- أوقاف أونلاين - https://foreign.awkafonline.com -

Maadili Makuu na Athari kubwa katika kuyainua Mataifa

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa viumbe vyote, anaesema katika Qurani tukufu:

{قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَى صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِّلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ}

Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye kuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.

Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, aliye pekee na hana mshirika katika Ufalme wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad, Ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu Mlezi, tunakuomba umswalie, umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake pamoja na Maswahaba wake wote, na watakaowafuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

Na baada ya Utangulizi huo:

Hakika Mtaifa yaliyostaarabika na kuendelea ndio yanayoyachunga Maadili Makuu na kuyafanya kama mfumo wa Maisha. Na Maadili haya sio maneno tu yasemwayo au kitu kinachotengwa maishani; bali Maadili hayatengani na Mfumo mkuu wa Tabia nzuri za Binadamu na jambo hili linaambatana na mafunzo ya Dini yetu Tukufu ambayo imewekwa mkusanyiko wa Maadili Makuu ambayo yanapangilia Uhusiano wa Binadamu na Mola Wake Mlezi na uhusiano wake na Ulimwengu.

Na katika Maadili haya Makuu, ni Usafi. Uislamu unausisitizia sana Usafi wa mwili, nguo, na eneo, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ وَإِنْ كُنْتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا وَإِنْ كُنْتُمْ مَرضى أَوْ عَلَى سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِنْكُمْ مِنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ مِنْهُ مَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُمْ مِنْ حَرَجٍ وَلَكِنْ يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ}

Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ}

Na nguo zako, zisafishe.

Na Mtume S.A.W, anasema: Mmoja wenu anapoamka kutoka usingizini, asiuingize mkono wake kwenye chombo mpaka auoshe mara tatu.

Na anasema Mtume S.A.W: Waogopeni watu wawili waliofukuzwa kwenye rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wakamuuliza: Ni akina nani hao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu? Akasema: Ni yule ambaye huenda haja katika njia ya watu au katika kivuli chao.

Na Uislamu umefungamanisha baina ya Usafi wa mwili na usafi wa Roho, na ukaufanya usafi wa mwili ukawa ni katika sababu za Usafi wa Roho. Kwani mwanadamu anapoulinda usafi wa mwili wake basi huwa ni sababu ya kusamehewa madhambi yake, ambapo Mtume wetu Muhammad S.A.W, anasema: Mja Mwislamu au Muumini anapotawadha kisha akauosha uso wake, yataondoka na maji katika uso wake makosa yote aliyoyaangalia kwa macho yake, au tone la mwisho la maji, na ikiwa ataiosha mikono yake miwili, basi yataondoka na maji makosa yote yaliyofanywa na mikono yako au na tone la mwisho la maji, na akiosha miguu yake miwili makosa yote yaliyopitwa na miguu yake yatatoka na maji au na tone la mwisho la maji mpaka atoke akiwa msafi hana dhambi hata moja.

Kama unavyohimiza Uislamu Usafi wa mtu, unahimiza sana pia Usafi wa watu wote. Anasema Mtume S.A.W: Safisheni viwanja vyenu. Na viwanja hapa ni maeneo yote ya nyumbani kwa mtu, kiwandani au hata shuleni na katika makongamano na maeneo yote ya uma yanayotembelewa, ukijumuisha na barabara na njia pamoja na viwanja vya Uma na maeneo mengine mengi. Kwa hiyo, ni wajibu kuyalinda maeneo hayo yote na kutoonekana chochote kisichostahiki kuwapo, na kuyaacha yakiwa masafi kuliko yalivyokuwa, na kuchangia katika kuyasafisha.

Na katika Maadili hayo ni: Kuheshimu Nidhamu, kwani hapana budi kwa kila jamii kuwa na baadhi ya Nidhamu na Misingi ya kiadilifu ambayo inadhibiti mienendo ya kila mmoja, na inamlindia kila mtu haki zake na kumwajibisha katika kuyatekeleza majukumu yake ipasavyo, na hivyo kuleta masilahi ya taifa ambayo humgusa kila mwananchi. Na yoyote anaezingatia mazingira ya nchi zilizoendelea na jamii zilizokwea juu kihadhi, ataona kwamba hazikufika hivyo isipokuwa kwa kuheshimu Misingi yake na kujiwajibisha katika kuitekeleza. Na jambo hilo hujenga mazingira ya kuheshimu haki za wengine na ni msingi wa haki kwa kutekeleza wajibu. Na mtu akawatendea watu vile anavyotaka atendewe yeye. Na huo ni ukamilifu wa Imani. Anasema Mtume S.A.W: Haamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye kile anachokipendelea kwa nafsi yake. Na haya ni majukumu ya kila mtu bile kutengwa. Anasema Mtume S.A.W: Nyinyi nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kwa kile alichokichunga. Imamu ni mchunga na ataulizwa kuhusu aliowachunga. Na Mwanaume ni mchunga wa Watu wake na ataulizwa kuhusu aliowachunga. Na Mke ni mchunga wa nyumba ya Mumewe na ataulizwa alichokichunga. Na Mtumishi ni mchunga wa Mali za Mwajiri wake na ataulizwa alichokichunga.

Kwa hiyo, kuiheshimu nidhamu na kuwajibika na masharti yake huenezwa Uadilifu na kusambaza moyo wa upendo na undugu na jamii huneemeka kwa Usalama, Amani na Utulivu.

Na katika Maadili ni: Ni kuchunga Hisia za Watu wote, ambapo Uislamu umekuja kwa kila kinachounyoosha Mwenendo na kuinyanyua juu hadhi ya hisia na kuzisogeza nyoyo zikawa pamoja kwa mujibu wa Misingi Mikuu wasiohitilafiana Watu pamoja na kuheshimu Mila na desturi za Watu na mambo walioyazoea. Hakika Sheria ya Uislamu imepitisha kila kizuri kisichochukiwa na Watu na ikakiharamisha kila kibaya kinachowadhuru Watu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ}

Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu…

Na kuzichunga hisia za Wote kunahukumia: Mtu kutumia vizuri mavazi yake, chakula chake, vinywaji vyake, na kujiepusha na Ubadhirifu unaokatazwa kisheria, na mwonekano usiokubalika. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِنْدَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ}

Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanaofanya israfu.

Vile vile ni lazima kuheshimu na kutekeleza ahadi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَوْفُوا بِالْعُقُودِ}

Enyi mlio amini! Timizeni ahadi.

Vilevile ni lazima kuheshimu Hisia za Watu wote katika kutembea, Mavazi na Ujumla wa Mazingira. Kutoka kwa Jaabir R.A, kwamba Mtume S.A.W, amekatazwa mtu kuunyanyua mguu wake juu ya mguu mwingine mbele ya Watu wengine huku akiwa ameulalia mgongo wake.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Kamba ya kandambili ya mmoja wenu inapomkatikia basi asiitembelee nyingine mpaka atakapoitengeneza iliyomkatikia. Lengo hapo ni kuchunga mazingira ya uma. Na katika kuchunga Hisia za Uma, ni kutotoa sauti kali mbele ya Watu, au kufanya kitendo kinachowachukiza Watu. Kutoka kwa Ibnu Omar R.A, amesema: Mtu mmoja (alibeua) alitoa sauti ya shibe mbele ya Mtume S.A.W, akasema Mtume: Jizuie kubeua mbele yetu kwani wale washibao sana Duniani ndio wenye njaa ya muda mrefu zaidi siku ya Kiama. Na kitendo hicho cha kubeua ingawa sio cha haramu, lakini kinapingana maadili ya Watu wote, na zaidi ya hayo; watu huwaudhi wengine kwa kula kwao vyakula vya haramu ambavyo husababisha harufu mbaya itoke midomoni mwao au katika mavazi yao na vile vile kwa kuchunga Hisia za Watu wote kwa kila kinachotoka kwa mtu, kama kitendo, kauli au kitu kingine chochote. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْؤُولًا}

Hakika masikio, na macho, na moyo – hivyo vyote vitasailiwa.

Na katika Maadili hayo ni: kusema na Watu kwa kauli nzuri na kuchagua maneno ya kuyatamka. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَقُل لِّعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنزَغُ بَيْنَهُمْ  إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوًّا مُّبِينًا}

Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet’ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet’ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu.

Na Mtume S.A.W, anasema: Neno zuri ni sadaka.

Na kwa ajili hiyo, ni vyema kuyatumia maneno mazuri yasiyowaudhi watu. Bwana wetu Omar bin Khatwaab, R.A, alipita kwa watu waliokuwa wameuwasha moto, hakupenda kuwasalimia kwa kusema: Asalaamu Alaikum enyi watu wa Moto; bali aliwasalimia kwa kusema: Asalaamu Alaikum enyi watu wa mwangaza.

Na katika Maadili hayo ni: mtu kuyaheshimu ya wengine na kutoyaingilia yasiyomuhusu. Katika jambo hili, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا}

Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo – hivyo vyote vitasailiwa.

Na Mtume wetu anasema S.A.W: Katika Uzuri wa Uislamu wa Mtu ni yeye kuyaacha yasiyomuhusu.

Ninaposema kauli yangu hii na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu msamaha kwa ajili yangu na kwa ajili yenu.

*        *        *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa viumbe vyote. Na ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine yoyote anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu asiye na mshirika wake, na ninashuhudia ya kwamba Bwana wetu Muhammad na Mtume wetu ni Mja na Mjumbe wake. Ewe Mola wetu Mlezi tunakuomba umswalie umrehemu na umbariki yeye na Jamaa zake na Maswahaba wake wote, na atakaye wafuata mpaka siku ya Mwisho.

Ndugu zangu Waislamu:

Hakika miongoni mwa nguzo muhimu za Maadili Makuu yanayochangia kuiendeleza jamii yoyo ni: Kuwa na haya. Na hii ni tabia ya kiislamu yenye hadhi ya juu na kumzuia mwenye nayo kufanya anayoweza kulaumiwa kwayo na humpelekea kujiepusha na kila lisilopendeza, na humukinga na sifa ya kupuuzia. Mtume S.A.W, alibainisha kwamba Haya ni katika tabia zilizoletwa na vitabu vyake Mwenyezi Mungu Mtukufu vilivyotangulia, ambapo anasema Mtume wetu S.A.W: Hakika miongoni mwa waliyoyadiriki watu kutoka katika Utume wa Mwanzo ni: Kama ukishindwa kuwa na haya basi fanya utakavyo.

Na Mtume wetu S.A.W, alipopitia kwa mmoja wa Answaar (Maswahaba wa Madina), huku swahaba huyo alikuwa nduguye kuhusu Haya, Mtume S.A.W, akasema: Mwache kwani Haya hutokana na Imani.

Na kutoka kwa Abdulahi bin Masuud R.A, alisema: Mtume S.A.W, amesema:

Muoneeni Haya Mwenyezi Mungu Mtukufu ukweli wa kumuonea Haya. Tukasema: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakika sisi tunaona Haya na tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa hilo. Akasema Mtume wetu S.A.W: Sio hivyo bali ni kumuonea Haya Mwenyezi Mungu Mtukufu ukweli wa kumuonea Haya. Nako ni: Kukihifadhi kichwa na yaliyomo kichwani. Na kulihifadhi tumbo na yaliyomo tumboni. Na kuyakumbuka mauti na usiku. Na anayeitaka Akhera huyaacha mapambo ya Dunia. Na atakaye fanya hivyo basi huyo atakuwa amemwonea Haya Mwenyezi Mungu Mtukufu ukweli wa kumuonea Haya.

Na Haya humzuia mtu na maovu. Na mtu asiye kuwa na Haya hana kinga yoyote.

     يَعيشُ المَرءُ ما اِستَحيا بِخَيرٍ ** وَيَبقى العودُ ما بَقِيَ اللِحاءُ

فَلا وَاللَهِ ما في العَيشِ خَـيرٌ  ** وَلا الدُنيا إِذا ذَهَبَ الحَياءُ

إِذا لَم تَخشَ عاقِبَةَ اللَيالـي  ** وَلَم تَـستَحيِ فَاِفـعَـل ما تَشاءُ

Na miongoni mwa nguzo muhimu za Maadili ambazo zina mchango mkubwa katika kustawisha Jamii na kuistaarabisha ni: Kuwa na Sifa nzuri. Kama vile uzuri wa Tabia, kuwafanyia Watu mambo mazuri na kujilinda na machafu na kuulinda ulimi wako kwa lugha unayoitumia na makosa pia yatokanayo na maneno machafu, na kujiepusha kila kisichopendeza. Imesemwa kwamba: Mtu atakaetangamana na watu bila ya kuwadhulumu na akazungumza nao bila kuwadanganya na akawaahidi bila ya kuvunja ahadi yake basi huyo ndiye katika wale waliokamilika kwa Sifa nzuri na uadilifu wake ukadhihirika na undugu wake ukawa ni wajibu na kumsengenya ni haramu.

Na sifa nzuri kwa Mtu humfanya awe na mwonekano mzuri wa nje na wa ndani, kwani yeye humchunga Mola Wake kwa Siri na kwa Dhahiri. Haonekani mwema mbele ya Watu tu kisha anapokuwa peke yake hukiuka na kuyafanya yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Anasema Mtume wetu S.A.W: Nitawajua Watu katika Uma wangu watakaokuja siku ya Kiama wakiwa na mema mfano wa majabali ya Tihama yaliyo meupe, na kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akayafanya hayana faida yoyote kwake. Hao ni ndugu zenu na ni wenzenu, wanauchukua usiku kama mnavyouchukua isipokuwa wao ni watu ambao wanapokuwa peke yao hukiuka na kuyafanya aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ama kupambana na Sifa njema kwa Watu huwa kwa kuwasaidia wao, na kuyapupia masilahi yao, na kwamba mtu awapendelee wengine kile anachokipendelea kwa nafsi yake. Anasema Mtume wetu S.A.W: Muislamu ni ndugu wa Mwislamu mwenzake asimdhulumu nduguye, na asimsaliti, na atakayemtatulia tatizo lolote ndugu yake, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu humtatulia yeye tatizo lake. Na mwenye kumwondolea uzito Mwislamu, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamwondoshea na yeye mazito ya Siku ya Kiama. Na atakaye msitiri mwislamu, Mwenyezi Mungu Mtukufu atamsitiri yeye Siku ya Kiama.

Na anasema Mtume wetu S.A.W: Watu Wapendwao sana na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni wale wenyekuwanufaisha wenzao. Na Tendo bora katika Matendo bora kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni furaha inayoingizwa kwa nduguyo Mwislamu, au ukamwondolea jambo zito, au ukamlipia deni lake au ukamwondolea njaa, na kutembea na ndugu yangu mwenye njaa (kwa ajili ya kutatuliwa) ni bora kuliko kukaa itikafu mwezi mzima katika Msikiti huu. Kwa maana ya Msikiti wa Madina!

Uislamu umepitisha mjumuiko wa Adabu zenye hadhi ya juu ambazo kama Uma wowote utashikamana nazo basi utafikia Kiwango cha juu cha ustawi, maendeleo na Ustaarabu. Na huo ndio mfumo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu usiobadilika wala kubadilishwa. Uzuri ulioje kwetu sisi kama tutazichukua Adabu hizi na kuzitekeleza ipasavyo kimwenenendo baina yetu, tukajiandaa katika Dunia na Akhera yetu.

Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, tunakuomba utuoneshe yanayotufaa katika Dunia na Akhera yetu, na utuwafikishe na yale yanayozifaa nchi zetu, na uilinde nchi yetu, wananchi wake na jeshi lake la Ulinzi na la Usalama.