Unafiki na Hiana na hatari zake kwa Watu na Nchi

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola wa viumbe vyote. Mwenyezi Mungu Mtukufu anaesema katika Kitabu chake Kitukufu:

{الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُمْ مِنْ بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمُنْكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ وَيَقْبِضُونَ أَيْدِيَهُمْ نَسُوا اللَّهَ فَنَسِيَهُمْ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ هُمُ الْفَاسِقُونَ}

{Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanaafiki ndio wapotofu}.

Na ninashuhudia kuwa hakuna Mungu mwingine anaestahiki kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, peke yake asiyekuwa na Mshirika wake. Na ninashuhudia kuwa Bwana wetu, Mtume wetu na Kipenzi chetu Muhammad, ni Mja wake na Mtume Wake, anaesema katika Hadithi Tukufu

     : ” آية المنافق ثلاث:إذا حدث كذب,وإذا وعد أخلف ,وإذا ائتمن خان” Alama za Mnafiki ni tatu: anapozungumza husema uongo, na anapoahidi huvunja ahadi, na anapoaminiwa hufanya hiana. Ewe Mola wetu mswalie na umrehemu na umbariki Bwana wetu Muhammad, na Jamaa zake na Maswahaba wake, na kila mwenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.أما بعد

Na baada ya hayo:

Jambo ambalo halina shaka ndani yake ni kwamba unafiki ni ugonjwa hatari, na ni janga linaloshambulia, na ni angamizi kwa watu na mataifa. Ni katika magonjwa hatari ya moyo ambayo hushambulia Imani ya kweli na hubomoa misingi yake na kuziangusha nguzo zake. Na ni janga la kijamii na la kimaadili lililo hatari mno ambalo huibomoa jamii, amani na utulivu wake; na kwa ajili hii, hakika hatari yake ni zaidi ya ukafiri na ushirikina; kwani ugonjwa wa Unafiki unapoingia katika mwili wa Umma huinyonya na kuikongoa mifupa yake, na huligawa neno la pamoja la Umma.

Vile vile silaha ya haini na kutumiwa ndivyo hatari zaidi vinavyoendelea kutishia mfumo mzima wa nchi na uwepo wake katika kipindi chote cha historia ambayo inazingatiwa kuwa ni ushahidi mzuri wa kwamba nchi zote zilizozorota na kuvunjika vunjika hadi kuteketea kabisa ukweli ni kwamba ziliangamizwa kwa ndani, na wahaini wote na watumiwa na mamluki walitoa mchango mkubwa dhidi ya nchi zao katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu. Kwa hivyo, daima hatari zinazozitishia nchi kutokea ndani ya nchi hizo ni hatari zaidi kuliko hatari ambazo zinazitishia nchi hizo kwa nje.

Sisi tunapaswa kutambua kwamba Unafiki uko wa aina mbili: Unafiki Mkubwa na Unafiki Mdogo. Katika aina hizi mbili, Unafiki Mkubwa ni hatari zaidi, nao ni wa Itikadi ambapo aliyenao hudhihirisha Uislamu na huficha ukafiri alionao ndani yake. Na aina hii, aliye nao hudumu milele Motoni, bali huwekwa katika daraja la Chini zaidi la Motoni. Na Unafiki wa aina ya Pili: Unafiki Mdogo: Nao ni ule wa kivitendo ambao ni kukengeuka katika mwenendo. Na kujivesha kitu chochote ni katika alama za wanafiki. Nako ni mtu kudhihirisha Uzuri na kuyaficha yote yaliyo kinyume na hivyo, na aina hii haimtoi mtu kikamilifu katika Dini; isipokuwa ni njia ya  kuelekea katika Unafiki Mkubwa ikiwa Muhusika hatatubu.

Hakika Qurani tukufu imetuhadithia, na Sunna ya Mtume S.A.W iliyotwaharika imetuhaidithia kuhusu wanafiki na sifa zao pamoja na tabia zao na sumu zao. Hatujawahi kuziona sifa hizo zinabadilika katika zama zozote, au kutofautiana kwa tofauti ya nchi. Na miongoni mwa alama muhimu zinazowatambulisha wanafiki ni:

* الكذب، وخلف الوعد، وخيانة الأمانة، والفجور في الخصومة

Uongo, kwenda kinyume na ahadi au miadi, na kufanya hiana katika kuaminiwa, na ukorofi katika ugomvi: Nazo ni sifa mbaya mno katika sifa za Wanafiki ambazo Mtume S.A.W amewasifu kwazo Wanafiki, nayo ni katika unafiki wa vitendo alioufafanua Mtume S.A.W, pale aliposema  : حيث قال : (أَرْبَعٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ كَانَ

 مُنَافِقًا خَالِصًا ، وَمَنْ كَانَتْ فِيهِ خَصْلَةٌ مِنْهُنَّ كَانَتْ فِيهِ خَصْلَةٌ مِنْ النِّفَاقِ حَتَّى يَدَعَهَا :

إِذَا اؤْتُمِنَ خَانَ ، وَإِذَا حَدَّثَ كَذَبَ ، وَإِذَا عَاهَدَ غَدَرَ ، وَإِذَا خَاصَمَ فَجَرَ).

) Mtu ambaye atakuwa na sifa hizi nne basi atakuwa Mnafiki Mtupu. Na atakayekuwa na yoyote katika hizo basi atakuwa na sehemu ya unafiki mpaka aiache: Anapoaminiwa hufanya hiana, na anapozungumza husema uongo, na anapoahidi huvunja ahadi yake, na anapogombana na mtu hufanya uovu).

 Mtu yoyote ambaye sifa hizi nne zitamkusanyikia, au moja kati yake, basi anakuwa Mnafiki mtu huyo, na sifa hizi zote huyavuruga masilahi ya Umma na hulenga katika kuyabomoa kabisa.

Mara nyingi huwa tunaona Mtu Mnafiki anasema Uongo ili amfikirishe mwingine kuwa yeye ni mkweli katika kauli na kvitendo vyake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يُعْجِبُكَ قَوْلُهُ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيُشْهِدُ اللَّهَ عَلَى مَا فِي قَلْبِهِ وَهُوَ أَلَدُّ الْخِصَامِ}

{Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu}.

Unapotajwa Unafiki, Udanganyifu na Hiana ya kuaminiwa katika Qurani tukufu, hutajwa pamoja na Uongo. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يُخَادِعُونَ اللَّهَ وَالَّذِينَ آَمَنُوا وَمَا يَخْدَعُونَ إِلَّا أَنْفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ * فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّهُ مَرَضًا وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ}،

{Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui. Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema kwao uwongo}.

Mtume S.A.W ametuonya kuhusu Uongo kwa kutuwekea wazi athari zake mbaya aliposema:

  (وَإِيَّاكُمْ وَالْكَذِبَ فَإِنَّ الْكَذِبَ يَهْدِي إِلَى الْفُجُورِ، وَإِنَّ الْفُجُورَ يَهْدِي إِلَى النَّارِ، وَمَا يَزَالُ الرَّجُلُ يَكْذِبُ وَيَتَحَرَّى الْكَذِبَ حَتَّى يُكْتَبَ عِنْدَ اللَّهِ كَذَّابًا)

( Uepukeni Uongo, kwani hakika ya Uongo hupelekea katika Uovu, na hakika ya Uovu hupelekea Motoni, na Mtu huendelea kudanganya na kujipamba na uongo mpaka kaandikiwa kwa Mwenyezi Mungu kuwa yeye ni Mwongo).

Na Mtume S.A.W aliulizwa: Je Muumini anaweza kuwa mwoga? Akasema: ndio. Akaambiwa: Je Muumini anaweza akawa Bakhili? Akasema: Ndio. Akaulizwa: Je Muumini anaweza akawa mwongo? Akasema: Hapana. Na Abu Bakari R.A ameupa uongo sifa ya hiana, katika kauli yake: Ukweli ni Uaminifu na Uongo ni Hiana

 Pia Uhaini na Utumiwaji (الخيانة والعمالة) ambavyo hupelekea kukata mahusiano ya upendo, na kubaguana hupelekea migogoro na migawanyiko, na kuvurugika kwa mahusiano. Na Mtume S.A.W amebainisha kuwa hiana ya kuaminiwa huwa fedheha kwa muhusika siku ya Malipo: Pindi Mwenyezi Mungu atakapowakusanya wa Mwanzo na wa Mwisho pamoja, Siku ya Kiama, kila aliyevunja ahadi atavuliwa vazi na patasemwa: Huu ni uvunjaji wa ahadi wa Fulani bin Fulani. Na Mtume S.A.W atakuwa Mgomvi wake Siku ya Kiama, ambapo amesema:

حيث قال : (ثَلَاثَةٌ أَنَا خَصْمُهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ، وَمَنْ كُنْتُ خَصْمَهُ خَصَمْتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ : رَجُلٌ أَعْطَى بِي ثُمَّ غَدَرَ ، وَرَجُلٌ بَاعَ حُرًّا فَأَكَلَ ثَمَنَهُ ، وَرَجُلٌ اسْتَأْجَرَ أَجِيرًا فَاسْتَوْفَى مِنْهُ وَلَمْ يُوفِهِ أَجْرَهُ)

 (Watu watatu mimi ni Mgomvi wao Siku ya Kiama, na yule mimi nitakayekuwa Mgomvi wake basi nitamfanyia ugomvi Siku ya Kiama: Mtu aliyeniahidi kisha akavunja ahadi yake, na mtu aliyemuuza Muungwana na akala thamani yake, na mtu aliyemwajiri mwajiriwa akatekeleza wajibu wake lakini hakumlipa ujira wake).

Na miongoni mwa aina hatari mno za Uhaini, ni uhaini wa nchi na kuziuza kwa thamani ya chini na kwa ajili ya lengo la Dunia lenye kutoweka kwa mfano wa yafanyavyo makundi yenye misimamo mikali ya kidini na wanaowafuata au wanaopita katika mkumbo wao na mfumo wao katika kuziuza nchi zao kwa thamani duni.

Na miongoni mwa sifa mbaya ambazo Uislamu umetuonya nazo: Ni Uovu katika ugomvi: الفجور في الخصومة. Nao ni mkusanyiko wa aina zote za shari, na ni asili ya kila jambo baya, na ni njia ya kumtoa mtu katika haki, na huifanya haki ikawa batili na batili ikawa haki. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ameusifu Uovu katika ugomvi kama ukubwa wa Ugomvi au uhasimu.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{ وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يُعْجِبُكَ قَوْلُهُ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيُشْهِدُ اللَّهَ عَلَى مَا فِي قَلْبِهِ وَهُوَ أَلَدُّ الْخِصَامِ}

{Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu}.

Na kutoka kwa Bi Aisha R.A, kutoka kwa Mtume S.A.W, amesema:

(إِنَّ أَبْغَضَ الرِّجَالِ إِلَى اللَّهِ الأَلَدُّ الخَصِمُ).

( Hakika watu wasiopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni Wagomvi waliopindukia).

Kwa hivyo Unafiki uko karibu zaidi na wasifu wa hali zao kwa kuwa wao ni wenye nyuso mbili, bali tunawaona katika zama zetu hizi wamepindukia mipaka kwa kiasi kikubwa mno, wakawa sasa wana nyuso zaidi ya elfu moja, nao ni katika watu wa shari zaidi katika viumbe. Anasema Mtume S.A.W: Mtawakuta watu walio na Shari zaidi ni wale wenye nyuso mbili ambao huja kwa watu hawa kwa uso mmoja na huwenda kwa wengine kwa uso mwingine.

Na katika alama za Unafiki:                            الإفساد في الأرض وادعاء الإصلاح

Ni wao kufanya Ufisadi Duniani na kudai kuwa wanatengeneza:

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika jambo hili:

{وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ قَالُوا إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ * أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْمُفْسِدُونَ وَلَكِنْ لَا يَشْعُرُونَ}

{Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji. Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui}.

Na uharibifu au ufisadi una sura za aina mbali mbali, miongoni mwazo ni: Ni kuzua habari mbaya za kuvunja moyo katika nchi, na kueneza Udhaifu na Unyonge katika nafsi za waumini wa kweli, na kutumbukiza fikra potovu, na mieleweko iliyokengeuka, na kueneza fitina baina ya watu, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu, Msema Kweli:

{لَوْ خَرَجُوا فِيكُمْ مَا زَادُوكُمْ إِلَّا خَبَالًا وَلَأَوْضَعُوا خِلَالَكُمْ يَبْغُونَكُمُ الْفِتْنَةَ وَفِيكُمْ سَمَّاعُونَ لَهُمْ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ}

{Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu}.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَقَالُوا لَا تَنْفِرُوا فِي الْحَرِّ قُلْ نَارُ جَهَنَّمَ أَشَدُّ حَرًّا لَوْ كَانُوا يَفْقَهُونَ}

{na wakasema: Msitoke nje katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una joto zaidi, laiti wangeli fahamu! }

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{قَدْ يَعْلَمُ اللَّهُ الْمُعَوِّقِينَ مِنْكُمْ وَالْقَائِلِينَ لِإِخْوَانِهِمْ هَلُمَّ إِلَيْنَا وَلَا يَأْتُونَ الْبَأْسَ إِلَّا قَلِيلًا}،

{Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu}. Na miongoni mwa sura za Ufisadi: ni kuwanyima watu haki zao, na kuwashusha hadhi.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ}،

{Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi}.

Na miongoni mwa sura zake ni: Kuvunja na Kubomoa, kuwaua wasiokuwa na hatia, na kuwatisha wenye amani, na kuzorotesha masilahi ya watu, na kutotekeleza majukumu ipasavyo, na vile vile rushwa, na upendeleo, na kula mali za watu kinyume na haki. Na uvivu wa kufanya ibada, kujionesha kwa watu\ mtu anapofanya ibada, na hasa katika tendo miongoni mwa matendo yaliyo bora zaidi na yenye kheri nyingi ambalo ni swala.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَى يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُون َاللَّهَ إِلَّا قَلِيلًا}

{Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na hali ni Yeye ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa unyong’onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kidogo tu}.

*******

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَمَا مَنَعَهُمْ أَنْ تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّهِ وَبِرَسُولِهِ وَلَا يَأْتُونَ الصَّلَاةَ إِلَّا وَهُمْ كُسَالَى وَلَا يُنْفِقُونَ إِلَّا وَهُمْ كَارِهُونَ}

{Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa kuwa walimkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala ila kwa uvivu, wala hawatoi michango ila nao wamechukia}.

Na Mtume S.A.W anasema: Hakuna Swala iliyo nzito kwa Wanafiki kuliko Swala yaAlfajiri na Isha, na kama watu wangejua yaliyomo ndani yake basi wangezienda swala hizi hata kwa kutambaa.

Na kutoka kwa Jabir bin Abdillah R.A, anasema: Mtume S.A.W alitoka akasema: Enyi watu. Jiepusheni na Shirki ya Siri, wakamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni ipi hiyo Shirki ya mambo ya ndani? Akasema: Ni Mtu kusimama na kuipamba swala yake kwa juhudi pevu kwa kuona watu wanamwangalia, na hiyo ndio Shirki ya Siri.

Ninaisema kauli yangu hii, na ninamwomba msamaha Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu na kwa ajili yenu.

*       *       *

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote. Na rehma na amani zimwendee Mtume wa Mwisho na Mjumbe wake, Bwana wetu Muhammad, S.A.W, na Jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Ndugu zangu Waislamu: Hakika miongoni mwa alama za Unafiki: Ni kuungana na Maadui na kuwasiliana nao dhidi ya Dini na Taifa, kufanya ujasusi, Kuwa Haini, kunukulu habari na maelezo, na kutoa siri za nchi. Kwa hiyo, mnafiki ni mtumiwa anayewasaidia maadui wa nchi yake dhidi ya watu wake, majirani zake na ndugu zake.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{فَتَرَى الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ يُسَارِعُونَ فِيهِمْ يَقُولُونَ نَخْشَى أَنْ تُصِيبَنَا دَائِرَةٌ فَعَسَى اللَّهُ أَنْ يَأْتِيَ بِالْفَتْحِ أَوْ أَمْرٍ مِنْ عِنْدِهِ فَيُصْبِحُوا عَلَى مَا أَسَرُّوا فِي أَنْفُسِهِمْ نَادِمِينَ}،

{Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema: Tunakhofu yasitusibu mabadiliko. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake wakawa wenyekujuta kwa waliyo yaficha katika nafsi zao}.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَإِنَّ مِنْكُمْ لَمَنْ لَيُبَطِّئَنَّ فَإِنْ أَصَابَتْكُمْ مُصِيبَةٌ قَالَ قَدْ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيَّ إِذْ لَمْ أَكُنْ مَعَهُمْ شَهِيدًا * وَلَئِنْ أَصَابَكُمْ فَضْلٌ مِنَ اللَّهِ لَيَقُولَنَّ كَأَنْ لَمْ تَكُنْ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُ مَوَدَّةٌ يَا لَيْتَنِي كُنْتُ مَعَهُمْ فَأَفُوزَ فَوْزًا عَظِيمًا}

{Na yupo kati yenu anaye bakia nyuma; na ukikusibuni msiba husema: Mwenyezi Mungu kanifanyia kheri sikuwa nao. Na ikikufikieni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema – kama kwamba hapakuwa mapenzi baina yenu naye: Laiti ningeli kuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa}.

Mnafiki hufurahi pale shari inapolifikia taifa na wananchi wake, au fitna ikaenea baina yao, au ubonjwa ukasambaa kwao, au wakavunjika nguvu yao.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنْ تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِنْ تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا وَإِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئاً إِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ}.

{Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo}.

Na Wanafiki wapya, pamoja na kuwa na sifa ya Uongo, Hiana na Kuvunja ahadi, kuvunja mikataba na makubaliano, na kuvuruga Rai ya Umma, na kuifanyia Dini hiana, wao wamejumuisha pia aina mpya ya Udanganyifu, ambapo iliyo wazi zaidi kati ya hizo ni Kuiuza Dini, na kuitumia Dini kwa maslahi ya makundi ambayo yanataka kuifanya Dini kama ngazi ya kupandia katika Uwanja wa Siasa, wakijipamba kwa aina mbali mbali za ufuasi wa juu juu wa Dini, na Udini wa Kisiasa, na kuinasibisha Imani kwao wao na kuikanusha kwa wengine wasio kuwa wao, wakihangaikia kujipatia pazia la kisheria la kazi zao, ukiongezea na kuwa wanafiki hao wapya wana sifa ya Uhaini wa Nchi na chuki dhidi ya nchi na pia kuiuza kwa thamani ya chini. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ameiahidi aina hii ya watu kwamba wao watazungukwa, na kwamba ghadhabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu zitawakumba hapa Duniani na kesho Akhera, na wale wanaopanga njama za kuwatumbukiza Waislamu katika Misukosuko na Matatizo basi vyote hivyo vitawarejea wao wenyewe.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 {وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ}

{Na vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya}.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu na amewaadhibu Wafuasi wa Unafiki Mkubwa kwa kuyumbayumba na kutokuwa na Utulivu, na kupatwa na kihoro na fedheha katika kila jambo lao.

 Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{مُذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَلِكَ لَا إِلَى هَؤُلَاءِ وَلَا إِلَى هَؤُلَاءِ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَلَنْ تَجِدَ لَهُ سَبِيلًا}

{Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na huko hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompatia njia}.

Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ قَاتَلَهُمُ اللَّهُ أَنَّى يُؤْفَكُونَ}

{Wao hudhania kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki? }

Na Mwenyezi Mungu ameziepusha nyoyo zao na Ufahamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W, na kwa hivyo uongofu haufiki katika nyoyo zao, na wala heri yoyote haiwi safi kwao.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{ذلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلى قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لا يَفْقَهُونَ}

{Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote}.

Na kwa upande wa adhabu yao katika Siku ya Mwisho, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{وَمِمَّنْ حَوْلَكُمْ مِنَ الْأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لَا تَعْلَمُهُمْ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ سَنُعَذِّبُهُمْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَى عَذَابٍ عَظِيم}

{Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa}.

Kwa hivyo, Adhabu ya kwanza wanaipata hapa Duniani, na Adhabu ya pili wanaipata Kaburini. Adhabu kubwa itakuwa Siku ya Mwisho, ambapo Mwenyezi Mungu atawakusanya Motoni, Wanafiki wote pamoja na wale waliokuwa nao katika mambo ya Shari.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ اللّهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا}

{Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanaafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannamu}.

 Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَنْ تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا * إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَاعْتَصَمُوا بِاللَّهِ وَأَخْلَصُوا دِينَهُمْ لِلَّهِ فَأُولَئِكَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ وَسَوْفَ يُؤْتِ اللَّهُ الْمُؤْمِنِينَ أَجْرًا عَظِيمًا}.

{Hakika wanaafiki watakuwa katika t’abaka ya chini kabisa Motoni, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru. Isipo kuwa wale walio tubu, na wakatengeneza na wakashikamana na Mwenyezi Mungu, na wakamtakasia Dini yao Mwenyezi Mungu. Basi hao ni pamoja na Waumini. Na Mwenyezi Mungu atakuja wapa Waumini ujira mkubwa}.

Na kwa ajili ya kuilinda nchi na kuvilinda vilivyomo, mshikamano na amani yake, hapana budi kwa kila mwananchi mwenye moyo msafi na mkunjufu, kuwa macho kama mlinzi, mtu mmoja mmoja au taasisi, na hapana budi kukusanya nguvu na juhudi kwa kila mwenye heshima, ili kukata mizizi ya Wahaini na Watumikao na wapelelezi wanaoshirikiana na Maadui miongoni mwa wahalifu, na kuwafedhehesha mbele ya watu wenye kushuhudia, na kuwafanya wakawa zingatio kwa kila mwenyekufikiria kupita njia ya wahaini na watumiwa, , kwa ajili ya kuilinda Dini yetu, nchi yetu na watu wake wote,na kabla ya yote hayo, kumridhisha Mola wetu Mtukufu, na kuzilinda nchi zetu, ili zisije zikapatwa na yale yaliyotokea katika nchi nyingine ambazo zilizembea na kupuuzia katika kupambana na Wahaini na Watumiwa na kudhani kuwa jambo lango ni dogo tu. Na Jambo hili halijawahi kuwa dogo katika historia ya Mataifa mbali mbali.

Ewe Mola wetu zitakase nyoyo zetu na unafiki, na uyatakase macho yetu na Hiana, na uzilinde ndimi zetu na Uongo, na uilinde nchi yetu na watu wake.

اللهم طهر قلوبنا من النفاق ، وأعيننا من الخيانة

وألسنتنا من الكذب، واحفظ بلادنا وأهلنا