Uisilamu ni dini ya ujenzi na ya uimarishaji
21 Rabiu L awal 1437H. Sawa na 1 Januari 2016 A.D.

awkaf-

 

Kwanza: Vipengele

 1. Kuimarisha ardhi ni jambo litakiwalo kisheria.
 2. Wito wa uisilamu katika ujenzi na uimarishaji wa ardhi.
 3. Kufanya vizuri kazi ni njia ya kuinuka kwa umma na raia
 4. Uisilamu unakataa aina zote za uvivu.
 5. Onyo la kubomoa na kufanya ufisadi katika ardhi.

Pili: Dalili

Ndani ya Kurani Tukufu

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: { Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo.}( 61)

 1. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Yeye ndiye aliyedhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa} (Almulk. 15)
 2. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu} (Muzammil. 20)
 3. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: { Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda} ( 105)
 4. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa.. na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema za ya Mwenyezi Mungu iko karibu na wanaofanya mema} (Al Aaraf. 56)
 5. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa} (Al maidah. 33)

Ndani  ya Hadithi za Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake)

Kutoka kwa Miqdam (Mwenyezi Mungu amwie radhi), kwamba Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “ Hakula mtu chakula bora kuliko alichochuma kwa kazi ya mikono yake, na hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu Daudi (juu yake rehma na amani) alikuwa akila kutokana na kazi za mikono yake. (Imepokewa na Bukhari)

 1. Na kutoka kwa Abdalla bin Abbas (Mwenyezi Mungu awawie radhi) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) “ atakaepambazukiwa hali ya kuwa amejitosheleza kutokana na kazi ya mkono wake basi amepambazukiwa hali ya kuwa amesamehewa. (Muujam Alwasiyt).
 2. Kutoka kwa Abi Hurayra (Mwenyezi Mungu amwie radhi) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) kujifungia mmoja wenu mzigo wa kuni juu ya mgongo wake ni bora kuliko kuomba mtu mwengine sawa ampe au amkatalie. (Imepokewa na Bukhari)
 3. Kutoka kwa Abi Hurayra (Mwenyezi Mungu amwie radhi) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) “mwenye kumhudumikia mjane au masikini, hupata malipo sawa na waipiganiao dini ya Mwenyezi Mungu, au anaesimama usiku kusali na kufunga mchana. (Imepokewa na Bukhari)
 4. Kutoka kwa Anas Bin Malik (Mwenyezi Mungu amwie radhi) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) iwapo kitasimama kiama na kwenye mkono wa mmoja wenu ana mche, kama ataweza kutosimama kabla ya kuipanda, basin a aipande. (Imepokewa na Bukhari)
 5. Kutoka kwa Ka`ab bin U`jrah (Mwenyezi Mungu amwie radhi). Kuna kijana alipita mbele ya Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake), masahaba wa Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) wakaona kwenye ngozi yake ukakamavu na ucheshi wake kitu ambacho kiliwavutia. Wakasema: “ ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu unaonaje lau kama kijana huyu angelikuwa anapigania njia ya Mwenyezi Mungu!! Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) akasema: “ iwapo  anawatafutia riziki watoto wake, basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na iwapo ametoka kuwatafutia riziki wazazi wake wawili watu wazima basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na  iwapo  ametoka  kwa ajili ya nafsi yake ili  kujikinga na haramu, basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu, na ikiwa ametoka kwa ajili ya kuitafutia familia yake riziki basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na  kama  ametoka kutafuta riziki kwa ajili ya kujifaharisha na kujilimbikizia basi atakuwa yupo katika njia ya shetani. (Imepokewa na Attabari).
 6. Kutoka  kwa Anas bin Malik (rehma na amani zimshukia juu yake) amesema: Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) alikuwa akisema “Ewe Mola angu, hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na kushindwa, uvivu, woga, ukongwe, ubakhili. Na ninajikinga kwako na adhabu za kaburi na fitina za uhai na umauti.” (Imepokewa na Muslim).

Maudhui

Hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu katika umbile bora zaidi, akamtukuza kuliko viumbe wengine, na kumdhalilishia ulimwengu kila kilichopo ulimwenguni. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba} Al Israa, 70. Pia amesema: {Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi.} Al baqara 29.

 Na ikapelekea ukarimu huu na neema hii kuwa ndio sababu ya ukhalifa katika ardhi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua} (Al baqara 30). Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akamwekea mwanadamu mipaka na kumpa jukumu kubwa kuhusu ibada nalo ni kumtaka  aiimarishe ardhi, na atowe hazina zake na vyenye thamani. Akasema { Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. } (Hud, 61.) Ikiwa na maana, amewatakeni kuijenga ardhi na kuiimarisha, na kuangalia vile alivyokupeni katika kheri na katika vyakula.

Mwenyezi Mungu amemuamrisha mwanadamu atafute na awe na sababu ya kutafutia riziki, na kuacha kujibweteka na kupiga uvivu kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu amesema { Yeye ndiye aliyedhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake.  Na kwake Yeye ndio kufufuliwa} (Almulk.15).

Na katika kufanya kazi hakuna wakati maalumu, mwanadamu hana budi kufanya kazi hadi mwisho wa pumzi zake, kuthibisha hilo, Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) anasema katika hadithi aliyoipokea Anas Bin Malik (Mwenyezi Mungu amwie radhi) amesema: amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) Kutoka kwa Anas Bin Malik (Mwenyezi Mungu amwie radhi) amesema: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) iwapo kitasimama kiama na kwenye mkono wa mmoja wenu ana mche, kama ataweza kutosimama kabla ya kuipanda, basi na aipande. (Imepokewa na Bukhari). Dini ya kiisilamu inatukuza sana ujenzi, na kuimarisha na inalingania hasa vitu hivi, hata iwapo katika wakati wa dhiki, kwani kuimarisha ni miongoni mwa sababu kuu za maendeleo ya umma na jamii.

 Uisilamu unazingatia sana elimu na mafunzo yote yanayoshikamana na kuijenga ardhi na kuimarisha dunia, ikawahimiza wafuasi wake kutembea katika pembe zake, na kujitafutia riziki zao baharini na nchi kavu pia, pamoja na kuhimizwa kufanya kazi. Inathibiti haya kutoka kwa hadithi ya Miqdam (Mwenyezi Mungu amwie radhi), kwamba Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “ Hakula mtu chakula bora kuliko alichochuma kwa kazi ya mikono yake, na hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu Daudi (juu yake rehma na amani) alikuwa akila kutokana na kazi za mikono yake”. (Imepokewa na Bukhari).

Uisilamu ni wito ulio wazi wa kufanya kazi ambazo zitapelekea kuimarisha na kujenga ili manufaa yarudi kwa ulimwengu mzima.

Kwa ajili hiyo: Uisilamu umeingalia kazi kwa mtazamo usio na mzaha na kuitukuza pia, na kunyanyua thamani ya kazi na kuifanya kuwa ndio sababu ya maeneleo. Na pia kuifanya kuwa ni ibada ambayo mtu hupata malipo. Aya za Kurani Tukufu zimehimiza kufanya kazi na kuishi. Likaja agizo la kutaka watu watawanyike katika ardhi kwa ajili ya kutafuta riziki baada ya amri ya kusali. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Na itakapokwisha sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa} Jumaa, 10.

Na Sayyidna I`rak Bin Malik (Mwenyezi Mungu amwie radhi) akishasali sala ya Ijumaa husimama mbele ya mlango wa msikiti, kisha husema “ewe Mola wangu hakika nimeitikia wito wako na nimekishasali faradhi yako, na ninaondoka kama ulivyoniamrisha, niruzuku katika fadhila zako kwani wewe ni mbora wa wanaoruzuku.”

Na kwa kutokana na umuhimu wa kazi kwa ajili ya kuimarisha na kujenga, aya nyingi ndani ya Kurani Tukufu zimezungumzia kuhusu kazi, vilevile hadithi za Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) zipo nyingi zilizoweka wazi jambo hili na kuhimiza na kutia shime kuhusu kazi, na kuacha kupiga uvivu na kujibweteka. Na kuweka wazi kuwa kufanya kazi ni kijiondoshea udhalilifu na kuwa na heshima na utukufu. Imepokewa na Abi Hurayra (rehma na amani zimshukia juu yake) amesma: amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimshukia juu yake) “kujifungia mmoja wenu mzigo wa kuni juu ya mgongo wake ni bora kuliko kuomba mtu mwengine sawa ampe au amkatalie. (Imepokewa na Bukhari). Na Sufyan Thawriy (Mwenyezi Mungu amrehemu) akipita kwa baadhi ya watu wakiwa wamekaa ndani ya msikiti wa mtukufu, huwaambia: “ ni nini kilichowafanya mukae? Nao hujibu: “Tufanye nini sasa!? Nae husema: tafuteni fadhila za Mwenyezi Mungu na wala musiwe waombaji kwa waisilamu.

Uisilamu umeweka wazi kuwa, yeyote atafutae maisha ya halali kwa ajili ya wanawe anahesabiwa kuwa yupo katika mashahidi na aliyefungamana na njia ya Mwenyezi Mungu. Imepokewa na Kutoka kwa Ka`ab bin U`jrah (Mwenyezi Mungu amwie radhi). Kuna kijana alipita mbele ya Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake), masahaba wa Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) wakaona kwenye ngozi yake ukakamavu na ucheshi wake kitu ambacho kiliwavutia. Wakasema: “ ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu unaonaje lau kama kijana huyu angelikuwa anapigania njia ya Mwenyezi Mungu!! Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) akasema: “ iwapo  anawatafutia riziki watoto wake, basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na iwapo ametoka kuwatafutia riziki wazazi wake wawili watu wazima basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na iwapo ametoka kwa ajili ya nafsi yake ili kujikinga na haramu  , basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu, na ikiwa ametoka kwa ajili ya kuitafutia familia yake riziki basi yupo katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na kama ametoka kutafuta riziki kwa ajili ya kujifaharisha na kujilimbikizia basi atakuwa yupo katika njia ya shetani. (Imepokewa na Attabari).

Na uisilamu haukutosheka kuwalingatia wafuasi wake kufanya kazi tu pekee kama ndio njia ya maendeleo, bali pia umewataka wafanye kazi kama itakiwavyo –wawe na ikhlasi- kwa ajili ya kupata mapenzi ya Mwenyezi Mungu na rehema zake. Imepokewa kutoka kwa Aisha (rehma na amani zimshukia juu yake). Kwamba Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) amesema: “ Hakika Mwenyezi Mungu – Mtukufu – anapenda mmoja wenu akifanya kazi aifanye vizuri.” (imepokewa na Tabbariy).

Kufanya kazi itakiwavyo na kuijali na kuihifadhi ni katika misingi ambayo uisilamu unataka ifuatwe, nayo ni lengo miongoni mwa malengo ya dini, humtukuza muisilamu kupata radhi za Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu huwa hakubali kazi isipokuwa ile iliyofanywa kwa ajili yake, kwani Mwenyezi Mungu ameumba kila kitu kwa uangalifu sana, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo} (Annaml, 88).

Na uisilamu ukahimiza kufanya vizuri na ipasavyo na kukataza kufanya ufisadi, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema} (Al baqara.195). Na akasema {Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.} (Al qasas.77).

Aya nyingi za Kurani Tukufu zimetaka mtu akifanya kazi basi aifanywe katika njia sahihi hii kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu, kusaidiana katia ya mtu na jamii, na akaahidi malipo makubwa sana na kumsifia sifa njema hapa duniani na kesho akhera. Na akaweka wazi kuwa mwanaadamu hatoacha kuwa anafanya kazi ilivyokuwa yupo chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu, mjuzi wa vilivyofichikana kifuani, Naye kwake hakifichiki hata kilicho kidogo sana katika matendo ya waja. Mwenyezi Mungu tawadhihirishia kwa kuwa amekisajili na atawalipa kwa hicho siku ya watakayokutana. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur’ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi} (Yunus. 61).

Mwenyezi Mungu Mtukufu ndie anayemchunga mwanadamu katika kazi zake, na humuona akiwa kiwandani, kondeni na hata katika biashara zake sehemu ambazo hufanyia kazi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema { Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.} (Tawbah. 105). Amri ya hapa ni kama walivyosema wafasiri: kuna kuogopesha: ikiwa na maana: matendo yenu hayafichikani mbele ya Mwenyezi Mungu na wala kwa Mtume wake wala kwa waumini, basi harakisheni kutenda mema, na fanyeni kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na pia kuna  – katika aya hii – bishara na kuhamasishwa, kwani iwapo mtu ataelewa kuwa matendo ayatendayo sawa ni mabaya au mazuri Mwenyezi Mungu ndie ayaonae, basi atakuwa na shime ya kuyakimbilia matendo mema, na kujiepusha na mabaya, na maneno mazuri yaliyoje ya mshairi Zuhayri:

Mtu akiwa na tabia ya aina yoyote * hata kama ataificha, basi watu wataijua”

 Pia imekuja katika hadithi za Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) zenye kuhimiza kufanya kazi kama itakiwavyo na kuimarisha kwa ajili ya kufikia kilicho bora na kizuri. Kwa mfano katika upande wa kuabudu kupitia ibada ya sala ambayo ninguzo kati ya mja na Mola wake, inatakiwa imamu wao awe mwenye ujuzi kuliko wote na awe anaisoma Kurani Tukufu vizuri, pia awe anaisoma kwa kuizingatia, ili ajumuike na wale waliobashiriwa na Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) kuwa atakuwapo pamoja na malaika wakarimu. Na vilevile kwa asimamiaye masuala ya maiti, Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) anasema: “ Mmoja wenu akimveka sanda maiti basin a amvike vizuri” (Imepokewa na Muslim).

Kutoka kwa A`swim Bin Kulayb Al jaramiy amesema: Baba yangu Kulayb amenihadithia kwamba yeye amehudhuria jeneza pamoja na baba yake alipokuwepo Mtume na mimi kipindi hicho ni mdogo mwenye akili na ufahamu, wakamaliza kusalia jeneza wakaenda makaburini walipomlaza, akasema, Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) akawa anasema “uwekeni vizuri mwanandani huu”. Mpaka watu kakadhania kuwa ni sunna, nikawageukia, akasema: “ Ama huu haumfai maiti na wala haumdhuru, isipokuwa Mwenyezi Mungu hupenda kwa mtenda kazi akifanya kazi basi aifanye vizuri.” (Imepokewa na Bayhaqiy).

Kazi yoyote aitendayo mwanadamu ni lazima aifanye vile itakiwavyo, amchunge Mwenyezi Mungu katika kazi hiyo, kwani Yeye Mwenyezi Mungu humuona mja huyo na kilichomo ndani ya moyo wake na atawahesabu juu ya matendo yao makubwa au madogo, mengi au machache.

Ama kwa wale ambao hawafanyi itakiwavyo kazi zao na wala hawamchungi Mwenyezi Mungu, hupata madhambi mengi kwa kadiri ya madhara atakayoyasababisha ya kupoteza mali na nguvu. Mfanya kazi ambaye hatimizi wajibu wake na huzembea na wala hafanyi kazi kama alivyoagizwa na akatosheka kujiridhisha yeye mwenyewe na akawa anapokea mshahara, huyu huwa anapokea mshahara wa haramu na watu watakwenda kudai madai yao siku ya kiama. Na yeyote ambae hii ndio sifa yake basi aelewe kuwa anabeba jukumu la kutokuendelea kwa umma na kuonekana kuwa upo nyumba kimaendeleo. Hatutoacha kumshtakia mbele ya Mwenyezi Mungu. Sayidna Omar (Mwenyezi Mungu amwie radhi) anasema: “namshtakia Mwenyezi Mungu kutokana na udhaifu wa kiongozi na ukhaini wa mwenye nguvu.”

Hakika uisilamu umepiga vita aina zote za kukata tama na uvivu ambao hausaidii kitu katika kujenga na kuimarisha. Na ukaifanya sifa ya uvivu kuwa ni sifa chafu, Mwenyezi Mungu amewakashifu wavivu kwenye kitabu chake kitukufu na kusema kuwa ni sifa za wanafiki, akasema {wala hawaji kwenye Sala ila kwa uvivu, wala hawatoi michango ila nao wamechukia} (Atawba. 54).

Uvivu ni njia mbaya na ni maafa makubwa yenye kuangamiza yenye kuharibu taifa na raia zake na pia hupelekea kutoendelea na kuonekana taifa lililo nyuma kimaendeleo. Nao ni ugonjwa hatari, mtu akiwa nao basi anaweza hata kupoteza utu wake. Imamu Raghib amesema: “ajiewekae bila kazi hujivua ubinaadamu na kujiweka kuwa mnyama, na hufikia pia kuwa kama maiti”.

Kwa ajili hiyo Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) akajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na uvivu na unyongonyevu, imepokewa kutoka kwa Anas bin Malik (rehma na amani zimshukia juu yake) amesema: Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) alikuwa akisema “Ewe Mola angu, hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na kushindwa, uvivu, woga, ukongwe, ubakhili. Na ninajikinga kwako na adhabu za kaburi na fitina za uhai na umauti.” (Imepokewa na Muslim).

Na Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) amelinganisha kati ya uvivu na ukongwe kwa sababu kila moja katika hivi viwili humfanya mtu kuwa mzito wa kutimiza wajibu aliotakiwa autimize.

Uvivu ni maafa yatokayo moyoni, na kizuizi chenye kuzuia kutimiza wajibu, hudhoofisha utashi, hupelekea kwenye ufakiri, na ni vimelea vyenye kuua, maradhi yenye kuangamiza, hudhoofisha ukuaji wa taifa na watu wake, na huzuia watu wasifanye kazi kwa bidii na kuyatafuta manufaa.

Uisilamu umeutia dosari uvivu na kutahadharisha kutokuwa nao, kwani una kuzembea katika mambo yasiyopasa kuzembewa, na kupelekea kujiweka mbali na

yaliyo muhimu na kuhisi kama kwamba ni sumu au kitu cha kuchukiza Mwenyezi Mungu atuepushe nao. Na –uvivu- humfanya mtu achukie mazuri kutokana na udhaifu wake wa kufuatilia, na humfanya aache yaliyo wajibu, kweli ni maafa yasiyoleta mafanikio, humsambaratisha kila aliye nao, na humfanya mvivu kuwa mwenye kutegemea wengine, asiye na uwezo wa kuchukua jukumu kama mtu kamili. Na hatari yake huenea kwa mmoja moja na hata kwa jamii nzima. Imamu Ali (Mwenyezi Mungu amwie radhi) anasema: Kuzembea ni ufunguo wa kukatisha tamaa, ulegevu na uvivu huleta maafa, na huzalisha maangamizo, asiyetafuta huwa hapati na pia hupelekea katika maovu.

 Uvivu si katika mambo yatakiwayo katika uisilamu na wala hauna thamani, kwani uisilamu hufukuzia mema na kuimarisha ulimwengu, ama wavivu wao hubomoa ustaarabu na huharakisha kubomoa aina zote nyengine za ustaarabu.

 Haya ni miongoni mwa mambo ambayo uisilamu umeyapiga vita, na ambayo katu hayajengi na kuimarisha ulimwengu na huleta ufisadi katika ardhi na kuiharibu nayo ni tabia yenye kudhalilisha iwapo atakuwa nayo mwanadamu. Tabia hii huwa hawawi nayo isipokuwa wanafiki pekee ambao Mwenyezi Mungu amesema. {Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu} (Al maida 64). Na anasema {wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu} (Al baqara. 60).

 Ufisadi upo wa aina nyingi, na ulio mbaya zaidi ni ule unaotumia jina la dini, umma umefikwa na mitihani kwa sababu ya ufisadi hali ya kuwa dini haihusiki kabisa. Huuwa, hujihalalishia mali na kuvunja heshima kwa jina la dini. Watu hawa Mwenyezi Mungu amewakashifu ndani ya kitabu chake akasema {Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu 205. Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi. 206. Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa mapumziko.} (Al baqara 204-206).

 Ufisadi kwanamna zake zote huyumbisha ukuaji na maendeleo ya taifa, na hueneza mabaya na kupelekea kutojali majukumu. Kwa ajili hiyo, hakuna budi kupinga ufisadi na wafanyao ufisadi. Kuupinga ufisadi ni kwa manufaa ya jamii nzima. Na kuzembea bila ya kuupinga ni maangamizo kwa jamii nzima. Imepokewa kutoka kwa Nuuman Bin Bashir (Mwenyezi Mungu awawie radhi), kwamba Mtume (Rehma na amani zimshukie juu yake) alikuwa akisema: “Mfano wa asimamiaye mipaka ya Mwenyezi Mungu na aliyeivuka ni mfano wa watu waliojazana kwenye marikebu, wengine wakawa wapo juu na wengine chini, wale waliopo chini wakiwa wanataka maji huwafuata wale waliopo juu, kisha huwaambia lau kama sisi tungelichukua fungu letu na wala tusingelikukereni mliopo juu. Iwapo –wa juu- wangeliwaacha na kile watakacho basi wangelizama wote na wangeliwapa watakacho basi wangeliokoka wote pamoja.” (Imepokewa na Bukhari).

Hakuna budi kusaidiana, kuwa pamoja na kushikamana kati ya waisilamu ili imani ipatikane pamoja na undugu wa kiisilamu.

Kuisafisha ardhi na wafanyao ufisadi , na kulinda njia na taasisi ni katika mambo mema na mazuri. Mwenyezi Mungu huwakinga wafanyao ufisadi kwa kuwepo watu wema, amesema {Basi mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanao kataza uharibifu katika nchi, isipo kuwa wachache tu, ambao ndio tulio waokoa? Na walio dhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni wakosefu} (Hud. 116). Kwani ufisadi ni ubomoaji wa jamii na hakuna njia ya kujiokoa nao isipokuwa kuuzuia.

Na umma wa kiisilamu kwa fadhila zake Mwenyezi Mungu una kheri nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Kuna bahari, maziwa, mito mikubwa, ndani ya ardhi muna madini yanayoitajika katika ulimwengu wetu wa kisasa, pia unamiliki hazina kubwa ya mafuta ulimwenguni, ukizidisha thamanikubwa ya akili na fikira na watendaji kazi. Kwa ajili hiyo umma hauna budi kuweka vitega uchumi vilivyo bora, na pia kutumia wakati katika yenye kuleta manufaa kwa watu, na kwa njia ya kuinua ustaarabu na maendeleo ya kielimu.

Umma wetu ni wa kazi na si wa kupiga uvivu, umma wa kujenga si wa kubomoa na kuharibu, umma wenye ustaarabu, na kutoendelea si sifa isifikayo katu kwa umma huu, ni juu ya kila muisilamu mwenye kuipenda dini yake na kujifaharishia nayo atende kwa ajili ya kuiinua dini yake na kuliinua taifa lake.