akasema yule muulizaji: Kisha nani? Mtume akasema: kisha Mama yako. Akasema yule muulizaji: kisha nani? Mtume akasema: kisha mama yako. Kisha akasema tena yule muuliza: kisha nani? Akasema Mtume S.A.W; kisha Baba yako. Na anasema Mtume S.A.W: Mtu atakayekuwa na watoto wa kike watatu na akawavumilia, akawalisha na kuwanywesha, akawavisha kwa jasho lake, basi sisi tutakuwa kwake yeye siku ya Kiama kizuizi cha Moto. Na katika mapokezi mengine. Anasema Mtume S.A.W: Mtu yoyote atakayewalea watoto wawili wa kike,  au watatu, au dada zake wawili au watatu, mpaka watakapoolewa  au akafariki dunia na kuwaacha, basi mimi nay eye tutakuwa kama vidole hivi, akaashiria kwa vidole viwili; cha tatu na cha shahada. Na kutoka kwa Abu Huraira R.A, amesema: Anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: Usianeni juu ya wanawake, kwani mwanamke ameumbwa kwa mbavu ya mwanaume, na hakika kitu kilichopinda zaidi katika mbavu ni kilicho juu yake, na utakapoenda kutaka kuinyoosha utaivunja, na ukiiacha itaendelea kuwa imepinda, basi usianeni wema juu ya wanawake. Neno kheri katika Hadithi hii ya Mtume ni neno linalokusanya maana pana zaidi ambapo linaashiria uwajibu wa kujipamba kwa maana bora za uwanaume pale wanaume wanapotangamana na wanawake. Haja iliyoje kwetu sisi ya kuyatekeleza maadili haya yenye thamani kubwa ambayo yamezikusanya kheri nyingi kwa ajili ya ubinadamu.

 Hakika Maadili haya yamekuja yakizitangulia zaka katika historia ya Ubinadamu na ya Kitabia ambayo kama watu watayazingatia vyema na wakayaingiza akilini mwao na wakayafanyia kazi ipasavyo, basi hapana shaka kwamba hiyo itakuwa ndiyo sababu ya furaha yao Duniani na Akhera.

Ewe Mola wetu Mlezo tukubalie sisi hakika wewe ni Msikivu Mjuzi, na tunakuomba utupokelee toba zetu hakika Wewe ni Mwingi wa kupokea Toba na Mpole mno.

  َّ